Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunasema asante kwa wahudumu wa kibinadamu kokote waliko katika kuokoa maisha-OCHA

Mwanamke mjamzito akipokea huduma ya matibabu katika kliniki ya afya ya muda mfupi nchini Nigeria.
© 2018 European Union
Mwanamke mjamzito akipokea huduma ya matibabu katika kliniki ya afya ya muda mfupi nchini Nigeria.

Tunasema asante kwa wahudumu wa kibinadamu kokote waliko katika kuokoa maisha-OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibindamu na masula ya dharura OCHA, imeeleza kuwa janga la virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19 limeongeza machungu katika changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo watoa huduma za kibinadamu kote duniani

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi na New York Marekani, OCHA imesema, “leo siku ya utu wa kibinadamu, dunia inawaenzi watoa huduma za kibinadamu, wengi wakiwa wanafanya kazi katika jamii zao, ambao wanaenda mbali zaidi katika nyakati ngumu kusaidia wanawake, wanaume na watoto ambao maisha yao yanavurugwa na majanga na pia janga la COVID-19. Lakini watoa huduma za kibinadamu hivi sasa wanajaribiwa kuliko wakati mwingine wowote, wakipambana na vizingiti vya vingi kama vile kuzuiwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, pamoja na upungufu wa rasilimali kwani mahitaji yanazidi fedha iliyopo. Na mara nyingi, wanahatarisha maisha yao ili kuokoa maisha ya wengine.”

Katika kuonesha ukubwa wa changamoto wanazokutana nazo watoa huduma wa kibinadamu, OCHA imeeleza kuwa katika wiki za hivi karibuni pekee, mashambulio mabaya yamewaua wafanyakazi wa kutoa usaidizi nchini Niger na Cameroon na tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona, wafanyakazi kadhaa wameshambuliwa duniani kote.    

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na OCHA, mashambulizi makubwa dhidi ya watoa huduma za kibinadamu kwa mwaka jana yalivuka idadi ya mashambulizi ya miaka iliyopita. Jumla ya wafanyakazi 483 walishambuliwa, 125 waliuawa, 234 walijeruhiwa na 124 wakatekwa katika matukio tofautitofauti 277. Hii ikiwa ni asilimia ongezeko la asilimia 18 la idadi ikilinganishwa na mwaka 2018.  

Mratibu mkuu wa wasuala ya kibinadamu na misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock amesema, “kwa watoa huduma za kibindamu popote mnakofanya kazi muhimu na ya kijasiri katika mstari wa mbele, tunasema asante sana. Mnaokoa maisha kila siku, na changamoto mpya na majanga yakiongezea katika changamoto zilizopo tayari, uvumilivu wenu ni kishawishi na njia nzuri ya kuwaenzi watoa huduma za kibinadamu ni kwa kufadhili zaidi kazi yao na kuhakikisha usalama wao.” 

Maadhimisho ya mwaka huu ni maadhimisho ya 11 tangu siku hii ilipopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Siku hii inaangukia katika siku ambayo kulitokea shambulizi tarehe 19 Agosti mwaka 2003 katika eneo la ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Baghdad Iraq na kuua watu 22 akiwemo Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Sergio Vieira de Mello. Tangu wakati huo, karibia watoa huduma za kindamu 5,000 wameuawa, kujeruhiwa au kutekwa na katika muongo mmoja wa kati ya 2010 hadi 2019 kumeshuhudiwa ongezeko la asilimia 117 la mashambulizi ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2000 hadi 2009.