Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi wa misaada wanaokoa maisha katika hali ya hatari: Siku ya Usaidizi wa Kibinadamu Duniani

Watoto hujificha na kulala chini ya karatasi za plastiki baada ya tetemeko la ardhi la kipimo cha 5.9 kupiga Mkoa wa Paktika nchini Afghanistan.
© UNICEF/Ali Nazari
Watoto hujificha na kulala chini ya karatasi za plastiki baada ya tetemeko la ardhi la kipimo cha 5.9 kupiga Mkoa wa Paktika nchini Afghanistan.

Wafanyakazi wa misaada wanaokoa maisha katika hali ya hatari: Siku ya Usaidizi wa Kibinadamu Duniani

Msaada wa Kibinadamu

Katika Siku ya usaidizi wa kibinadamu Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 19 Agosti, wafanyakazi wa misaada Ahmad Alragheb, anayeishi nchini Syria, na Veronica Houser, aliyeko Afghanistan, wanazungumza kuhusu juhudi muhimu za kibinadamu katika nchi hizi, na changamoto wanazokabiliana nazo wao na wenzao.

Syria, ambako waliokimbia makazi wanasaidia waliokimbia makazi yao
"Wafanyakazi wa mashirika ya kibinabinadamu wanajiweka katika hali zisizo salama sana kuokoa watu, lakini hakuna chaguo lingine", anaelezea Ahmad Alragheb, meneja wa mpango wa usalama wa chakula wa NGO ya Mercy-USA nchini Syria, moja ya nchi zilizo na hali ya hatari zaidi.

"Misaada ya kibinadamu inalengwa na wakundi ya wapiganaji kwa sababu inaunga mkono watu wanaojaribu kuwa wastahimilivu", anasema Alragheb, ambaye mwaka 2019 alifurushwa kutoka mji alikozaliwa wa Idlib, Syria, baada ya serikali kuliteka eneo hilo.

Wafanyakazi wengi wa misaada ya kibinadamu wameuawa katika taifa hilo la Mashariki ya Kati, hata hivyo wanaendelea kutoa msaada kwa watu, na kuwazuia wengi kufa kwa njaa.
Syria tete, ambayo imekuwa ikikumbwa na msukosuko wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muongo mmoja, imeshuhudia takriban watu milioni mbili wakiacha makazi yao kutafuta hifadhi katika maeneo mengine.

Shirika la Mercy-USA, kwa ushirikiano na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), mara kwa mara huvuka mpaka wa Syria kutoka ofisi zao nchini Uturuki kutoa msaada wa chakula kwa Wakimbizi wa Ndani 200,000 na malazi kwa raia 1,396 katika kambi15 nchini humo. Hili linawezekana kutokana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloruhusu wahudumu wa kibinadamu kuvuka kwa usalama mpaka wa Syria kutoka sehemu tofauti.

Wakimbizi wa ndani nchini Syria wakiwa wamejipanga mstari tayari kwa kupokea msaada wa kibinadamu
Mercy-USA / Ammar Abo Alnoor
Wakimbizi wa ndani nchini Syria wakiwa wamejipanga mstari tayari kwa kupokea msaada wa kibinadamu

Mojawapo ya masuala muhimu yanayowakabili wakimbizi wa ndani ni kwamba mahema wanamoishi yametengenezwa kwa ajili ya kudumua kwa mwaka mmoja tu. Hata hivyo, ni vigumu kiuchumi kuyabadilisha kila mwaka, na baadhi ya wakimbizi wa ndani wamekuwa wakiishi katika hema moja kwa miaka mitano.

Takriban asilimia 80 ya watu waliokimbia makazi yao ni watoto na wanawake, kundi ambalo ni hatari sana; Faragha ya wanawake ni jambo muhimu na mahema mengi, na kuishi pamoja na watoto wao, haiwapi nafasi salama ya kujistiri, au kupata ulinzi dhidi ya uchokozi, na sio mahali pazuri pa kuishi kwa baadhi ya wanawake, hawawezi hata kuvua hijabu zao kwa muda wa miezi kadhaa kwa vile kila mara wapo wazi na wanaweza kuangaliwa.

Alragheb anaeleza kwamba watu wamepoteza mali zao zote, hawana mahali pa kurejesha maisha yao ya kawaida, na ni vigumu kwao kupata kazi nchini Syria, ambayo inakabiliwa, "kutokuwa na mwisho. mzunguko wa matatizo” ameeleza.

Mfanyikazi wa UNICEF Veronica Houser akizungumza na Waafghani.
Sayed Habib Bidel
Mfanyikazi wa UNICEF Veronica Houser akizungumza na Waafghani.

Mapambano ya elimu kwa wanawake nchini Afghanistan

Msukumo wa kuwasaidia wengine unaweza kuwa na nguvu ya kutosha kuwafanya watu waache faraja na usalama wa nyumba zao, na kuelekea mahali penye mgogoro mkubwa ili kupigania haki za binadamu za watu wanaoishi huko.

Hii ilikuwa ndio hali iliyomkuta Veronica Houser, ambaye alihama kutoka Marekani hadi kwenye ujumbe wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Afghanistan, miezi miwili baada Taliban kutwaa mamlaka mjini Kabul Agosti mwaka 2021. "Nilihisi tofauti kati ya fursa niliyokuwa nayo pale nilipozaliwa, ikilinganishwa na ukiukwaji wa haki za wanawake wengine", anasema.

Akiwa amewahi kufanya kazi nchini Rwanda na Sudan Kusini, alitarajia kuleta mabadiliko nchini Afghanistan kwa kuchapisha hadithi na kupaza sauti za wale ambao hawasikiki mara kwa mara.

Moja ya maswala makuu ya ujumbe wa UNICEF ni kupigwa marufuku kwa wasichana kwenda shule za upili, nchi pekee ulimwenguni ambapo hii hufanyika. Wengi wa wasichana wanakataa kukata tamaa, na wanadumisha matumaini kwamba shule zitafunguliwa hivi karibuni.

Wakati huo huo, UNICEF inasambaza mamilioni ya vitabu vya kiada na vifaa vya shule majimboni, na inajenga nafasi mpya za elimu inaporuhusiwa. Shirika la Umoja wa Mataifa limeanzisha maeneo rafiki kwa wanawake na wasichana ambapo watoto wanaweza kucheza, wanawake wanaweza kujieleza, na kupata usaidizi wa kisaikolojia na kijamii.
"Mgogoro wa elimu pia ni ulinzi na shida ya afya ya akili", anasema Houser. "Wasichana hawa hawawezi kuona marafiki zao, hawajui maisha yao ya baadaye yatakuwaje, wanahisi wasiwasi, na wengine hata kuingia kwenye ndoa za utotoni".

Wanawake wakipokea mgao wa chakula katika eneo la usambazaji wa chakula huko Herat, Afghanistan.
© UNICEF/Sayed Bidel
Wanawake wakipokea mgao wa chakula katika eneo la usambazaji wa chakula huko Herat, Afghanistan.

Inahitajika juhudi za Kijiji kizima

Siku ya Usaidizi wa Kibinadamu duniani inatukumbusha jinsi kazi ya usaidizi wa kibinadamu ilivyo hatari, lakini muhimu. Miaka 19 iliyopita, wenzao 22 waliuawa katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Baghdad. 
Katika kukumbuka shambulio hili baya la tarehe 19 Agosti, jumuiya ya kibinadamu inatoa pongezi kwa wale ambao wamepoteza maisha yao kusaidia wale walio hatarini katika migogoro duniani kote.
Mwaka jana 2021 wafanyakazi wa misaada 141 waliuawa duniani kote, idadi kubwa zaidi tangu 2013. 
Licha ya hatari zote, wahudumu wa kibinadamu wanaendelea na shughuli zao huku idadi ya watu walioathiriwa na majanga ikifikia rekodi ya juu.
Kuwepo kwa wasaidizi wa kibinadamu wa kitaifa ni kwamba wote isipokuwa wawili wa wafanyakazi waliouawa mwaka jana, duniani, walikuwa wanatoka katika nchi waliyofanya kazi.
Kauli mbiu ya Siku ya usaidizi wa Kibinadamu Duniani kwa mwaka huu ni #Ittakesavillage ikimaanisha inahitaka juhudi za kijiji kizima, ikirejelea methali ya Kiafrika “Inahitaji kijiji kulea mtoto”, ikimaanisha jinsi jamii nzima inavyoweza kufanya kama kijiji cha kimataifa kusaidia watoto, na wanadamu, kuishi katika mazingira salama na malezi.