Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wenye utapiamlo wako hatarini kufa kutokana na magonjwa yatokanayo na uhaba wa maji: UNICEF

Mtoto akichota maji kwenye chanzo ambacho kinamaji kidogo kutokana na ukame uliokausha maziwa huko Dollow Somalia
© UNICEF/Sebastian Rich
Mtoto akichota maji kwenye chanzo ambacho kinamaji kidogo kutokana na ukame uliokausha maziwa huko Dollow Somalia

Watoto wenye utapiamlo wako hatarini kufa kutokana na magonjwa yatokanayo na uhaba wa maji: UNICEF

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF limesema watoto walio katika Pembe ya Afrika na Ukanda wa Sahel wanaweza kufa kwa idadi kubwa iwapo hawata pata misaada ya kibinadamu kwa haraka kwakuwa tayari watoto hao wanakabiliwa na utapiamko mkali na sasa wapo hatarini kupata magonjwa yaenezwajo ya maji.

Idadi ya watu waliokumbwa na ukame katika nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia bila upatikanaji wa maji salama imeongezeka kutoka watoto milioni 9.5 mwezi Februari hadi kufikia watoto milioni 16.2 mwezi Julai mwaka huu, hali inayo waweka watoto na familia zao katika hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa kama vile kipindupindu na kuhara.

Taarifa iliyotolewa na UNICEF kutoka New York Marekani, Darak Senegal na Nairobi Kenya imemnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto Catherine Russell akisema 

“Historia inaonesha wakati viwango vya juu vya utapiamlo mkali kwa watoto vinapochanganyikana na magonjwa hatari ya milipuko kama kipindupindu au kuhara, vifo vya watoto huongezeka sana na kwa kusikitisha. Wakati maji hayapatikani au si salama, hatari kwa watoto huongezeka kwa kasi”.

Mvulana mwenye umri wa mwaka mmoja anayekabiliwa na utapiamlo mkali anapimwa mzunguko wa mkono wake wa juu katika hospitali ya Dolow, Ethiopia.
© UNICEF/Ismail Taxta
Mvulana mwenye umri wa mwaka mmoja anayekabiliwa na utapiamlo mkali anapimwa mzunguko wa mkono wake wa juu katika hospitali ya Dolow, Ethiopia.

Zaidi ya watoto milioni 2.8 katika pembe ya Afrika na Ukanda wa Sahel wanakabiliwa na utapiamlo mkali, ambao ina maana wako katika hatari ya kufa kutokana na magonjwa yanayosababishwa na maji mara 11 zaidi kuliko watoto wanaolishwa vizuri.

Akizungumzia msaada wa kibinadamu unaotolewa amesema katika pembe ya Afrika wamepokea asilimia 3 ya msaada wanao hitaji na katika pembe ya afika wamepokea asilimia 22 pekee. Hali inayofanya “Familia katika maeneo yote yaliyoathiriwa na ukame wanalazimishwa kufanya chaguzi zisizowezekana.

Akichora picha ya hali wanayo pitia wazazi Mkuu huyo wa UNICEF amesema “Hebu fikiria kama mzazi unapaswa kuchagua kati ya kununua mkate au kumnunulia maji mtoto mwenye njaa na kiu ambaye tayari ni mgonjwa, au kati ya kumtazama mtoto wako akipatwa na kiu kikali au kumwacha anywe maji machafu ambayo yanaweza kusababisha magonjwa hatari,”.

Njia pekee ya kukomesha mzozo huu ni kwa serikali, wafadhili, na jumuiya ya kimataifa kuongeza ufadhili ili kukidhi mahitaji makubwa ya watoto, na kutoa usaidizi unaobadilika wa muda mrefu ili kuvunja mzunguko wa mgogoro.

UNICEF inaendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha na huduma za kisekta kwa watoto na familia za wenye mahitaji makubwa katika Pembe ya Afrika na Sahel, ikiwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa maji yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi, huduma za usafi wa mazingira na usafi, kuchimba vyanzo vya kuaminika vya maji chini ya ardhi, matumizi ya mifumo ya jua, kutambua na kutibu watoto wenye utapiamlo, na kuongeza huduma za kinga.

Mgogoro mkubwa wa maji umekumba sehemu kubwa ya Somalia baada ya mvua kutonyesha kwa misimu kadhaa
United Nations
Mgogoro mkubwa wa maji umekumba sehemu kubwa ya Somalia baada ya mvua kutonyesha kwa misimu kadhaa

Magonjwa na vifo vitokavyo na uhaba wa maji

Taarifa hiyo imeeleza watu wengi katika Pembe ya Afrika wanategemea maji yanayoletwa na wachuuzi kwenye lori au mikokoteni ya punda.

Lakini katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ukame, familia nyingi haziwezi tena kumudu kununua maji wakitolea mfano nchini Kenya  katika kaunti 23 zinazokabiliwa a ukame bei ya maji imeongezeka kwa asilimia 400 huko Mandera, na Kaunti ya Garissa bei ikiongezeka kwa asilimia 260 ikilinganishwa na Januari 2021.

Hiko nchini Somalia, milipuko ya kuhara na kipindupindu umeripotiwa takriban katika wilaya zote zilizoathiriwa na ukame, huku wagonjwa 8,200 wakiripotiwa kati ya mwezi Januari na Juni,2022 idadi hii ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya wagonjwa walioripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Katika ukanda wa Sahela nako hali ni tete, nchini Burkina Faso, Chad, Mali, Niger na Nigeria, ukame, vita na ukosefu wa usalama vinasababisha uhaba wa maji, huku watoto milioni 40 wakikabiliwa na viwango vya juu sana vya hatari ya maji. 

Tayari watoto wengi zaidi wanakufa kutokana na maji yasiyo salama na ukosefu wa vyoo unaokabili wananchi walioko katika ukanda wa Sahel kuliko sehemu nyingine yoyote ya dunia, kulingana na Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO.