Hatua za kupambana na COVID-19 Sudan zaathiri misaada ya kibinadamu:OCHA

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA leo limesema hatua za kupambana na kusambaa kwa virusi vya Corona , COVID-19 zinaathiri fursa, ufikishaji wa misaada na huduma za kibinadamu nchini Sudan.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi msemaji wa OCHA, Jens Laerke amesema “Wagonjwa saba vikiwemo vifo viwili vimethibitishwa na, wagonjwa wote waliwasili Sudan kutoka nje na sasa wanapatiwa matibabu katika vituo maalum vya kujitenga mjini Khartoum.”
Kwa mujibu wa OCHA hatua hizo za kukabiliana na corona ni pamoja na kutotembea hovyo kuanzia saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi, kufungwa kwa shule kwa mwezi mmoja kuanzia katikati ya mwezi Machin a kupunguzwa kwa wafanyakazi katika baadhi ya ofisi muhimu za serikali.
Umoja wa Mataifa na wadau mashirika yasiyo ya kiserikali NGO’s wanaweka mipango mbadala ya kuhakikisha kuendelea kwa utoaji wa msaada wa kibinadamu na kupunguza athari kwa watu ambao tayari wameathirika na hawajiwezi.
OCHA inasema “Kuna jumla ya watu milioni 9.2 wanaohitaji msaada nchini Sudsan na watu hao wanajumuisha wakimbizi na wakimbizi wa ndani karibu milioni 3. “
Kwa mujibu wa shirika hilo kuanzia mwezi huu wa Aprili mathalani washirika wanapanga kuanza kutoa mgao wa chakubwa wa miezi 2-3 kwa mara moja.
Hii itasaidia kupunguza mikusanyiko ya mara kwa mara ya watu na kuwa na uwezekano wa kusambaa kwa virusi vya Corona.
Na ili kupunguza hatari ya maambukizi kwa Watoto wenye utapiamlo OCHA inasema kutakuwa na ongezeko la ugawaji wa lishe ambayo ni chakula kilichokisha pikwa tayari kwa kuliwa na itasaidia kupunguza safari za wataalam kwenye vituo vya lishe.
Pia “Muongozo mpya na utaratibu vinaandaliwa kuhakikisha kwamba wahudumu wa afya wanaweza kuendelea kutoa chanjo, lishe na kuhakikisha mipango ya lishe kwa Watoto na Watoto wachanga katika wakati huu wa changamoto mpya.”
Kwa mujibu wa shirika hilo shughuli zote zinazohusisha mikusanyiko ya watu ikiwemo mafunzo, warsha, mikutano na kampeni za uelimishaji kuhusu ukatili wa kijinsia zimesitishwa.
Hatahivyo “udhibiti wa kesi binafsi, ushauri nasaha, rufaa na huduma za faragha kwa manusura wa ukatili wa kijinsia vinaendelea”.
Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA limeonya kwamba marugfuku za watu kutembea na kusalia nyumbani zitawaweka wanawake katika hatari zaidi ya dhuluma na ukatili majumbani.
Katika jimbo la Blue Nile mashirika ya misaada ya kibinadamu yameanzisha mipango ya kuongeza maafira na ujuzi kwa wahudumu wa afya kuweza kukabiliana na COVID-19.
Pia wataelimisha jamii kuhusu kujikinga na kufuatilia vituo ambavyo watu wanawasili kwenye jimbo hilo kusaidia kubaini na kuwatenga wanaoshukiwa kuwa na virusi hivyo.
Nako Darfur Kusini wizara ya afya imetenga vituo viwili vywa kuwaweka waathirika na inapeleka mashineza kubaini ugonjwa huo na vifaa vya kujikinga.
Kwa sasa kampeni za uelimishaji zinaendelea Darfur Kusini kwa kusambaza vipeperushi, mabango na ujumbe kupitia Radio na runinga.