Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukraine inaadhimisha miezi sita ya 'vita visivyo na maana': Guterres

Mtoto mdogo wa kike amesimama kwenye vifusi vya shule yake iliyoharibika huko Horenka, katika mkoa wa Kyiv, Ukraine.
© UNICEF/Olena Hrom
Mtoto mdogo wa kike amesimama kwenye vifusi vya shule yake iliyoharibika huko Horenka, katika mkoa wa Kyiv, Ukraine.

Ukraine inaadhimisha miezi sita ya 'vita visivyo na maana': Guterres

Amani na Usalama

"Vita visivyo na maana" nchini Ukraine sasa vimefikisha miezi sita tangu kuzaliwa, na mwisho hauonekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo , akirudia ombi lake la kutaka kupatikane amani.

"Hatua hii ya kusikitisha na ya kuhuzunisha" imeambatana na maadhimisho ya miaka 31 ya uhuru wa Ukraine, Guterres aliwapongeza watu wa nchi hiyo. [scald=257732:sdl_editor_representation] "Watu wa Ukraine na kwingineko wanahitaji amani na wanahitaji amani sasa," alisema Mkuu huyo wa UN na kufafanua kuwa "Amani kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Amani kwa mujibu wa sheria za kimataifa.” Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alishiriki katika mkutano huo kwa njia ya video ingawa wakati fulani hotuba yake haikuweza kusikika vyema. Alisema kuwa dunia inategemea uhuru wa nchi yake. Maendeleo ya biashara ya nafaka Katika kipindi cha tangu uvamizi wa Urusi tarehe 24 Februari, maelfu ya raia wameuawa au kujeruhiwa, mahitaji ya kibinadamu yameongezeka, na ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu umeripotiwa. Mamilioni ya watu ulimwenguni kote pia wanaendelea kukabiliwa na mzozo wa chakula, mbolea na mafuta ulimwenguni, athari mbaya ya vita. Katibu Mkuu alitoa taarifa kuhusu ziara yake nchini Ukraine wiki iliyopita kufuatilia makubaliano ya kihistoria ya kurejesha nafaka kutoka nchi hiyo katika masoko ya kimataifa. "Ninaweza kuripoti kwa Baraza kwamba Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, uliotiwa saini Istanbul mnamo mwezi Julai 2022, unaendelea vizuri na meli nyingi zinazoingia na kutoka bandari za Ukraine, zikiwa zimesheheni zaidi ya tani 720,000 za nafaka na bidhaa zingine za chakula. ,” aliwaambia mabalozi. Mpango huo uliotiwa saini na Ukraine, Urusi, uturuki na Umoja wa Mataifa unawakilisha "maonesho yenye nguvu ya kile kinachoweza kupatikana, hata katika mazingira mabaya zaidi, tunapoweka watu mbele," aliongeza ingawa akiashiria kazi ambayo bado iko mbele. "Sehemu nyingine ya mpango huu wa pamoja ni upatikanaji usiozuiliwa wa masoko ya kimataifa ya chakula na mbolea ya kutoka Urusi, ambayo haiko chini ya vikwazo. Ni muhimu kwamba serikali zote na sekta binafsi zishirikiane kuzileta sokoni.” Tishio la nyuklia Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia alisisitiza wasiwasi wake juu ya hali ya ndani na karibu na Kiwanda cha Nishati ya Nyuklia cha Zaporizhzhia, ambacho kimekuwa na mashambulizi makali katika wiki za hivi karibuni. "Taa za tahadhari zinawaka," alisema. "Hatua zozote ambazo zinaweza kuhatarisha uadilifu wa kimwili, Usalama na ulinzi wa kiwanda cha nyuklia hazikubaliki. Kuongezeka kwa hali yoyote kunaweza kusababisha uharibifu wa kibinafsi." Guterres amekaribisha na kuunga mkono Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kupeleka timu yake ya wataalamu kwenye kinu hicho, ambacho ni kituo kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya. Wakati huo huo, juhudi zinaendelea kupeleka Ujumbe wa Kutafuta Ukweli ulioanzishwa hivi karibuni huko Olenivka, ambapo zaidi ya wafungwa 50 wa vita wa Ukraine waliuawa katika mlipuko katika kituo cha kizuizini mwishoni mwa mwezi Julai. [scald=257722:sdl_editor_representation] Takwimu za vifo na majeruhi Kuanzia mwezi Februari 24, hadi Agosti 23, 2022, Umoja wa Mataifa ulirekodi vifo vya raia 13,560 nchini humo. Takriban raia 5,614 waliuawa, wakiwemo watoto 362, na 7,946 walijeruhiwa, kutia ndani watoto 610. Hata hivyo Umoja wa Mataifa, umesema idadi halisi inaweza kuwa mkubwa zaidi. Zaidi ya asilimia 90 ya majeruhi hayo yalisababishwa na matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi. "Kila moja ya nambari hizi ni binadamu, ambaye maisha yake au afya yake imepotea au kuharibiwa," alisema Matilda Bogner, Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kufuatilia Haki za Kibinadamu nchini Ukraine, katika kumbukumbu ya miezi sita tangu uvamizi wa Urusi kwa Ukraine. Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa pande zote kuhakikisha ulinzi wa raia wakati wote wa mapigano. Hasa tangu kuongezeka kwa mzozo wa silaha ambao umedumu "kwa miaka 8" ambao umesababisha vifo zaidi, mateso, na uharibifu. [scald=257712:sdl_editor_representation] Kesi za watu kuwekwa vizuizini kiholela na upotevu zinafanyika pande zote mbili "Kila siku tunazungumza na watu walioathiriwa na vita, na tunasikiliza na kuweka kumbukumbu za ukiukwaji wa haki za binadamu za kimataifa na sheria za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na uhalifu wa kivita," aliongeza Bogner. Aidha, raia pia ni wahanga wa kuwekwa kizuizini kiholela na kutoweka. Umoja wa Mataifa umegundua visa vya watu 327 (wanaume 279, wanawake 47) katika eneo linalodhibitiwa na jeshi la Urusi na vikundi vilivyojihami tangu Februari 24. Katika kundi hilo, waathirika 105 (wanaume 86 na wanawake 18, na mtoto mmoja) waliachiliwa, na 14 walipatikana wamekufa (wanaume 13 na mwanamke 1). Kuhusu vikosi vya jeshi la Ukraine, Umoja wa Mataifa ulirekodi kukamatwa kwa watu 39 kiholela (wanaume 35 na wanawake 4) na kesi zingine 28 (wanaume 24 na wanawake 4) za watu kutoweka. Wakati wa kukamatwa huku, "kanuni za kiutaratibu na kimahakama za haki ya uhuru zilikiukwa". Wafungwa wa vita "wanateswa na kutendewa vibaya" Kulingana na Umoja wa Mataifa, wengi wa waathirika hao walikabiliwa na mateso kutoka pande zote mbili. "Binadamu, hata awe nani, lazima atendewe kwa heshima," akasisitiza Mkuu wa Misheni ya Umoja wa Mataifa ya Kufuatilia Haki za Kibinadamu nchini Ukraine. Aliongeza kuwa, wafungwa wa vita pia "waliteswa na kutendewa vibaya". Changamoto nyingine iliyowakabili wachunguzi ilikuwa kufikia magereza. "Wakati tuna uwezo wa kufikia wafungwa wengine wanaohusishwa na migogoro katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali, hatuna uwezo wa kuwafikia wafungwa wanaohusishwa na migogoro wanaoshikiliwa katika maeneo mengine," alisisitiza Bi Bogner. Kwa hivyo Umoja wa Mataifa unaitaka Urusi kuwapa waangalizi uhuru wa ufikiaji kamili kwa watu wote waliozuiliwa kuhusiana na mzozo huo wa kivita, wakiwemo wale wanaozuiliwa na makundi yenye silaha yenye uhusiano na Urusi. Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa unaendelea kuandika yale wanayoyaona katika nchi hizo, ambayo ni muhimu ili kuzuia ukiukwaji zaidi na kuwawajibisha wale waliohusika na ukiukaji wa zamani. "Tunasisitiza wito wetu kwa wahusika kuhakikisha mara kwa mara wanawaokoa na kuwalinda raia kwa muda wote wa mapigano," alisema Mkuu wa Ujumbe wa Kufuatilia Haki za Kibinadamu nchini Ukraine.