Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utumwa wa zama za sasa: Watu milioni 50 watumikishwa kazini na kwenye ndoa!

Wafanyakazi wa majumbani ni miongoni mwa sehemu ya nguvu kazi duniani ambayo iko hatarini zaidi kutumikishwa.
@ILO/J.Maillard
Wafanyakazi wa majumbani ni miongoni mwa sehemu ya nguvu kazi duniani ambayo iko hatarini zaidi kutumikishwa.

Utumwa wa zama za sasa: Watu milioni 50 watumikishwa kazini na kwenye ndoa!

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Watu milioni 50 walikuwa wakiishi katika utumwa wa zama za kisasa mwaka jana 2021, kwa mujibu Ripoti ya hivi karibuni ya makadirio ya utumwa huo duniani ambayo imetolewa na shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa, ILO, Wakfu wa Walk Free na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo mjini Geneva nchini Uswisi, ILO, IOM na Wakfu wa Walk Free, makadirio ya hivi karibuni kupitia utafiti wao, yanaonesha kuwa kazi za kulazimishwa na ndoa za kulazimishwa zimeongezeka sana katika miaka mitano iliyopita. 

Watu milioni kumi zaidi walikuwa katika utumwa wa kisasa mwaka jana 2021 na hivyo kufikia watu milioni hamsini ikilinganishwa na makadirio ya kimataifa ya mwaka 2016. Wanawake na watoto wanabaki katika mazingira magumu kupita kiasi, umebaini utafiti.  

Watu wanatumiishwa kwenye ndoa!

Kati ya watu hawa, milioni 28 walikuwa katika kazi ya kulazimishwa na milioni 22 wakiwa katika ndoa za kulazimishwa. 

Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Ryder kwa amenukuliwa kwa maskitiko akisema, "inashangaza kwamba hali ya utumwa wa kisasa haibadiliki. Hakuna kinachoweza kuhalalisha kuendelea kwa ukiukwaji huu wa kimsingi wa haki za binadamu.”  

Baadhi ya misingi ya kabila, dini na tamaduni ni upenyo wa utukimishwaji wa kisasa

Ripoti imeonesha kuwa wafanyakazi wahamiaji wana uwezekano wa zaidi ya mara tatu kuwa katika kazi ya kulazimishwa kuliko wafanyakazi wazima wasio wahamiaji ndio maana Mkurugenzi Mkuu wa IOM, amesema, “ripoti hii inasisitiza udharura wa kuhakikisha kwamba uhamiaji wote ni salama, wenye utaratibu na wa kawaida." 

Taarifa imeeleza kuwa utumwa wa kisasa unatokea karibu kila nchi duniani, na unapita katika misingi ya kikabila, kitamaduni na kidini. Zaidi ya nusu (asilimia 52) ya kazi zote za kulazimishwa na robo ya ndoa zote za kulazimishwa zinaweza kupatikana katika nchi zenye kipato cha juu au cha kati.