Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa ya Ulaya msiweke Watoto vizuizini:UN

Watoto wahamiaji wanaosubiri pasi za kusafiria wakichora picha za nyumba walizokimbia. Wapo katika eneo rafiki kwaa watoto linalofadhiliwa na UNICEF kwenye mpaka wa Mexico na Guatemala huko Ciudad Hidalgo, Mexico, Januari 29, 2019.
© UNICEF/UN0277463/Bindra
Watoto wahamiaji wanaosubiri pasi za kusafiria wakichora picha za nyumba walizokimbia. Wapo katika eneo rafiki kwaa watoto linalofadhiliwa na UNICEF kwenye mpaka wa Mexico na Guatemala huko Ciudad Hidalgo, Mexico, Januari 29, 2019.

Mataifa ya Ulaya msiweke Watoto vizuizini:UN

Haki za binadamu

Nchi za barani Ulaya zimeshauriwa kuacha kuwaweka Watoto wahamiaji vizuizini na badala yake watumie njia mbadala ambazo hazitasababisha Watoto hao kuathirika kisaikolojia, kuzidisha mfadhaiko na wasiwasi pamoja na unyanyasaji. Haya yamesemwa kwenye taarifa ya pamoja ya mashirika matatu ya umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, la kuhudumia Watoto UNICEF na la uhamiaji IOM.

Taarifa hiyo kutoka Geneva Uswisi imeeleza kuwa kuwaweka Watoto vizuizini kuna athari mbaya kiafya na ustawi wa Watoto na kunaweza kuwa na athari mbaya ya muda mrefu katika ukuaji wao na utambuzi.

Mkurugenzi wa UNHCR barani Ulaya Pascale Moreau amesema “nchi kadhaa barani humo tayari zimeonesha kuna njia mbadala za kuweka Watoto na familia zao kizuizini na kuweza kuwa salama kwa utu na gharama nafuu na kwamba mataifa yote ya ulaya yanapaswa kufuata mbinu hizo ili kulinda haki na ustawi wa Watoto wakimbizi na wahamiaji.”

Akiunga mkono kauli hiyo mkurugenzi wa kanda hiyo wa OIM Ola Henrikson amesema wanahamasisha serikali za mataifa ya ulaya badala ya kuweka vizuini Watoto na familia zao watumie programu za kijamii, kuangalia kila mhitaji na mahitaji yake Pamoja na njia nyingine mbadala zinazojali haki. “Umoja wa familia na maslahi bora ya Watoto yanaenda sambamba katika mustadha wa wahamijai”.

Wakimbizi na watoto wahamiaji waishio katika kituo cha mapokezi Moria, sehemu za Lesvos, Ugiriki
UNICEF/Pavlos Avagianos
Wakimbizi na watoto wahamiaji waishio katika kituo cha mapokezi Moria, sehemu za Lesvos, Ugiriki

Walioyaona katika nchi 38

Taarifa hiyo ya pamoja imesema walifanya mapitio katika nchi 38 barani ulaya na mambo waliyoaona yanatia wasiwasi kwa watoto. 

Katika mapitio hayo pia waligundua njia bora mbadala wa kuweka watoto vizuizini kama vile kuacha watoto kuishi kwa kujitegemea kwa namna wanavyoweza, kuwaweka watoto kwenye vituo vya malezi ya familiapamoja na mifano mingine kadha wa kadha inayofaa kwa watoto na inayozingatia ustawi wa watoto ambayo ipo katika nchi mbalimbali za ulaya na ambayo inatoa masuluhisho yanayoweza kutumika na kwa gharama nafuu kwa nchi zinazopokea watoto hao. 

“Jambo la kwanza kuzingatia ni kuwa watoto wahamiaji ni watoto bila kujali wanatoka wapi na kwanini waliacha nyumba zao” amesema Afshan Khan Mkurugenzi wa kanda ya Ulaya wa UNICEF na kuongeza kuwa “kuwaweka vizuizini watoto kamwe sio suluhisho kwa maslahi yao, ni ukiukwaji wa haki zao na lazima kuepukwe kwa ghatama yoyote”.

Mapendekezo yaliyotolewa na mashirika hayo matatu ya Umoja wa Mataifa ni pamoja na kupanua njia mbadala za kuweka watoto pamoja na familia zao vizuizini, kuwekeza katika mazingira bora ya mifumo ya ulinzi ya kuwapokea ndani ya nchi zao na kuimarisha uwezo wa kitaifa wa ukusanyaji na ufuatiliaji wa takwimu ndani ya mataifa ya muungano wa Ulaya.