Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaanzisha kituo maalum cha kusaidia wananchi wa Pembe ya Afrika

Rekodi ya watu milioni 11.7, karibu robo ya wakazi wa Sudan, wanatarajiwa kukabiliwa na njaa katika kilele cha msimu wa mwambo mwezi Septemba.
©FAO/Ahmedalidreesy Adil
Rekodi ya watu milioni 11.7, karibu robo ya wakazi wa Sudan, wanatarajiwa kukabiliwa na njaa katika kilele cha msimu wa mwambo mwezi Septemba.

WHO yaanzisha kituo maalum cha kusaidia wananchi wa Pembe ya Afrika

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO limetangaza kuongeza shughuli zake katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuanzisha kituo maalum cha huduma jijini Nairobi nchini Kenya wakati huu eneo hilo likikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula unaosababishwa na migogoro, matukio mabaya ya mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na ukame mbaya zaidi kushuhudiwa katiak kipindi cha miaka 40, kupanda kwa bei ya chakula kimataifa pamoja na bei ya mafuta.

Taarifa ya kuanzishwa kwa kituo hicho imetolewa katika mkutano wa siku mbili wa WHO ( Juni 26 -27) uliofanyika jijini Nairobi nchini Kenya ambapo mkurugenzi mkuu msaidizi wa WHO kitengo cha mwitikio wa dharura Dkt. Ibrahima Socé Fall alieleza kuwa kituo hicho kinalenga kupanga namna ya kuzisaidia nchi saba zilizo na dharura ya kiafya zilizopo katika pembe ya Afrika ambazo ni Ethiopia, Somalia, Kenya, Djibouti,Sudan Kusini, Sudan na Uganda pamoja na kuratibu kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine.
 
Kwa mujibu wa WHO changamoto zilizotajwa hapo juu zimesababisha zaidi ya watu milioni 80 wanaoishi Katika ukanda huo kukosa uhakika wa chakula huku utapiamlo ukiongezeka hususan kwa watoto pamoja na kuongezeka kwa mahitaji mengine ya kiafya ikiwemo maji safi na hivyo familia kujikuta zikihaha kusaka chakula, huduma za afya na kuwa hatarini kupata magonjwa ya milipuko. 
 
Dkt Socé Fall amesema Shirika hilo limefungua kituo hicho kwakuwa “Gharama za kutochukua hatua ni kubwa,” akifafanua kuwa “Wakati kipaumbele kilicho wazi kabisa ni kuzuia watu watoke kwenye njaa, lazima wakati huo huo tuimarishe mwitikio wetu wa kiafya ili kuzuia magonjwa na kuokoa maisha. Hata maisha ya mtu moja yakipotea kutokana na ugonjwa unaozuilika kwa chanjo, kuhara, au matatizo ya kiafya kutokana na utapiamlo katika ulimwengu wa leo ni maisha ya watu mengi sana.”
 
Amesema kituo hiki kitasaidia kuratibu mwitikio wa mahitaji ya wananchi na kuandaa utoaji wa vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha katika maeneo vinapohitajika zaidi lengo likiwa ni kuhakikisha watu walioathirika wanaweza kupata huduma muhimu za afya, kutibu watoto wagonjwa wa utapiamlo mkali, kuzuia, kugundua, kutibu na kukabiliana na magonjwa ya milipuko ya kuambukiza.
Changamoto za kiafya zinatofautiana baina ya nchi na nchi, mfano nchini Uganda changamoto ipo kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo wakati nchini Sudan Kusini asilimia 60ya wananchi wake wakikabiliwa na njaa. 
 
Pamoja na kutofautiana hapa na pale , nchi zote saba (Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda) zinakabiliana na milipuko ya surua na kipindupindu.