Tunafanya kila liwezekanalo kuwasaidia Wasudan: UN
Tunafanya kila liwezekanalo kuwasaidia Wasudan: UN
Mashirika ya umoja wa Mataifa yanaendelea kufanya kila liwezekanalo ili kuwasaidia mamilioni ya watu wa Sudan ambao wanahitaji msaada hivi sasa kutokana na machafuko yanayoendelea.
Leo mratibu Mkuu wa Umoja Mataifa kuhusu misaada ya dharura, Martin Griffiths ambaye yuko Kenya kusaka suluhu ya kufikisha misaada ya kiutu nchini Sudan, amemshukuru Rais William Ruto kwa uongozi na usaidizi wake kuona hatua za dharura za kiutu zinachukuliwa ili misaada ifikie nchini Sudan.
Ametoa kauli hiyo baada ya Rais Ruto kuongoza mkutano uliohudhuriwa na viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa wakiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed, Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi na Bwana Griffiths.
Ujumbe wa Griffiths uko bayana “Tunahitaji kutafunta njia ya kufikisha misaada nchini Sudan na kuisambaza kwa wale wenye uhitaji “
Na kwa pande hasimu katika mzozo wa Sudan amewaambia “Lindeni raia na miundombinu ya raia . Pia hakikisheni mnatoa dfursa salama ya watu wanaokimbia kutoka katika maeneo yenye mapigano wanaondoka salama n ani lazima kuheshimu wahudumu wa mkibinadamu na mali zao. Saidien na kuwezesha operesheni za misaada na mwisho heshimuni wahudumu wa afya, usafiri na majengo yao.”
Kuna pengo la fedha kusaidia Sudan
Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya dharura, OCHA Jens Laerke amezungumza na waandishi wa habari huko Geneva Uswisi hii leo na kusema mashirika ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kiutu yanakabiliwa na pengo la dola bilioni 1.5 la kufanikisha operesheni zake Sudan wakati huu mahitaji yanaongezeka kutokana na mapigano yanayoendelea, maelfu ya watu wakifurushwa makwao.
Amesihi wahisani kuwa wakarimu zaidi ili ombi hilo la jumla ya dola bilioni 1.75 ambalo hadi sasa limefadhiliwa kwa asilimia 14 pekee liweze kukamilika kwani bila fedha za kutosha hawawezi kuendesha operesheni zao za kiutu kwa ukamilifu.
“Kwa maneno mengine, mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa na washirika wetu wanakabiliwa na pengo la ufadhili la dola bilioni 1.5. Tunatoa wito kwa wafadhili wote kutoa fedha kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu, ambayo tayari yalikuwa yakihangaika hata kabla ya ongezeko la machafuko ya hivi karibuni na ambayo yatahitaji pesa kutekeleza ufufuaji upya wa operesheni za misaada nchini Sudan ufufaji ambao tunashughulikia. Bila hiyo, hawawezi kufanya kazi.
Laerkeameongeza kuwa “pale ambapo hali ya usalama nchini Sudan inaruhusu, washirika wetu wanaendelea na shughuli zao, hasa kutoa huduma za afya na lishe.”
Wakimbizi 100,000 ni miongoni mwa walioondoka Sudan
Sshirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na wadau wanaendelea na kuongeza operesheni zao wakati watu wakiendelea kuvuka mpaka baina ya Sudan na mataifa Jirani.
msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi Olga Sarrado Mur amewaambia waandishi wa habari hii leo kwamba shirika hilo litazindua mpango wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wa kuchukua hatua za usaidizi Sudan, wakati huu ambapo takwimu za serikali, wadau na UNHCR zinaonesha kuwa zaidi ya watu 800, 000 wamekimbia Sudan na kuelekea Chad, Ethiopia, Sudan Kusini, na kwingineko, ambapo 600,000 ni wasudan na 200,000 ni wasudan kusini na wengineo waliokuwa wanapatiwa hifadhi Sudan.
Mpango utakaozinduliwa na UNHCR Kukabiliana na Wakimbizi wa Kikanda utajumuisha mahitaji ya kifedha.
Olga amesema “Tunajadili maelezo na washirika wetu katika kila nchi na tunapanga kutoa ombi haraka iwezekanavyo. Nchi jirani na Sudan zilizoathiriwa na dharura hii mpya tayari zinawahifadhi wakimbizi wengi na wakimbizi wa ndani. Wengi wanasalia na uhaba mkubwa wa fedha. Nchi zinazohifadhi wakimbizi zitahitaji usaidizi wa ziada ili kutoa ulinzi namsaada unaohitajika. Miongoni mwa mahitaji ya dharura ni maji, chakula, malazi, huduma za afya, vifaa vya msaada, kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, na huduma za ulinzi wa watoto”.