Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanajeshi Iran wanafyatulia risasi waandamanaji kutoka angani - Bachelet

Mkazi nchini Iran akiatazama nyota kutoka eneo la Deyr Gachin Caravansary nchini Iran, eneo ambalo liko mbali na miji inayokumbwa na misako ambako pia waandamanaji wanakumbwa na msako unaotia shaka Umoja wa Mataifa.
Unspalsh/Mohamad Babayan
Mkazi nchini Iran akiatazama nyota kutoka eneo la Deyr Gachin Caravansary nchini Iran, eneo ambalo liko mbali na miji inayokumbwa na misako ambako pia waandamanaji wanakumbwa na msako unaotia shaka Umoja wa Mataifa.

Wanajeshi Iran wanafyatulia risasi waandamanaji kutoka angani - Bachelet

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameelezea hofu  yake juu ya kuendelea kwa ukosefu wa uwazi kuhusiana na vifo na matibabu ya watu 7,000 wanaoshikiliwa nchini Iran, wakati huu ambapo msako unaripotiwa kuendelea katika taifa hilo.

Yaelezwa kuwa vikosi vya usalama nchini Irana vinakabiliana na waandamanaji kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi, virungu na katika matukio mengine, risasi za moto zilielekezwa kwa washambuliaji ambao wanaonekana kutokuwa na tishio lolote kwa askari hao.

“Ripoti zinasema kuwa walinzi wa kikosi cha mapinduzi cha kiislamu, IRCG walihusika katika kushambulia waandamanaji ambapo picha za video zilizothibitishwa zinaonyesha ghasia za kiwango kikubwa dhidi ya waandamanaji ikiwemo wanajeshi wenye silaha wakifyatua risasi kutoka kwenye helikopta angani na pia kutoka juu ya jengo la sheria la mji mmoja,” amesema Bi. Bachelet.

Msemaji wa ofisi ya  hak iza binadamu ya Umoja wa Mataifa, Rupert Colville amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo ya kwamba takribani watu 7,000 wameripotiwa kukamatwa katika majimbo 28 kati ya majimbo 31 ya Iran tangu  kuanza kwa maandamano makubwa nchini humo tarehe 15 ya mwezi uliopita na kwamba Kamishna Mkuu Bachelet ana hofu kubwa kuhusiana na mazingira wanamoshikiliwa.

 Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet
ILO/M. Creuset
Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet

“Hofu pia ni kuhusu wanahudumiwa vipi, ukiukwaji wa haki yao ya kuhakikisha sheria inazingatiwa na uwezekano ya kwamba idadi kubwa wanaweza kufunguliwa mashtaka yanayohusisha hukumu ya kifo,” amesema Bwana Colville.

Amesema hadi sasa wana taarifa zinazodokeza ya k wamba takribani watu 208 waliuawa wakiwemo wanawake 13 na watoto 12.

Halikadhalika amesema kuna ripoti ambazo hadi sasa hawajaweza kuthibiitsha zinazodokeza ya  kwamba idadi ya waliouawa kwenye misukosuko nchini Iran ni zaidi ya maradufu ya hiyo 208 inayoripotiwa.