Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na AU watia saini makubaliano kuimarisha utimizaji wa malengo muhimu ya afya

Kampeni dhidi ya Ebola ambako wahamasishaji wanajibu maswali ya wanajamii huko Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC. (Agosti 2019)
© UNICEF/Thomas Nybo
Kampeni dhidi ya Ebola ambako wahamasishaji wanajibu maswali ya wanajamii huko Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC. (Agosti 2019)

WHO na AU watia saini makubaliano kuimarisha utimizaji wa malengo muhimu ya afya

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO na muungano wa Afrika, AU wametia saini mkataba wa makubaliano ya dhamira yao ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika kutimiza malengo muhimu ya afya.

Mkataba huo umetiwa saini leo katika makao makuu ya WHO mjini Geneva, Uswisi na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus na Mwenyekiti wa  Kamisheni ya AU, Moussa Faki Mahamat.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Dkt. Tedros amesema, mkataba huo unalenga mambo matatu muhimu kwa ajili ya ushirikiano, mosi, kutoa mafunzo ya kiufundi kwa shirika la dawa la Afrika kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya kuwezesha uzalishaji wa dawa mashinani. 

Pili kuimarisha ushirikiano kati ya vituo vya uzuiaji na udhibiti wa magonjwa bara Afrika kwa ajili ya kulenga utayari wakati wa dharura kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya kiafya. Mkurugenzi Mkuu huyo ameongeza kwamba,"Mlipuko wa ebola unaoshuhudiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni kumbusho la namna nchi wanachama wa AU wako hatarini ya madhara ya majanga. Kwa muda mrefu dunia imewekeza katika hofu na sio utayari, tunaharakisha kuelekeza pesa kwa mlipuko na pindi unapotokomezwa hatujiandai kuzuia mlipuko mwingine. WHO imedhamiria kufanya kazi na nchi wanachama kuwajengea uwezo kukabiliana na majanga na dharura zingine za kiafya."

Lengo la tatu amesema ni kuunga mkono utekelezaji wa makubaliano ya Addis Ababa kuhusu bima ya afya kwa wote na tamko la AU kuhusu ufadhili wa ndani.

Ili kuwezesha hilo Dkt. Tedros amesema, WHO itasimamia mazungumzo baina ya mawaziri wa fedha na wa afya ili kusaidia nchi kuunda mifumo thabiti na endelevu ya ufadhili wa afya. 

Hata hivyo, amesema ni muhimu kuimarisha mazungumzo na sekta zote za serikali kuzungumzia ni kwa nini watu wanakuwa wagonjwa au kufariki, hewa tunayovuta, chakula tunachokula, maji tunayokunywa na mazingira ambamo tunaishi, kufanya kazi na kucheza.

Dkt. Tedros ameongeza kwamba mambo matatu ya mkataba yanazua changamoto ambazo ni lazima ziangaziwe kwa pamoja kama ndoto ya pamoja ya Afrika yenye afya bora na salama itafikiwa,“mosi, ni lazima tuwekeze katika bidhaa za tiba ambazo ni za viwango vya juu, ni salama na zenye ufanisi.Pili, ni lazima tuwekeze katika maandalizi na sio hofu na tatu ni lazima tuwekeze katika huduma ya afya ya msingi.”

Makubaliano hayo yamekuja wakati muhimu katika kuchagiza huduma ya afya kwa wote.