Sudan inakabiliwa na janga la njaa, watoto, wakimbizi hatarini - WFP, UNHCR na UNICEF

23 Septemba 2022

Hali ya kibinadamu nchini Sudan ni ya kuangaliwa na kushughulikiwa kwa haraka kwani inazidi kuwa tete ikiweka maisha ya wanadamu hatarini, yameeleza Ijumaa leo mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa likiwemo la mpango wa chakula, WFP, la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la kuhudumia watoto, UNICEF. 

Sudan inakabiliwa na janga njaa linalozidi kuongezeka kutokana na madhara ya mabadiliko ya  tabianchi, mizozo ya muda mrefu na kupanda kwa bei za vyakula zikiacha familia zikitatizika kupata na kumudu bidhaa za msingi za chakula, Mwakilishi wa WFP nchini Sudan, Eddie Rowe, hii leo amewakumbusha  wanahabari mjini Geneva, Uswisi, kwamba, “mapema mwaka huu, WFP ilionya kwamba hadi watu milioni 18 wanaweza kukabiliwa na uhaba wa chakula ifikapo Septemba na kuna tathmini zinazoendelea kuthibitisha kuwa hofu yetu hiyo mbaya imetimia.” 

Sudan imekumbwa na mvua kubwa na mafuriko tangu Agosti ambayo yanatatiza msimu wa upanzi na yataathiri mazao. Takribani hekta 5,000 za ardhi tayari zimeharibiwa. Wakati huo huo, ukosefu wa usalama unaendelea kuzuia watu kuyafikia mashamba huko Darfur. 

Takriban watu milioni 15, au theluthi moja ya watu, wanakabiliwa na njaa nchini Sudan ikiwa  ni ongezeko la asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka jana kwa mujibu wa tathmini ya kina ya hivi karibuni iliyofanywa na WFP kuhusu uhakika na uwepo wa chakula.

“Tulipata fursa ya kuwatembelea watu katika kambi za wakimbizi wa ndani, huko Darfur hivi karibuni. Mara kwa mara, wasiwasi juu ya usalama na uwezo wao wa kupata ardhi yao ya kulima ndiyo masuala waliyoibua. Tunapoingia katika msimu wa upanzi nchini Sudan, WFP ina wasiwasi mkubwa kuhusu athari ambazo migogoro inayoendelea na majanga ya tabianchi yataleta kwenye mavuno yajayo. Mavuno ya mwisho tayari yalikuwa duni sana, na uzalishaji wa nafaka ulikuwa chini kwa asilimia 30 kuliko wastani wa miaka mitano iliyopita.” Ameeleza Eddie Rowe ambaye pia ndiye Mkurugenzi wa WFP Sudan. 

Aidha WFP inaeleza kuwa janga la chakula duniani linaloendelea pia limesukuma bei za vyakula vikuu kutoweza kufikiwa na wengi nchini Sudan huku gharama ya kapu la chakula ikipanda kwa asilimia 137 mwaka hadi mwaka. Takriban kila familia inatumia zaidi ya theluthi mbili ya mapato yao kwa chakula pekee, jambo ambalo linaacha pesa kidogo kulipia mahitaji mengine. 

Hatua zinatakiwa 

WFP inafanya kazi nchini Sudan katika nyanja mbili: kuokoa maisha ambayo yako katika hatari ya haraka ya njaa, huku ikijenga msingi kwa jamii kukidhi mahitaji yao ya chakula. Katika kukabiliwa na mahitaji ambayo hayajawahi kushuhudiwa na mtazamo usio na uhakika wa ufadhili, WFP inaangazia programu za muda mrefu za kujenga mnepo na kujitegemea kwa jamii. 

Hadi sasa, katika mwaka wa 2022 WFP imesaidia karibu watu milioni 5 kote Sudan, ikiwa ni pamoja na watu milioni 2.4 kwa msaada wa chakula, karibu watoto na akina mama milioni 1.3 kwa virutubisho vya lishe kutibu na kuzuia utapiamlo na watoto milioni 1.8 wenye umri wa kwenda shule kwa chakula cha shule au mgao wa nyumbani. Pia wanasaidia kuongeza vyandarua vya usalama na kusaidia wakulima kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno. 

Rasilimali hazitoshi 

WFP inalenga kuwafikia watu milioni 10 mwaka 2022 kwa msaada wa chakula na programu za kukabiliana na hali hiyo, lakini matazamio yasiyo na uhakika wa ufadhili yanaweza kutatiza uwezo wao wa kufikia lengo hilo.

Wakimbizi

Kwa upande wake Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limeonya juu ya kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu kwa wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan huku gharama za maisha zikiongezeka kutokana na athari za vita vya Ukraine, athari zinazoendelea kutokana na janga la COVID-19, na hali mbaya ya hewa inayotokana na janga la tabianchi.   

Sudan ni mwenyeji wa miongoni mwa idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao katika bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na zaidi ya wakimbizi milioni 1.1 wengi wao kutoka Sudan Kusini  na wakimbizi wa ndani milioni 3.7 wa Sudan, hasa katika Darfur na Kordofan. 

UNHCR inasema mfumuko wa bei ulikuwa tayari umepanda kwa kasi mwaka 2020 na unasalia kuwa juu zaidi kuliko viwango vya kabla ya COVID-19. Ongezeko kubwa la bei za vyakula na zisizo za vyakula na uhaba wa bidhaa muhimu ikiwa ni pamoja na mkate na mafuta yanaleta matatizo kwa jumuiya zinazowakaribisha, na kuathiri kwa kiasi kikubwa waliolazimika kuhama makazi yao, hasa wale wasio na usaidizi wowote wa kifedha. 

UNHCR inasema inashirikiana na serikali na wadau, “ili kuongeza mwitikio wetu, lakini juhudi za kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa wakimbizi na Wasudan waliokimbia makazi yao zinakabiliwa na shida kubwa kwa sababu ya ufadhili mdogo. Usaidizi mdogo unaweza kuwaacha wakimbizi wengi na jumuiya za wenyeji bila usaidizi muhimu, na kuwaacha kwenye hatari zaidi ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa.” 

UNHCR inaitaka jumuiya ya kimataifa kutoa ufadhili unaohitajika na mashirika ya kibinadamu nchini Sudan, kusaidia wakimbizi, wakimbizi wa ndani na jumuiya zinazowahifadhi. 

Watoto

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kupitia Mwakilishi wake Mandeep O’Brien UNICEF hii leo akizungumza na waandishi wa habari ameeleza kuwa watoto Sudan  katikati ya dhoruba la janga. 

"Katika muhtasari huu, lengo langu ni kusisitiza ukubwa wa changamoto wanazokabiliana nazo watoto wa Sudan. Na kushiriki hisia fulani ya hatua gani inahitajika haraka. Watoto wanashikwa na dhoruba kamili ya majanga juu ya majanga. Zaidi ya mtoto mmoja kati ya kila watoto watatu wa Sudan wanahitaji msaada wa kibinadamu. Takwimu hii ya kushangaza inatafsiriwa kwa karibu wasichana na wavulana milioni 8. Hili ni ongezeko la milioni 2.7 au asilimia 35 tangu 2020.” Amesema Mandeep O’Brien. 

Ameongeza akisema, "watoto milioni tatu walio chini ya umri wa miaka 5 nchini Sudan wana utapiamlo, ambapo 650,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali sana. Takriban nusu yao watakufa bila matibabu." 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter