Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko wanaojitolea kusaidia wengine hata wenyewe wakiwa kwenye shida- Guterres

Msaada wa kisaikolojia pia ni muhimu kwa wale wanaokumbwa na majanga. Pichani mnasihi wa kisaikolojia kutoka IOM akiwaelekeza wanawawake kuvuta pumzi ndani na nje kama sehemu ya kuondoa msongo wa mawazo.
IOM/Léo Torréton
Msaada wa kisaikolojia pia ni muhimu kwa wale wanaokumbwa na majanga. Pichani mnasihi wa kisaikolojia kutoka IOM akiwaelekeza wanawawake kuvuta pumzi ndani na nje kama sehemu ya kuondoa msongo wa mawazo.

Heko wanaojitolea kusaidia wengine hata wenyewe wakiwa kwenye shida- Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Hii leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya utoaji wa misaada ya kibinadamu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepazia sauti watoa huduma za kibinadamu ambao hufanya kazi kutwa kucha ili dunia iwe pahala bora hasa wale wanaopitia majanga wanaojikuta wao wenyewe wakibeba jukumu la kutoa msaada. 

Katika ujumbe wake aliotoa kwa njia ya video hii leo, Katibu Mkuu ametumia methali isemayo yahitaji Kijiji kukuza mtoto, akiongeza kuwa yahitaji pia Kijiji kusaidia watu wanaokumbwa na majanga ya kibinadamu.

Kijiji hiki kinajumuisha waathirika ambao kila wakati wao ndio wa kwanza kuchukua hatua pale janga linapotokea; majirani wakisaidia majirani. Inajumuisha pia jamii ya kimataifa ambayo inaungana kusaidia watu hao wakati wanajikwamua na kujijenga upya.

Amesema wengine ni mamia ya maelfu ya watu binafsi watoa misaada wakiwemo wanaojitolea na watu wabobevu kwenye tasnia zao wakitoa huduma za afya na elimu, maji na chakula, malazi na ulinzi, msaada wa matumaini.

Katibu Mkuu amesema watoa misaada hao huweka maisha yao rehani wakitekeleza majukumu hayo katika maeneo hatari zaidi hata kuweza kufikirika.

Naomi akiwa kwenye kioski tayari kuchukua fedha taslimu za msaada kutoka WFP
© WFP/Andy Higgins
Naomi akiwa kwenye kioski tayari kuchukua fedha taslimu za msaada kutoka WFP

“Leo hii idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu imekuwa kubwa kuliko wakati wowote,” amesema Katibu Mkuu akitaja sababu kuwa ni mizozo, mabadiliko ya tabianchi, COVID-19, umaskini, njaa na kiwango kisicho cha kawaida cha ukimbizi wa ndani. 

Amesema katika siku ya leo ya usaidizi wa kibinadamu, hebu na tuwafurahie wasaidizi wa kibinadamu kokote waliko. Ujasiri wao, na vile vile tuwakumbuke wale waliopoteza maisha wakitekeleza jukumu hilo la kiutu.

Siku ya usaidizi wa kibinadamu duniani ilitengwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2008 kufuatia shambulio la ofisi ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Baghdad, Iraq mwaka 2003, shambulio lililoua wahudumu wa kibinadamu 22.