Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nitarina asali na kuuza dumu moja dola 50- Mnufaika wa mafunzo Sudan Kusini

Familia za waliokimbia makaiz yao sababu ya machafuko wakiwa wamepata hifadhi huko Tambura nchini Sudan Kusini
UNMISS
Familia za waliokimbia makaiz yao sababu ya machafuko wakiwa wamepata hifadhi huko Tambura nchini Sudan Kusini

Nitarina asali na kuuza dumu moja dola 50- Mnufaika wa mafunzo Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Sudan Kusini, zaidi ya wakimbizi 50 waliorejea nyumbani pamoja na wakimbizi wa ndani eneo la Tambura jimboni Equatoria Magharibi wamenufaika na mafunzo ya stadi za kuwawezesha kupata kipato, mafunzo yaliyotolewa kwa pamoja na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani Sudan Kusini ,UNMISS na shirika la kiraia la wanawake, ANIKA. Tupate maelezo kamili kutoka kwa Assumpta Massoi. 

Kuni zinakolea, sufuria inapata moto na sauti ni za wakimbizi wa ndani wakikoroga sufuria yenye mchanganyiko wa kutengeneza mafuta na sabuni za mwili pamoja na sabuni za kusafisha vyombo. Hapa ni Yambio nchini Sudan Kusini.

Hawa nao ni wanafunzi wengine wa kutengeneza mizinga ya nyuki, tayari kuitundika na kuanza kurina asali. 

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani Sudan Kusini, UNMISS unasema mafunzo haya ya miezi mitatu yalikuwa ni muhimu kwa ajili ya maridhiano na kujijenga upya kwa sababu wanufaika hawa waliathiriwa na mapigano ya mwaka jana ambapo makumi ya maelfu walipoteza makazi na wengine wengi waliuawa. 

Miongoni mwa wanufaika ni Lilian Ngbapai, mama wa watoto wawili, na mumewe aliuawa wakati wa mapigano Tambura. 

Walinda amani wa UNMISS wakiwa katika ulinzi Sudan Kusini. (Maktaba)
UNMISS
Walinda amani wa UNMISS wakiwa katika ulinzi Sudan Kusini. (Maktaba)

Lilian anasema, “Mapigano yalinikuta Tambura, na nimeona mambo mengi mabaya. Ndugu zangu pia waliuawa; dada, mjomba, ndipo nikakimbilia Yambio. Nilipopata taarifa kuhusu haya mafunzo kwa ajili ya wakimbizi wa ndani, niliamua kujiunga. Mafunzo haya yana manufaa makubwa kwangu na familia. Sasa nafahamu kutengeneza sabuni, mafuta ya kupaka mwilini, mafuta ya kusafisha nywele. Na nitaanzisha biashara yangu.” 

Kwa upande wa mafunzo ya ufugaji nyuki, shuhuda ni Vincent Arkangelo, aliyerejea Sudan Kusini mwaka 2021 na kukumbana tena na ghasia Tambura. 

Vincent anasema, “Kwa kweli ninaamini mafunzo haya yatanisaidia sana mimi na jamii yangu kwa sababu nimejifunza mbinu za kisasa za ufugaji nyuki. Nitafundisha jamii yangu kwa sababu najua ufugaji nyuki ni mbinu ya kujipatia kipato. Nitatengeneza mizinga na Mungu akipenda nitarina asali. Nikiuza sokoni dumu moja ni sawa na dola 50.” 

UNMISS inaamini kuwa mradi huu utakuwa kichocheo cha amani ya kudumu na wanufaika kwa upande wao watakuwa wachechemuzi wa utulivu na maendeleo.