Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na UNICEF wasaidia juhudi zakupambana na kipindupindu kinachozidi kuenea nchini Malawi

Kambi ya kipindupindu huko Nsanje, Malawi
Moving Minds Multimedia/Malawi
Kambi ya kipindupindu huko Nsanje, Malawi

WHO na UNICEF wasaidia juhudi zakupambana na kipindupindu kinachozidi kuenea nchini Malawi

Afya

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la afya ulimwenguni WHO na la Kuhudumia Watoto UNICEF wametangaza kuongeza nguvu kwenye juhudi za kuzuia kuenea kwa Ugonjwa wa kipindupindu nchini Malawi.

Taarifa ya mashirika hayo iliyotolewa huko Lilongwe Malawi imesema mlipuko huo, ambao hapo awali ulianzia kusini mwa nchi hiyo, sasa umeenea katika mikoa ya kaskazini na katikati ya Malawi. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali iliyolewa kwa vyombo vya habari jumatatu ya tarehe 22 Agosti 2022 mpaka siku hiyo wagonjwa wenye kipindupindu walikuwa ni 1,483 na vifo 58 vimerekodiwa ambapo kiwango hicho cha vifo ni sawa na asilimia 3.9. Wagonjwa wanaendelea kuongezeka nje ya maeneo ambayo ni kitovu cha ugonjwa huo katika wilaya zilizo zoeleka na kuathiri jamii za watu wanaoishi kwenye mwambao wa ziwa na maeneo yenye watu wengi maeneo ya mijini yaliyo na ukosefu wa maji ya kitosha pamoja na huduma za vyoo. Mwakilishi wa UNICEF nchini Malawi Rudolf Schwenk amesema “Athari za mlipuko mkubwa zaidi zitalemea sekta za huduma za afya ya umma ambazo tayari zimeelemewa na mifumo ya utoaji wa huduma za afya nchini humu, hivyo ni lazima kuchukua hatua sasa” huku akiongeza kuwa “Habari njema ni kwamba tunajua suluhisho.” Kila kifo kitokanacho na Kipindupindu kinaweza kuzuilika Licha ya juhudi zinazoendelea katika kukabiliana na mlipuko wa kitaifa wa kipindupindu, mapungufu makubwa yameonekana ikiwa ni pamoja na hitaji la haraka la kugunduliwa na kudhibiti mapema, kupatikana kwa vifaa muhimu vya kusimamia wagonjwa na matibabu ya maji, usafi wa kibinafsi na uhifadhi wa maji katika ngazi ya kaya na mawasiliano ya kutoa elimu kuhusu kuzuia na kuhamasisha mazoea chanya ya usafi. UNICEF na WHO zinatoa wito kwa washirika na wafadhili kusaidia kutoa fedha za ziada na misaada mingine ili kuiwezesha Malawi kukabiliana na changamoto hizi na kudhibiti mlipuko huu. Mwakilishi wa WHO nchini Malawi Neema Rusibamayila Kimambo amesisitiza kuwa shirika lao litaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wizara ya Afya ya Malawi katika kutekeleza udhibiti wa haraka na wamuda mredu wa kipindupindu, kukabiliana nacho na hatua za kujikinga.” Kila kifo kutokana na kipindupindu kinaweza kuzuilika kwa kutumia zana tulizonazo leo.” Tangu kutangazwa kuzuka kwa mlipuko wa kipindupindu mwezi Machi mwaka huu 2022, UNICEF na WHO yamekuwa yakifanya kazi kwa karibu na Wizara ya Afya, Maji na Usafi wa Mazingira, mamlaka za wilaya, na wengine, katika kuandaa na kuratibu mpango wa kukabiliana na kuwasilisha vifaa na huduma muhimu kwa familia na jamii katika wilaya zilizoathiriwa na kipindupindu nchini Malawi.