Hatua mpya na ushirikiano vinasaidia vita dhidi ya Ebola DRC:UN

8 Novemba 2018

Hatua mpya za kukabiliana na changamoto za vita dhidi ya mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC zinazaa matunda ingawa mlipuko huo bado unasalia kuwa hatari na usiotabirika.

Hayo yameelezwa leo wa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani , WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus na Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix walipozungumza kwa pamoja na waandishi wa habari baada ya kuzuru maeneo mbalimbali ya Beni Mashariki mwa DRC ambako ndio kitovu cha mlipuko wa Ebola.

Viongozi hao wamepata fursa ya kukutana na wahudumu wa afya , wawakilishi wa asasi za kiraia, walinda amani na uongozi wa eneo hilo na kupongeza juhudi kubwa zinzofanywa na wahudumu wa afya na wadau wengine katika vita dhidi ya kusambaa kwa Ebola. Na baada ya kushuhudia hali halisi Dkt Tedros amewaeleza waandishi wa habari kwamba

"Bila shaka tuna changamoto lakini pia tuna mafanikio mengi , tumezuia usambaaji katika eneo la Mangina, Oicha, Makeke na Komanda. Na ukweli kwamba Ebola haijasambaa katika majimbo mengi na nchi jirani ni ushahidi tosha wa kazi kubwa inayofanywa na washirika wote”.

Hata hivyo amesema changamoto kubwa katika juhudi hizo ni usalama

 “Panapokuwa na shambulio operesheni zinasimama , na wakati operesheni zinasita, virusi vinafaidika na kutuathiri katika njia mbili , mosi ni kukimbizana na kazi zilizosimama za chanjo, au na huduma zingine , hivyo suluhu tuliyokubalina kama wadau ni ulinzi zaidi kwa MONUSCO kuongeza juhudi za miakakti ambayo tayari imeshaanza.”

  Naye mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani Bwana. Lacroix akielezea matumaini ya juhudi za pamoja amesema “Tunakabiliwa na changamoto lukuki na kubwa, lakini inatia moyo kuona kwamba juhudi zetu za kutoa huduma kama chombo kimoja cha Umoja wa Mataifa zimefanikiwa katika maeneo mengi na zitaendelea kusaidia katika kuokoa maisha na kutokomeza mlipuko wa Ebola.”

 

Watoto wa shule sehemu za Beni -DRC wajifunza kuwa kuosha mikono ndiyo njia bora ya kujilinda dhidi ya Ebola
UNICEF/Thomas Nybo
Watoto wa shule sehemu za Beni -DRC wajifunza kuwa kuosha mikono ndiyo njia bora ya kujilinda dhidi ya Ebola

Tangu mlipuko ulipozuka mwezi Agosti kumekuwa na visa 308 na vifo 191, na takribani nusu ya visa hivyo vimekuwa Beni mji ulio na watu laki 8. Na mlipuko wa sasa ni mlipuko wa 10 katika historia ya nchi hiyo na uko mbioni kuvunja rekodi ya mlipuko mkubwa kabisa uliopita mjini Yambuku mwaka 1976 ambapo kulikuwa na visa 318 na vifo 280.

Mpaka sasa watu 27,000 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola na kila mmoja amepata moja ya dawa nne mpya za majaribio kitu ambacho hakijawahi kufanyika hapo kabla.

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter