Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 10 wako hatarini kutokana na ukame Pembe ya Afrika:UNICEF

Usambazaji wa msaada wa chakula na WFP katika jamii Ethiopia.
© WFP/Claire Nevill
Usambazaji wa msaada wa chakula na WFP katika jamii Ethiopia.

Watoto milioni 10 wako hatarini kutokana na ukame Pembe ya Afrika:UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Takribani watoto milioni 10 wameathirika vibaya na ukame Pembe ya Afrika kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo sasa linahaha kusaka dola milioni 250 ili kunusuru maisha ya watoto hao na mustakbali wao.

Hali ni dhahiri shairi ukame umetamalaki kila kona, mazao yamekauka na watoto wamekumbwa na utapiamlo mkali kutokana na lishe duni.  

UNICEF inasema hali hii haijawahi kushuhudiwa kwa miaka 40 nchini Ethiopia, Kenya na Somalia na sasa watoto milioni 1.7 wanahitaji matibabu ya haraka kwa ajili ya unyafuzi unaowakabili na idadi inatarajiwa kuongezeka 

Shirika hilo linasema hili ni janga juu ya janga lakini hatua za haraka na za pamoja zinaweza kusaidia kuepusha zahma kubwa zaidi kwani mshikamano wa mwaka 2017 ulisaidia kuepusha janga la baa la njaa na kuokoa maisha ya maelfu ya watu wakiwemo watoto. Catherine Russell ni mkurugenzi mtendaji wa UNICEF mwishoni mwa wiki alikuwa Ethiopia kushuhudia hali halisi anasema,“UNICEF na washirika wake tunahitaji haraka dola milioni 250 kuokoa maisha ya watoto na mustakbali wao. Hatua zetu lazima zijumuishe sekta mbalimbali na ziende mbali zaidi ya kukabili uhakika wa chakula, zijumuishe WASH, lishe, huduma za afya, huduma za elimu na msaada” 

Ameongeza kuwa msaada huo unahitaji pia kupigwa jeki na uwekezaji katika kujenga mnepo, kuhimili mabadiliko ya tabianchi na programu za kuzisaidia jamii kukabili hali inayobadilika kila uchao. 

Amesisitiza kuwa pamoja na changamoto zingine lukuki zinazoikumba dunia hivi sasa ikiwemo vita ya Ukraine dunia isiipe kisogo Pembe ya Afrika kwani bado fursa ipo ya kuzuia zahma kubwa na kunusu maisha sasa na wala si kesho.