Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatuna matumaini ya maisha yetu na watoto wetu - Wakimbizi Sudan kusini  

Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini
UNMISS
Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini

Hatuna matumaini ya maisha yetu na watoto wetu - Wakimbizi Sudan kusini  

Wahamiaji na Wakimbizi

Video ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS inaonesha msururu wa watu na virago vyao, wengi wao wanawake na watoto, wakiwasili katika makazi ya muda yaliyoanzishwa kwenye eneo la ujumbe huo wiki chache zilizopita baada ya kuibuka kwa machafuko huko Tambura, jimboni Equatoria Magharibi. 

Marcella Barangba anasimulia yaliyowakumba. “Mimi ni mmoja wa watu ambao tumekimbia maeneo yetu kutokana na mzozo wa hivi majuzi. Tuna shida kubwa. Tunakaa katika hali duni sana na watoto wetu hawana chakula. Tumekata tamaa. Ninawasihi washambuliaji wenye silaha ambao wanafanya hivyo kwetu kuacha vurugu ili tuweze kuishi kwa amani na umoja. Hebu fikiria na msimu huu wa mvua, tutakaa wapi na watoto wetu? wamepora na kuchoma vituo vyote vya afya, tutapata wapi dawa za kututibu sisi na watoto wetu? maana baadhi ya watoto tayari ni wagonjwa.” 

Msimamizi wa Ofisi ya UNMISS Christopher Murenga anasema machafuko yamesababisha vituo vya kuhifadhi wakimbizi sasa kufikia vinne katika eneo hilo 

“Kufuatia mapigano ambayo yalitokea mwishoni mwa wiki iliyopita, kulikuwa na msururu mrefu wa watu wanaoyakimbia makazi yao ambao wamefika kwenye kituo chetu cha muda cha doria, wanatafuta makazi na pia mahali salama. Kwa sababu ya wingi, tuliwawahamishia katika eneo letu la kambi ya zamani hapa Tambura. Tunatarajia kupata msaada wa kibinadamu katika eneo hili.” 

Wanajeshi walipofanya doria katika vijiji ambako wananchi wamekimbia wamekuta nyumba zimechomwa moto. 

“Uharibifu umekuwa mkubwa. Tunajaribu kuzuia uharibifu zaidi kwa kufanya kazi na serikali kuu na za mitaa, vyombo vya usalama na washirika wengine katika kujaribu kudhibiti hali hii na kuhakikisha kuwa inakoma. Inasikitisha sana kuona kwakiasi gani uharibifu mkubwa umefanyika na watu wengi ambao walikuwa wakitarajia amani baada ya kutiwa saini kwa Mkataba wa Amani lakini sasa wamekosa kabisa matumaini.” 

 Mkimbizi mwingine, Lucia Alfred anasema amepoteza matumaini,“Mambo mabaya mengi yametutokea, hasa akinamama wenye watoto wadogo. Tuko katika hali ngumu sana. Tunataka kujua serikali yetu na ulimwengu wote unafikiria nini juu ya maisha yetu ya baadaye? Hawa watoto hapa, maisha yao ya baadae yatakuwaje?, wanahitaji kupewa nafasi ya kuishi kwa amani na sisi kuweza kulima katika ardhi yetu. “ 

UNMISS inaendelea na juhudi za kushirikiana na viongozi wa serikali na wadau wa masuala ya kibinadamu kuwalinda na kuwapatia mahitaji wakimbizi hao wa ndani.