Hatua za haraka zinahitajika kunusuru maisha ya mamilioni dhidi ya njaa:FAO
Ukame, mafuriko na vita katika nchi ambazo tayari zimeathirika na migogoro vinatishia kuwaweka mamilioni ya watu katika hatari ya baa la njaa kwa mujibu w shirika la Umoja wa Mataifa lachakula na kilimo, FAO.
Shirika hilo linasema limepokea chini ya asilimia 30 ya fedha za ufadhili zinzohitajika ili kuzuia zahma zaidi ya ukosefu wa uhakika wa chakula katika baadhi ya migogoro iliyoendelea kuvuma mwaka 2018 ikiwemo Afghanistan, Syria na Bangladesh.
Rosanne Marchesich, mkuu wa timu ya hatua za dharura na mnepo kwenye shirika la FAO anasema, hatua za haraka za kibinadamu zinahitajika ili kukidhi mahitaji ya watu milioni 33 duniani kote, na kutaja nchi nyingine zinazohitaji msada wa haraka kutokana na ukosefu ufadhili mdogo
“Tuna nchi nyingi ambazo hazina ufadhili wa kutosha hivi sasa , tuna Jamhuri ya Afrikaya Kati, tuna Haiti ambayo inakabiliwa na msimu unaokuja wa vimbunga hali tunayokabiliana nayo kila mwaka, na tuna nchi kama Iraq, Myanmar na ukanda wa Sahel ambazo zinakabiliwa na msimu wa mwambo unaohusiana na ukame wa muda mrefu ikiwa ni mgogoro mwingine na Sudan na Syria kutokana na athari za ukame unaoendelea na msimu unaokuja," amesema Rosanne.
Hivi sasa kiasi cha fedha kinahitajika ili kunusuru zahma hiyo ambapo Rosanne anasema “FAO inaomba haraka dola milioni 109 kwa ajili ya kuwafikia watu milioni 3.6, ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika nchi ambazo zimetajwa. Matatizo ya kusaidia yanatofautiana kati ya nchi na nchi lakini tunachojikita nacho ni uzalishaji mazao, mbogamboga kuboresha ufugaji na bila shaka udhibiti wa maliasili kwa ajili ya uzalishaji endelevu.”