Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaomba milioni 73 tuweze kuwapatia chakula wakimbizi na wakimbizi wa ndani Ethiopia

Watoto waliokimbia makazi yao kutokana na migogoro na ukame, wakiwa katika Mkoa wa Afar, Ethiopia.
© UNICEF/UN0639245/Sewunet
Watoto waliokimbia makazi yao kutokana na migogoro na ukame, wakiwa katika Mkoa wa Afar, Ethiopia.

Tunaomba milioni 73 tuweze kuwapatia chakula wakimbizi na wakimbizi wa ndani Ethiopia

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Ethiopia wametoa ombi la dola milioni 73 ili kuweza kuendelea na utoaji wa msaada wa chakula kwa wakimbizi 750,000 walioko nchini humo katika kipindi cha miezi sita ijayo. 

Taarifa kutoka Addis Ababa nchini Ethiopia imeyataja mashirika hayo kuwa ni lile la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP, linalihudumia wakimbizi UNHCR yanayoshirikiana na lile la serikali ya Ethiopia la kuhudumia wakimbizi na waliorejea kutoka ughaibuni RRS. 

Taarifa hiyo imefafanua kuwa ifikapo mwezi October WFP haitakuwa na chakula kabisa hali itakayowaacha maelfu ya familia katika hali ya hatari kwakuwa wanategemea chakula hicho cha msaada ili kuweza kuishi. 

Mwakilishi wa WFP nchini Ethiopia Claude Jibidar amesema “robo tatu ya wakimbizi wataachwa bila chakula ufadhili usipopatikana mara moja, kuendelea kukatwa kwa fedha kunatuweka kwenye wasiwasi maana wakimbizi wengi wanaweza kufikiria kurejea katika maeneo yao ya asili ambayo si salama.”

Mkuu huyo wa WFP anawasiwasi huo kutokaa na ukweli kwamba kupunguzwa kwa mgao wa chakula nchini humo kulianza mwezi Novemba 2015 kwa asilimia 15, mwezi Novemba 2021 chakula kilipunguzwa kwa asilimia 40 na mwezi June mwaka huu 2022 mgao umepunguzwa mpaka asilimia 50.

 FAO na washirika wake waliwasilisha tani 262 za mbolea katika eneo la Tigray nchini Ethiopia kusaidia uzalishaji wa chakula.
© FAO/Michael Tewelde
FAO na washirika wake waliwasilisha tani 262 za mbolea katika eneo la Tigray nchini Ethiopia kusaidia uzalishaji wa chakula.

Utafiti baada ya mgao kupunguzwa 

Kutokana na upungufu wa fedha wa muda mrefu, WFP tayari imelazimika kupunguza mgao kwa wakimbizi 750,000 waliosajiliwa wanaoishi katika kambi 22 na maeneo matano katika jumuiya zinazowahifadhi katika mikoa ya Afar, Amhara, Benishangul-Gumuz, Gambella, Somalia na Tigray.

Ili kutambua athari zilizoletwa na kuendelea kupunguzwa kwa mgao wa chakula na kutambua usalama wa chakula na hali ya kijamii na kiuchumi ya wakimbizi mashirika hayo WFP, UNHCR na RRS walifanya tathmini katika kambi za Afar, Beneshangul- Gumuz, Gambella na Mkoa wa Somalia na kuhoji kaya 1,215. 

Matokeo yanaonyesha kuwa kaya nyingi zaidi ziliendelea kuchukua mikakati hasi ya kukabiliana na hali hiyo kwa kupunguza idadi ya milo inayoliwa kwa siku, kutumia vyakula vya bei ya chini au visivyopendelewa sana, au kupunguza sehemu ya milo inayotolewa.

Kaya zaidi zimeripotiwa kujihusisha na vitendo vya udhalilishaji, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha watoto katika shughuli za kuwaongezea kipato, ukusanyaji na uuzaji wa kuni, huku kadhaa zikikopa fedha, zikitegemea marafiki au ndugu kwa chakula. 

Hali hii inawalazimu wakimbizi kutegemea rasilimali za jumuiya inayowakaribisha na mazingira wanayoishi ambayo pia huongeza uwezekano wa migogoro inayotokana na rasilimali kati ya wakimbizi na jumuiya zinazowapokea.

Naibu mwakilishi wa UNHCR nchini Ethiopia Margaret Atieno amesema pamoja na kushukuru wafadhili waliotoa msaada mpaka sasa lakini ufadhili zaidi unahitaji kwa haraka kwakuwa hali ilivyo sasa wana wasiwasi mkuubwa kuhusu ukosefu wa chakula kwa wakimbizi 

“Kuendelea kukosekana kwa mgao kamili kwa ajili ya wakimbizi pamoja na athari za ukame mbaya zaidi kuwahi kutoke anchini humu katika kipindi cha miaka 40 kutadhoofisha sana mafanikio yaliyopatikana katika ulinzi wa wakimbizi na hatari ya kuathiri Maisha ya amani yaliyopo baina ya wenyeji na wakimbizi.”

Familia ikiwa katika mkoa wa Somali nchini Ethiopia wakijenga makazi ya muda baada ya kukimbia makazi yao ya asili
© UNFPA Ethiopia/Paula Seijo
Familia ikiwa katika mkoa wa Somali nchini Ethiopia wakijenga makazi ya muda baada ya kukimbia makazi yao ya asili

Hali itakuwa mbaya baina ya wenyeji na wakimbizi 

Ethiopia inawahifadhi wakimbizi na wasaka hifadhi zaidi ya milioni moja. Wengi wao wanatoka nchi za Sudan Kusini, Somalia, Eritrea na Sudan. Kati ya wakimbizi hao, takriban 750,000 wanategemea moja kwa moja msaada wa chakula unaotolewa na mashirika ya kibinadamu.

RRS inasimamia usambazaji wa msaada wa chakula na pesa taslimu kwa wakimbizi kwa njia ya uwajibikaji na uwazi zaidi kwa mujibu wa hifadhidata ya kibayometriki.

Mkurugenzi wa RSS Tesfahun Gobezay amesema nchi yake ya Ethiopia “pamoja na sera na ahadi zake za wakimbizi, imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kuwa wakimbizi na jumuiya zinazowahifadhi wanajitegemea kwa uendelevu kwakutumia rasilimali zake chache huku ikipambana na mapungufu ya ufadhili ya mara kwa mara kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.”

Gobezay anasema hali inayoendelea sasa ya kukatwa kwa mfuko wa jumla wa msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi nchini Ethiopia katika miaka ya hivi karibuni sio tu kumeathiri mahitaji ya kimsingi ya wakimbizi, lakini pia kumezuia utegemezi endelevu uliokusudiwa wa muda mrefu na kuishi pamoja kwa wakimbizi na jamii zinazowapokea.