Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watumishi 3 wa WFP wauawa Sudan; Mkuu wa shirika hilo asitisha huduma

Wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP wakipakia dengu kwenye lori huko El-Fasher huko Darfur Kaskazini nchini Sudan.
© UN Photo/Albert Gonzalez Farran
Wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP wakipakia dengu kwenye lori huko El-Fasher huko Darfur Kaskazini nchini Sudan.

Watumishi 3 wa WFP wauawa Sudan; Mkuu wa shirika hilo asitisha huduma

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP limesitisha kwa muda operesheni zake nchini Sudan kutokana na mapigano kati ya vikosi kinzani vya kijeshi kwenye mji mkuu Khartoum, mapigano ambayo yamesababisha vifo vya wafanyakazi wake watatu jana Jumamosi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa tayari ametaka wahusika wa tukio hilo wafikishwe mbele ya sheria.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Cidy McCain, wafanyakazi hao walikuwa wanatekeleza majukumu yao ya kuokoa maisha ya watu huko Kabkabiya, Darfur Kaskazini.

Katika tukio lingine la Jumamosi, ndege ya shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya anga, UNHAS iliyokuwa inaratibiwa na WFP iliharibiwa kwa kiasi kikubwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum wakati wa mapigano, na hivyo kukwamisha uwezo wa  kusafirisha watoa huduma za kiutu na misaada ndani ya taifa hilo.

Katika taarifa yake, Bi. McCain ameelezea kuwa operesheni zote za shirika hilo nchini Sudan zimesitishwa, wakati ambapo hali ya usalama nchini Sudan ikifanyiwa tathmini.

“WFP imejizatiti kusaidia wananchi wa Sudan wanaokabiliwa na changamoto ya kupata uhakika wa chakula,” amesema Bi. McCain, “lakini hatuwezi kufanya kazi yetu ya kuokoa maisha iwapo usalama wa wafanyakazi na watendaji wetu iko hatarini. Pande zote lazima zifikie makubaliano ya hakikisho la usalama wa wafanyakazi wa kiutu Sudan na iwezeshe kuendelea kutoa huduma za usaidizi wa kibinadamu nchini Sudan. Hicho kinasalia kuwa kipaumbele chetu.”

Kifo wakati wa kutoa huduma za kiutu hakikubaliki na natoa wito wa hatua za haraka za hakikisho la usalama kwa wale wanaosalia nchini.

Bi. McCain amesisitiza kuwa vitisho kwa watendaji wa WFP vinafanya watendaji wetu washindwe kufanya kazi kwa usalama na kwa ufanisi nchini humo na kutekeleza majukumu muhimu ya WFP.

‘Haki bila kuchelewa’:Katibu Mkuu UN

Kufuatia sakata hilo nchini Sudan, siku ya Jumapili Katibu Mkuu Antonio Guterres ametoa wito kwa wahusika wafikishwe mbele ya sheria bila kuchelewa.

Kupitia  taarifa yake, Bwana Guterres ameelezea hofu yake kuhusu kuendelea kwa mapigano na kukumbusha pande kinzania juu ya umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa ikiwemo wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa wafanyakazi wote na wadau wa Umoja wa Mataifa, ofisi na mali zao.

Katibu Mkuu amesisitiza wito wa sitisho la mapigano na kurejea kwa mazungumzo na kusisitiza kuwa ataendelea kushirikiana na viongozi wa kikanda na wadau wa Sudan ili kutatua janga linaloendelea nchini humo.

Wafanyakazi wa huduma za kiutu wasilengwe na uporaji mali za UN ukome

Katika hatua nyingine, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuratibu kipindi cha mpito Sudan, UNITAMS amelaani vikali mashambulizi ya Jumapili na kusisitiza kuwa rai ana wafanyakazi wa kutoa huduma za kibinadamu katu wasilengwe kwenye mapigano kati ya vikundi kinzani.

Bwana Perthes amerejelea ripoti ya kwamba makombora yalilenga makazi ya Umoaj wa Mataifa na maeneo ya mashirika ya kiutu, huku mali zikiporwa kwenye maeneo kadhaa huko Darfur.

Amesema vitendo vyote hivyo vya ghasia vinavuruga utoaji wa misaada muhimu ya kiutu na lazima zikome. “Pindi matukio kama haya yanatokea, ni wanawake, wanaume na watoto wenye uhitaji zaidi ndio wanapata madhara zaidi.”

Bwana Perthes alitangaza Jumapili kuwa ameshawishi pande kinzani kwenye mapigano ambazo ni jeshi linaloundwa na wanamgambo wa zamani wa Janjaweed (RSF) dhidi ya jeshi la serikali, SAF, zisitishe mapigano kwa misingi ya kiutu, kati ya saa 10 jioni na saa 1 usiku saa za Sudan.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wataka utulivu

Wajumbe wa Baraza la Usalama nao wamepazia sauti sakata linaloendelea Sudan wakitoa wito wa kumalizwa kwa chuki huku wakieleza masikitiko yao kutokana na vifo na majeruhi.

Katika taarifa yake, wamesihi pande husika kurejesha utulivu, na kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kutatua janga linaloendelea Sudan.

Wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kwa operesheni za huduma za kiutu, halikadhalika usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nao upatiwe hakikisho.

“Tunasisitiza azma yetu ya kutambua kwenye umoja, mamlaka, uhuru na eneo la Jamhuri ya Sudan,” wametamatisha katika taarifa yao.