Kama ilivyo kwa Nafaka, Mbolea pia inahitajika katika soko la dunia: Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwa katika meli ya majaribio kupitia bahari ya Marmara nchini Uturuki ili kumtazama Kamanda Jasiri.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwa katika meli ya majaribio kupitia bahari ya Marmara nchini Uturuki ili kumtazama Kamanda Jasiri.

Kama ilivyo kwa Nafaka, Mbolea pia inahitajika katika soko la dunia: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo nchini Uturuki ametembelea na kukagua shughuli zinazoendelea za ukaguzi wa meli kutoka Ukraine zenye shehena ya nafaka zinazoenda kuuzwa katika soko la kimataifa na kupongeza muungano wa wakaguzi hao kutoka Ukraine , Urusi, Uturuki na Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri wanayofanya ambayo itasaidia dunia kuondokana na upungufu wa chakula uliosababisha bei kupanda na kuathiri zaidi nchi zinazoendelea zenye rasilimali chache kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi wake. 

Hii leo asubuhi na mapema Katibu Mkuu Guterres alitembelea kituo cha uratibu wa pamoja cha mpango wa Nafaka wa Bahari nyeusi - JCC.

Baada ya kuwasili, Katibu Mkuu alipanda boti ya majaribio katika Bahari ya Marmara ambako alisafiri  mpaka kufika karibu na meli ijulikanayo MV Brave Commander, hii ni meli ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP ambayo ilichukua zaidi ya ngano tani 23,000 huko Yuzhny/Pivdennyi Ukraine na inapeleka nafaka hizo pembe ya Afrika kusaidia watu wanaokabiliwa na njaa kutokana na ukame mkali uliolikumba eneo hilo. 

Mjini Istanbul, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anaangalia meli ya WFP SSI Invincible 2, ikielekea Ukraine kuchukua shehena kubwa zaidi ya nafaka ambayo bado inasafirishwa nje ya nchi chini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.
UN Photo/Mark Garten
Mjini Istanbul, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anaangalia meli ya WFP SSI Invincible 2, ikielekea Ukraine kuchukua shehena kubwa zaidi ya nafaka ambayo bado inasafirishwa nje ya nchi chini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.

Ziara eneo la ukaguzi wa meli

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ambaye mwezi Julai alikuwa nchini Uturuki kuongoza utiaji saini baina ya Ukraine na Urusi licha ya nchi hizo mbili kuwa katika vita tangu mwezi Februari mwaka huu kuruhusu Nafaka na Mbolea kusafirishwa kwenye soko la dunia kupitia Bahari Nyeusi kwa sharti la kila meli kutoka Ukraine kupita kituoni hapo kwa ajili ya kukaguliwa ili zisibebe magendo alijiunga na kundi la wakaguzi kutoka Kituo cha Uratibu wa Pamoja na kupanda pia meli ya SSI INVINCIBLE II.

Meli hiyo iko njiani kuelekea Chornomorsk nchini Ukraine kupakia karibu tani 50,000 za nafaka hii itakuwa ni shehena kubwa zaidi kuondoka Ukraine tangu kuanza kwa vita. 

Akiwa kituoni hapo pia alikutana kwa nyakati tofauti tofauti na wajumbe wa Urusi na Ukraine na kisha kuwa na kikao rasmi cha JCC ambapo aliwashukuru washiriki wote kwa weledi wao na utekelezaji wa kazi hii ya kibinadamu katika kuhakikisha kuwa mpango huu unafanikiwa na kunufaisha watu wote ulimwenguni.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia katika Kituo cha Uratibu wa Pamoja huko Istanbul, Uturuki.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia katika Kituo cha Uratibu wa Pamoja huko Istanbul, Uturuki.

Pongezi kwa timu ya ukaguzi 

Mara baada ya kutembelea kituo cha ukaguzi Katibu Mkuu Guterres alirejea njini Instabul na kufanya mkutano na waandishi wa habari tukio alilojumuika na Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Hulusi Akar ambapo mosi aliishukuru serikali ya Uturuki kwa jukumu lake kuu katika Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.

“Ninakushukuru zaidi kwa jukumu lako muhimu katika Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.  Kiini cha mpango huu ni Kituo cha Uratibu wa Pamoja ambacho huwezesha usafirishaji salama wa meli kadhaa za kibiashara.” Alisema Guterres wakati akimshukuru Waziri wa Ulinzi wa Uturuki.

Akiisifu timu ya ukaguzi mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema kila mjumbe katika JCC awe kutoka Ukraine , Urusi, Uturuki au Umoja wa Mataifa amefanya kazi nzuri kwani kwa pamoja  wamekuwa wakifanya kazi kwa kujitolea na taaluma kuleta ujuzi wao wa kipekee na shauku ya kuunga mkono kazi hii muhimu.

“Juhudi hizi zinaonesha kile tunachoweza kufikia tukiwana utashi wa kisiasa, utaalamu wa hali ya juu wa utendaji kazi, na juhudi za pamoja.” Alisema na kuongeza kuwa “Ningependa hasa kumtambua kaimu mratibu wetu wa timu ya Umoja wa Mataifa Frederick Kenney kwa kujitolea na bidii yake katika Mpango huu. Na ninamkaribisha, Amir Abdulla, ambaye nimemteua kama Mratibu wa kuongoza timu ya Umoja wa Mataifa. Analeta utaalam wa miongo kadhaa katika shughuli ngumu za kibinadamu.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwa katika meli ya majaribio kupitia bahari ya Marmara nchini Uturuki ili kumtazama Kamanda Jasiri.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwa katika meli ya majaribio kupitia bahari ya Marmara nchini Uturuki ili kumtazama Kamanda Jasiri.

Bila mbolea 2023 hali itakuwa mbaya

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa aliwaeleeza wana habari kile alichoone mapema hii leo alipotembelea kuona meli ya zinazokaguliwa  kwenye Bahari ya Marmara na kuongeza kwamba aliachokiona hapa Istanbul na Odesa ni sehemu tu ya makubaliano ya suluhisho linalohitajika katika oko la dunia. 

Alitaja sehemu nyingine ya mpango huo ulio sainiwa mwezi Julai ni kuhakikisha mbolea kutoka Urusi inafika katika soko la dunia ili iweze kuwafikia wakulima duniani kote.
"Bila ya mbolea mwaka huu 2022, kunaweza kusiwe na chakula cha kutosha mwaka wa 2023," Guterres alisema, "kupata chakula na mbolea zaidi kutoka Ukraine na Urusi ni muhimu ili kuleta utulivu katika masoko ya bidhaa na bei ya chini kwa watumiaji."

Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu juhudi za kuhakikisha mbolea kutoka Urusi inaondolewa vikwazo katika soko la kimataifa alisema “Nimekuwa nikisema mara kwa mara, na imekuwa ikiwekwa wazi na nchi zilizoweka vikwazo kwamba havihusu chakula na mbolea. Lakini bila shaka, kuna athari ya kutisha katika sekta binafsi na kuna idadi fulani ya vikwazo na matatizo ambayo yanahitaji kuondolewa kuhusiana na meli, kuhusiana na bima na kuhusiana na fedha. Na ninaweza kukuambia kuwa tunafanya kazi kwa bidii kwa ushirikiano na Marekani na Muungano wa Ulaya ili kuweza kuondoa vikwazo hivyo na kuruhusu kile tunachokiona kuwa ni muhimu sana kwa wananchi hasa katika nchi zinazoendelea.”

Guterres amesema kwa sasa wako mwanzoni mwa mchakato mrefu zaidi, lakini tayari umeonesha uwezo wa makubaliano haya muhimu kwa ulimwengu. “Niko hapa na ujumbe wa pongezi kwa wale wote katika Kituo cha Uratibu wa Pamoja na ombi kwa kazi hiyo muhimu ya kuokoa maisha iendelee. “ alihitimisha hotuba yake huku akiahidi Umoja wa Mataifa kuendelea kujitolea kikamilifu ili kufikia malengo ya makubaliano yao.