Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO kutoa orodha ya vijidudu vinavyoweza kusababisha milipuko ya magonjwa siku zijazo

WHO inasisitiza umuhimu wa utafiti kuhusu ugonjwa wa Kifua kikuu hasa kile kilicho sugu dhidi ya dawa.
WHO/S.Ramo
WHO inasisitiza umuhimu wa utafiti kuhusu ugonjwa wa Kifua kikuu hasa kile kilicho sugu dhidi ya dawa.

WHO kutoa orodha ya vijidudu vinavyoweza kusababisha milipuko ya magonjwa siku zijazo

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limesema linazindua mchakato wa kisayansi wa kimataifa ili kusahihisha orodha yake ya kipaumbele cha vijidudu ambavyo vinaweza kusababisha milipuko ya magonjwa au majanga ya milipuko ya kimataifa ili kuongoza uwekezaji wa kimataifa, utafiti na maendeleo (R&D), hasa katika suala la chanjo, vipimo na matibabu. 

Taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo mjini Geneva Uswis imesema likianzia na mkutano uliofanyika Ijumaa iliyopita, Novemba 18, WHO inawakutanisha zaidi ya wanasayansi 300 ambao watazingatia ushahidi kuhusu zaidi ya familia 25 za virusi na bakteria, na vilevile ugonjwa X.  

Ugonjwa X umejumuishwa ili kuashiria vijidudu visiyvojulikana ambayvo vinaweza kusababisha janga kubwa la kimataifa.  

Kwa mujibni wa WHO wataalamu hao watapendekeza orodha ya vijidud vya kipaumbele vinavyohitaji utafiti zaidi na uwekezaji.  

Mchakato huo utajumuisha vigezo vya kisayansi na afya ya umma, pamoja na vigezo vinavyohusiana na athari za kijamii na kiuchumi, ufikiaji wa huduma na usawa. 

Orodha ya kwanza ilitolewa 2017 

Shirika hilo la afya duniani limesema orodha hiyo kwa mara ya kwanza ilitolewa mwaka 2017 na zoezi la mwisho la kipaumbele lilifanyika mwaka wa 2018. Orodha ya sasa inajumuisha pia coronavirus">COVID-19, homa inayosababishwa na virusi ikiambatana na homa kali, kutapika na kupoteza uwezo wa kuona vizuri ilijulikanayo kama Crimean-Cong haemorrhagic fever, ugonjwa wa virusi vya Ebola, homa ya virusi vya Marburg, homa ya Lassa, ugonjwa wa matatizo ya kupumua kwa Mashariki ya Kati (MERS), homa kali ya matatizo ya kupumua (SARS), magonjwa ya Nipah na henipaviral yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama, homa ya bonde la ufa, Zika na ugonjwa X usiojulikana. 

Kwa mujibu wa Dkt. Michael Ryan, mkurugenzi mtendaji wa mpango wa dharura wa afya katika shirika la WHO "Kulenga vijidudu vya kipaumbele na familia za virusi kwa utafiti na maendeleo ya hatua za kukabiliana navyo ni muhimu kwa hatua za kudhibiti mlipuko wa mjanga ya haraka ya kitaifa na kimataifa. Bila kuwepo uwekezaji mkubwa wa R&D kabla ya janga la COVID-19, haingewezekana kuwa na chanjo salama na madhubuti zilizotengenezwa kwa wakati na haraka zaidi.”  

Utafiti na maendeleo R & D 

Kwa vijidudu vya magonjwa ambavyo vitabainika kama kipaumbele  mpango wa WHO wa utafiti na maendeleo au R&D wa magonjwa ya mlipuko hutengeneza mkakati maalum, ambao huweka wazi mapungufu ya maarifa na vipaumbele vya utafiti.  

Na pale inapofaa, wasifu wa bidhaa lengwa, ambao hufahamisha makampuni watengenezaji wa vifaa tiba kuhusu vipimo vinavyohitajika vya chanjo, matibabu na vipimo vya uchunguzi, na kisha hutengenezwa.  

Juhudi pia hufanywa kuweka mwongozo, kukusanya na kuwezesha majaribio ya kitabibu ili kuunda zana hizi.  

Juhudi za ziada kama vile kuimarisha uangalizi wa udhibiti na maadili pia huzingatiwa. 

Dkt. Soumya Swaminathan, mwanasayansi mkuu wa WHO amesema "Orodha hii ya vijidudu vya kupewa kipaumbele imekuwa ndio kitovu kwa jumuiya ya utafiti kuhusu wapi pa kutia nguvu zaidi ili kudhibiti tishio lijalo la magonjwa ya milipuko.” 

Ameongeza kuwa “ Orodha hii imeandaliwa kwa pamoja na wataalam katika uwanja huo na ndio mwelekeo uliokubaliwa ambapo sisi kama jumuiya ya kimataifa ya utafiti tunahitaji kuwekeza nguvu zetu na fedha ili kutengeneza vipimo, matibabu na chanjo. Tunawashukuru wafadhili wetu kama vile serikali ya Marekani, washirika wetu, na wanasayansi wanaofanya kazi na WHO kuwezesha suala hili.”