Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa 15 wa Ebola DRC watokomezwa; Uganda yaendelea kudhibiti

Mhudumu wa afya akimchanja dhidi ya Ebola, mwanaume mjini Beni, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC. (Maktaba)
World Bank/Vincent Tremeau
Mhudumu wa afya akimchanja dhidi ya Ebola, mwanaume mjini Beni, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC. (Maktaba)

Mlipuko wa 15 wa Ebola DRC watokomezwa; Uganda yaendelea kudhibiti

Afya

Mlipuko wa Ebola uliotangazwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wiki sita zilizopita sasa umetokomezwa, limesema shirika la Umoja wa MAtaifa la afya ulimwenguni, WHO wakati huu ambapo nchi Jirani ya Uganda inaongeza kasi kukabili mlipuko wa Ebola aina ya virusi Sudan ulioripotiwa wiki moja iliyopita.

WHO kanda ya Afrika imetoa ripoti hizi kupitia taarifa yake iliyotolewa katika miji ya Brazaville, Congo, Kinshasa huko DRC na Kampala nchini Uganda.

“Ikiwa ni mgonjwa mgonjwa mmoja tu aliyethibitishwa kuwa na Ebola kwenye mlipuko huo wa 15 DRC,” WHO inasema ni mlipuko ambao umekuwa na madhara madogo zaidi tangu Ebola ianze kukumba taifa hilo la Maziwa Makuu.

Mlipuko wa 14 wa Ebola uliotangazwa kudhibitiwa tarehe 4 mwezi Julai mwaka huu ulikuwa na wagonjwa wanne waliothibitishwa na kulikuwa na vifo vitano.

Mlipuko wa Ebola DRC unatokana na virusi aina ya Zaire, au #Ebolazaire, moja ya aina sita ya virusi vya Ebola.

Uganda kwa upande wake inahaha kudhibiti #EbolaSudan ambapo hadi sasa kuna wagonjwa 36, kati yao 18 wamethibitishwa kuwa na Ebola na wengine 18 bado wanashukiwa kuwa na ugonjwa huu na hadi tarehe 25 mwezi huu wa Septemba watu 23 wamethibitishwa kufariki dunia .

WHO inasema kwa DRC maandalizi ya kukabili Ebola na hatua za kuchukua zinaleta matunda mema.

Watu wakitembelea wanafamilia katika kituo cha kutibu Ebola huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC (Picha Maktaba)
World Bank/Vincent Tremeau
Watu wakitembelea wanafamilia katika kituo cha kutibu Ebola huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC (Picha Maktaba)

DRC imejipanga vema kukabili Ebola

“Siku chache baada tu ya mlipuko kutangazwa wa Ebola jimboni Kivu Kaskazini, mamlaka za afya zilisambaza chanjo kupitia mfumo wa kuwasaka na kuwachanja wale wote walioshukiwa kuwa karibu na wagonjwa,” imesema taarifa hiyo ya WHO.

Zaidi ya watu 500 walipatiwa chanjo wakiwemo 350 waambata wa wagonjwa pamoja na wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele.

Takribani watu 182 waliokuwa karibu na mgonjwa wa mwanzo walifuatiliwa kwa zaidi ya siku 21 na kuthibitishwa kuwa hawako tena hatarini kupata Ebola.

Uchambuzi wa sampuli kutoka kwa mgonjwa wa kwanza aliyethibitishwa unaonesha kuwa mlipuko huo una uhusiano na mlipuko wa mwaka 2018 hadi 2020 kwenye majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Ijapoku mlipuko wa sasa Kivu Kaskazini umetangazwa kumalizika, mamlaka za afya zinaendelea na mikakati ya ufuatiliaji na kuwa tayari kuchukua hatua iwapo kuna masalia yoyote ya maambukzi yataripotiwa.

Hatua za DRC zinaweza kutumika Uganda kukabili mlipuko

Wahudumu wa afya nchini Uganda.
WHO Africa
Wahudumu wa afya nchini Uganda.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amepongeza DRC kwa mikakati yake iliyofanikisha hatua ya sasa ya kudhibiti mlipuko wa 15 wa Ebola akisema. “tunaweza kutumia mbinu hizi kukabili mlipuko huko Uganda. Ingawa  bado hakuna chanjo dhidi ya Ebola aina ya virusi vya Sudan, tunaweza kudhibiti Ebola kwa kufuatilia waliokuwa karibu na wagonjwa, kubaini, kuwaweka karantini na kutoa usaidizi wa huduma.”

Hivi sasa EbolaSudan nchini Uganda imeripotiwa katika wilaya tatu za Mubende, Kyegegwa na Kassanda.

Hadi sasa watu 399 waliokuwa karibu na wagonjwa wamebainika na wanafuatiliwa.