Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziara ya Katibu Mkuu wa UN kuhusu Ukraine: “Nafurahia kuripoti mafanikio fulani“

Raia kutoka Mariupol wanakimbia Azovstal eneo la Mariupol kufuatia operesheni ya kuhamishwa inayoongozwa na UN.
© UNOCHA/Kateryna Klochko
Raia kutoka Mariupol wanakimbia Azovstal eneo la Mariupol kufuatia operesheni ya kuhamishwa inayoongozwa na UN.

Ziara ya Katibu Mkuu wa UN kuhusu Ukraine: “Nafurahia kuripoti mafanikio fulani“

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonip Guterres amelihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo jioni (05-05-2022) na kueleza kuwa wakati wa ziara yake maalum nchini Urusi na Ukriane hakusita kuwaeleza kinaga ubaga bila kupepesa maneno kwa nyakati tofauti na marais wa nchi hizo kwakuwa anataka kuona mzozo na ukatili unaoendelea sasa unamalizika mara moja. 

Akiwahutubia wajumbe wa Baraza hilo Guterres amesema “Katika safari zangu zote, sikumung’unya maneno. Nilisema jambo lile lile huko Moscow (Urusi) kama nilivyofanya huko Kyiv (Ukraine) ambayo ndiyo hasa nimesema mara kwa mara hapa New York. Yaani kwamba: Uvamizi wa Urusi kwa Ukraine ni ukiukaji wa uadilifu wa mipaka yake na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine na Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu, Osnat Lubrani, ana mkutano na waandishi wa habari mjini Zaporizhzhia, Ukraine.
© UNOCHA/Kateryna Klochko
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine na Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu, Osnat Lubrani, ana mkutano na waandishi wa habari mjini Zaporizhzhia, Ukraine.

“Mafanikio fulani”

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza pia ziara yake imezaa matunda  na kuwapongeza Rais Vladmir Putin wa Urusi na Volodymyr  Zelenskyy wa Ukraine kwakuwa baadhi ya masuala yaliyojadiliwa yametekelezwa na kuwezesha Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu ICRC kuwaondoka  watu waliokwama Mariupol.

“Ninafuraha kuwajulisha kuwa tuna mafanikio fulani. Mpaka kufikia sasa, misafara miwili ya kupita kwa usalama imekamilika kwa ufanisi. Wa kwanza, iliokamilika tarehe 3 Mei, raia 101 walihamishwa kutoka kwenye kiwanda cha Azovstal pamoja na watu wengine 59 kutoka eneo la jirani. Katika operesheni ya pili iliyokamilika jana usiku, zaidi ya raia 320 walihamishwa kutoka mji wa Mariupol na maeneo jirani.”

Guterres pia amegusia kuendelea kwa operesheni ya tatu lakini akasema haitakiwi kuzungumziwa kwa sasa
“Ni sera yetu kutozungumza juu ya maelezo yoyote kabla ya kukamilika kwa operesheni hii ili kuepusha kudhoofisha mafanikio yanayoweza kutokea.Ni vyema tukafahamu kwamba hata nyakati hizi za mawasiliano ya hali ya juu, diplomasia ya kimya bado inawezekana na wakati mwingine ndiyo njia pekee ya kuleta matokeo.”

Raia waliohamishwa kutoka kiwanda cha chuma cha Azovstal huko Mariupol wanafikia usalama huko Zaporizhzhia.
© UNOCHA/Kateryna Klochko
Raia waliohamishwa kutoka kiwanda cha chuma cha Azovstal huko Mariupol wanafikia usalama huko Zaporizhzhia.

Misaada ya kibinadamu

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kutoa misaada ya kibinadamu (OCHA), Martin Griffiths, naye alipata fursa ya kuhutubia katika Mkutano huo ambapo alieleza hali ilivyo sasa nchini Ukraine na uharibifu wa miundombinu ya kiraia na zaidi ya yote akaeleza zaidi ya Waukraine milioni 13 wamejikuta wakilazimika kukimbia makazi yao, kuachana na maisha yao waliyozoea na kusambaratika na wanafamilia.

Alibainisha kuwa wazee na wengine ambao hawakuweza kukimbia, wameshindwa kutafuta hifadhi kutokana na mabomu, uhaba wa mahitaji muhimu na kutokuwepo kwa taarida za uokoaji.

“Na tangu vita kuanza, tishio la unyanyasaji wa kijinsia limeongezeka huku madai ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake, wasichana, wanaume na wavulana yakiongezeka.” Amesema Griffiths.

Shule moja huko Kharkiv, kaskazini-mashariki mwa Ukraine, imeharibiwa baada ya kushambuliwa kwa makombora.
© UNICEF/Kristina Pashkina
Shule moja huko Kharkiv, kaskazini-mashariki mwa Ukraine, imeharibiwa baada ya kushambuliwa kwa makombora.

Kiongozi huyo ambaye pia anasimamia misaada ya dharura amesema “ Mpaka sasa tuna  wafanyakazi 1,400 waliosambazwa kote nchini Ukraine, tumefanikiwa kuwafikia zaidi ya watu milioni 4.1 kwa aina fulani ya usaidizi katika mikoa 24 yote ya nchi.”

Mkuu huyo wa OCHA alitaja maeneo wanayoendelea kushughulikia kwa sasa yamegawanyika katika makundi matatu lakini mipango yao mpaka kufikia mwisho wa mwezi Mei ni kuhakikisha wamewafikia watu milioni 1.3 kwa usaidizi wa pesa taslimu.

Haki za binadamu na sheria za Kimataifa 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet alijiunga na Mkutano huo kutokea jijini Geneva Uswisi na kueleza kuwa mpaka sasa mzozo wa Miaka 8 kati ya Ukraine na Urusi na Vita rasmi iliyoanza siku 71zilizopita umefanya baadhi ya wafanyakazi wa ofisi yake kuhamia Ukraine kufuatilia tuhuma na kukusanya ushahidi wa uvunjifu wa haki za binadamu na mikataba ya kimataifa. 

“Ripoti za matukio mabaya, kama vile shambulio kwenye hospitali nambari 3 na ukumbi wa michezo wa kuigiza. Mariupol, kwenye kituo cha reli huko Kramatorsk, kwenye maeneo ya makazi huko Odesa, ... Inaonekana hakuna mwisho mbele ya ripoti za kila siku za vifo vya raia na majeraha.” Amesema Bachelet 

Amesema timu yake iliyoko nchini Ukraine imekuwa ikizungumza na watu ambao wameeleza kuwa na kiwewe kutokana na madhila yaliyo wafika au kushuhudia. 

Ofisi yake imeripoti mara kwa mara, watu wengi ambao ni majeruhi kutokana na matumizi ya silaha za milipuko zenye athari kwa eneo pana katika maeneo yenye watu wengi, kama vile makombora, silaha nziton ikiwa ni pamoja na mifumo mingi ya kurusha roketi, na makombora na mashambulizi ya angani.

Akitaja baadhi ya yale yaliyorekodiwa Mkuu huyo wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema “Ofisi yangu imerekodi matukio mabaya ya uvunjifu wa haki za binadamu. Katika maeneo ya jirani na Kyiv, kuanzia mwishoni mwa Februari kwa takriban wiki 5, vikosi vya Urusi vililenga raia wa kiume, ambao waliwaona kuwa wa kutilia shaka. Wanaume waliwekwa kizuizini, kupigwa, kwa ufupi kunyongwa na, katika visa vingine, kupelekwa Belarusi na Urusi, bila familia zao kujua, na kuzuiliwa katika vituo vya mahabusu kabla ya kesi. Wafanyakazi wangu walikutana na familia zinazotafuta ndugu zao wa kiume, wakitamani kujua walipo, ikiwa wako hai, na wanawezaje warudishe. Familia zilipigwa risasi walipokuwa wakijaribu kutoroka katika misafara.”