Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usasa hautuepushi na mauaji ya kimbari bali maadili na vitendo -UN

Jua likizama katika kambi ya Auschwitz-Birkenau walikopata mateso wayahudi.  Kambi hii iliyopo Poland imesalia kuwa ishara ya ugaidi, mauaji ya kimbari na ya holocaust.
UN / Evan Schneider
Jua likizama katika kambi ya Auschwitz-Birkenau walikopata mateso wayahudi. Kambi hii iliyopo Poland imesalia kuwa ishara ya ugaidi, mauaji ya kimbari na ya holocaust.

Usasa hautuepushi na mauaji ya kimbari bali maadili na vitendo -UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Miaka 70 tangu kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa wa kuzuia mauaji ya kimbari, bado watu wanauawa, wanabakwa, nyumba zao kutiwa moto, wananyang’anywa ardhi zao kwa sababu tu ya utambulisho wao.

Hiyo ni sehemu ya hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyotoa leo  kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakati wa tukio la kuadhimisha miaka 70 ya mkataba huo uliopitishwa tarehe 9 Desemba mwaka 1948.

Ametolea mfano waislamu wa kabila la Rohingya huko Myanmar, “ambao kwa mfumo maalum wamekuwa wanauawa, wanateswa, wanabakwa, wanachomwa moto wakiwa wanashuhudia, ni waathirika wa kile kinachoitwa mauaji ya kimbari. Katu sitasahau simulizi za kuogopesha nilizosikia kutoka kwa wakimbizi wa kabila la rohingya huko Bangladesh mapema mwaka huu.”

Kama hiyo haitoshi, Guterres amesema kwingine duniani, ubaguzi wa rangi, kauli za chuki, ghasia, chuki dhidi ya wanawake na wasichana, chuki dhidi ya wayahudi, waislamu na wageni inazidi kuongezeka.

Warohingya wakivuka mto Naf ili kufikia kambi za wakimbizi nchini Bangladesh
© UNHCR / Andrew McConnell
Warohingya wakivuka mto Naf ili kufikia kambi za wakimbizi nchini Bangladesh

“Kizazi changu kiliamini kuwa  baada ya mauaji ya halaiki yaliyofanywa na manazi, tusingalishuhudia tena mauaji ya kimbari. Tulikosea,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “usasa hautulindi dhidi ya mauaji ya kimbari. Zama za dijitali hazitulindi dhidi ya mauaji ya kimbari. Hakuna kinachoweza kutulinda zaidi ya matendo yetu kwa kuzingatia maadili na misingi.”

Ametaka maadhimisho ya miaka 70 ya mkataba huo wa kimataifa ambao amesema una vipengele muhimu vya kudhibiti mauaji   ya kimbari, yatumike kukumbuka pia utu wa waathirika wa mauaji hayo.

“Kwa kufanya hivyo tunaahidi kuhakikisha jamii zilizoathiriwa na uhalifu huu zinaweza kuelezea simulizi zao, kuweka kumbukumbu ya kihistoria ya kilichotokea na pale panapofaa wapatiwe fidia’” amesema Guterres

Ameshukur wale wote wanaosaidia kuhifadhi kumbukumbu hizo akisema ni matarajio yake kubuniwa kwa mbinu za kisasa za kuelimisha vijana na vizazi vijavyo juu ya machungu ya mauaji ya kimbari.

Hadi sasa nchi 149 pekee ndio zimeridhia mkataba dhidi ya mauaji ya kimbari na 45 bado hazijafanya hivyo na Guterres amezisihi zichukue hatua kwani kwa kufanya hivyo ni ujubme tosha kuwa mauaji ya kimbari yanapingwa dunia nzima.