Uganda yatangaza mlipuko wa Ebola ya virusi aina ya Sudan

20 Septemba 2022

Nchini Uganda mamlaka za afya zimetangaza mlipuko wa Ebola katika wilaya ya Mubende katikati mwa nchi hiyo baada Taasisi ya utafiti wa virusi nchini humo kuthibitisha kuwa kifo cha mwanaume mmoja kimesababishwa na ugonjwa huo wa Ebola wa aina ya virusi kutoka Sudan au #EbolaSudan.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni kanda ya Afrika iliyotolewa leo mjini Brazaville, Congo na Kampala, Uganda inasema uchunguzi ulitokana pia na vifo vya watu 6 wilayani humo mwezi uliopita na sasa kuna wagonjwa wengine 8 wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo.

Hii ni mara ya kwanza kwa zaidi ya muongo mmoja, Uganda inapata aina hiyo ya Ebola, amesema Dkt. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO, kanda ya Afrika akisema “tunashirikiana kwa karibu na mamlaka za kitaifa za afya Uganda ili kuchunguza chanzo cha mlipuko huu na wakati huo huo tunasaidia harakati za kusambaza hatua za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.”

Amesema jambo linalotia moyo ni kwamba, Uganda si ngeni katika hatua fanisi za kudhibiti Ebola, “tunashukuru kwa utaalamu wake, hatua zimechukuliwa haraka kutambua virusi hivyo na tunategemea utaalamu na ufahamu huo katika kukomesha kusambaa zaidi.”

Tayari WHO imetuma timu za kusaidia kutoa huduma kwa wagonjwa.

Kumekuweko kwa milipuko saba ya aina hii ya Ebola ambapo minne nchini Uganda na milipuko mitatu nchini Sudan. Mara ya mwisho Uganda iliripoti mlipuko mwaka 2021.

Mwaka 2019 Ebola yenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ikipatiwa jina #EBolaZaire ililipuka Uganda na viruso hivyo vilitokea DRC.

Chanjo iliyoko ni ya EbolaZaire na si EbolaSudan

Ingawa chanjo ya Ebola, imeonekana fanisi katika kudhibiti kuenea kwa Ebola, chanjo hiyo aina ya Ervebo (rVSV-ZEBOV) ina ufanisi katika kukabili EbolaZaire na si EbolaSudan.

Chanjo nyingine iliyotengenezwa na Jonhson Johnson inaweza kufaa lakini bado haijafanyiwa majaribio kwa virusi aina ya EbolaSudan.

Ebola ni ugonjwa hatari ambao unaweza kusabaisha kifo na hupata binadamu na nyani. Ina aina sita ya virusi, ambavyo vitatu kati yao ni Bundibugyo, Sudan na Zaire na vimeshasababisha milipuko.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter