Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimejifungua wiki 3 sasa, bado natokwa damu, hospitali hakuna dawa- Mkimbizi Sudan Kusini

Machafuko yamesababisha watu kukimbia maeneo ya vijijini karibu na Yei jimbo la Equatoria kati, Sudan Kusini.
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Machafuko yamesababisha watu kukimbia maeneo ya vijijini karibu na Yei jimbo la Equatoria kati, Sudan Kusini.

Nimejifungua wiki 3 sasa, bado natokwa damu, hospitali hakuna dawa- Mkimbizi Sudan Kusini

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashirika ya kibinadamu yakiongozwa na shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, yanaendelea kutoa msaada wa chakula kwa wakimbizi wa ndani waliokimbia makazi yao Equatoria Magharibi Sudan Kusini kufuatia mashambulizi ya silaha.

Ni mkimbizi Julia Sali akishukuru kwa msaada alioupata anasema, "tumekuwa tukiteseka, tukikimbia kutoka sehemu moja hadi nyingine bila chakula, lakini leo nashukuru Umoja wa Mataifa kwa sababu wametuokoa kwa chakula. Nina furaha sana." 

Taarifa ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS inasema wanawake, watoto na wazee walikimbia kwa kilometa 14 na wamepiga kambi shuleni na katika kiwanja cha kanisa katika eneo laTambura. 

Watu wanasema kwamba hawakuwa na hiari zaidi ya kuacha kila kitu chao na kukimbia wakati vikundi vyenye silaha vilipovamia kwenye vijiji vyao, wakichoma vibanda vyao na kutapanya risasi hewani. Mama wa miaka 13, Karmela Gerio mwenye umri wa miaka 36 mama wa watoto 13, kabla ya kupokea msaada, akisimulia jinsi alivyotoroka eneo la tukio wakati huo akiwa mjamzito wa kujifungua wakati wowote anasema, “Ninaishi na watoto wangu wote hapa kanisani. Nilijifungua wiki tatu tu zilizopita na bado ninatokwa damu, bado sijisikii vizuri. Siwezi kwenda hospitali na hata hivyo hakuna dawa huko. Chakula ni shida. Tangu asubuhi, watoto wangu hawajala; wanalilia chakula lakini sina chakula cha kuwapa. Nahisi kuzimia nikijaribu kusimama na siwezi kutembea. Hata nikifanikiwa kurudi nyumbani, sijui itakuwaje kwangu. " 

Angalau kwa sasa, misaada ya kibinadamu kutoka Umoja wa Mataifa imehakikisha kuwa watoto hawalali na njaa.  Magdelina Casemiro ni mmoja wa waliokwisha kupokea msaada anasema,"Kibanda changu kiliteketezwa na kila kitu ndani yake lakini leo ninafurahi kupokea vyakula hivi. Watoto wangu wanaweza kula kitu leo.” 

Afisa wa Haki za Binadamu wa UNMISS Leticia Mariano ni sehemu ya timu ambayo iko katika eneo ikifanya uchunguzi wa matukio hayo anasema kuwa walinda amani wanazidisha doria ndani na karibu na Tambura ili kuzuia vurugu zaidi. "Tuna watu kadhaa ambao bado hawajulikani waliko na hii inasikitisha sana. Wengine wanatafuta waume zao, baba zao, na watoto wao ambao wamepotea. Mbali na hayo, tuna uharibifu wa vitu. Hawa wakimbizi wa ndani, maelfu yao wamepoteza kila kitu. Wamepoteza nyumba zao ambazo ziliteketezwa kama unavyoona hapa.  Zimeteketezwa kabisa hadi chini. Wamepoteza mali zao zote, wamepoteza mazao yao, mbuzi wao na kuku wanazurura tu. Lazima waanze maisha kuanzia sifuri ambayo ni kiwango kikubwa cha kiwewe na bado hawajui ni nini kilitokea kwa familia zao. Kwa hivyo, ni hali ya wasiwasi sana.”