WFP nchini Kenya yapokea ufadhili mkubwa zaidi wa kupambana na njaa 

23 Septemba 2022

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limekaribisha mchango wa dola za Marekani milioni 194.5 kutoka kwa Serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), ili kutoa msaada muhimu wa chakula na lishe na kujenga uwezo wa kukabiliana na hali hiyo kwa maelfu ya watu wanaokabiliwa na changamoto za ukame mbaya zaidi katika miongo minne.  

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo jijini Nairobi, Kenya imeeleza kuwa mchango huo mkubwa zaidi kuwahi kutolewa na mfadhili mmoja kwa operesheni ya WFP nchini Kenya pia utasaidia mahitaji ya chakula ya maelfu ya wakimbizi. 

"Tunashukuru sana kwa mchango huu mkubwa zaidi kutoka kwa Serikali ya Marekani kusaidia maelfu ya watu walioathiriwa na ukame mkali na wale waliofurushwa kutoka makwao kutokana na migogoro," amesema Lauren Landis, Mkurugenzi wa WFP nchini Kenya na akaongeza akisema, "WFP inaongeza kwa kasi msaada wa kuokoa maisha ili kusaidia familia zilizoathiriwa zaidi na ukame ambao maisha yao yameharibiwa na misimu minne ya mvua iliyoshindwa mfululizo." 

Ufadhili huu utaiwezesha WFP kuongeza kasi ya kukabiliana na ukame kwa kutoa msaada wa chakula na fedha taslimu kwa watu 535,000 wanaokabiliwa na hali ya dharura ya njaa (kutoka watu 108,000 katika nusu ya kwanza ya 2022), kutibu utapiamlo kwa watoto wadogo 570,000, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha , na kuongeza mgao wa chakula hadi asilimia 80 (kutoka asilimia 50) kwa zaidi ya wakimbizi 500,000. WFP pia itaendelea kutoa mipango ya kujenga uwezo wa kustahimili ukame kama vile kukarabati miundombinu ya umwagiliaji na programu za mseto wa maisha kama vile ufugaji nyuki na kuanzishwa kwa mazao yanayostahimili ukame kwa watu 370,000. 

"Bado hakuna mwisho wa janga hili la ukame na tunatoa wito kwa wafadhili wote kuhakikisha ufadhili unaotabirika na endelevu katika mwaka huu na hadi 2023 ili kuokoa maisha na kuzuia watu wengi zaidi kukumbwa na njaa." amesema Landis. 

WFP inasema kwa kuna Wakenya milioni 3.5 wasio na chakula kutokana na ukame kwa mujibu wa ripoti ya Tathmini ya Mvua za Muda Mrefu 2022 iliyotolewa mwezi Agosti. Zaidi ya watu 700,000 wako katika viwango vya dharura na inakadiriwa watoto 940,000 (wenye umri wa miezi 6-59) na wajawazito 135,000 nchini kote wana utapiamlo na wanahitaji matibabu ya haraka. Ripoti hiyo pia inakadiria kuwa idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula inaweza kuongezeka hadi milioni 4.35 ifikapo Oktoba huku ukame ukizidi kuwa mbaya. 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter