Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA yatangaza washindi 10 wa miradi ya kuwawezesha wanawake na wasichana

Wasichana na wavulana kutoka kituo cha vijana mjini Nairobi, Kenya wakielezea fikra kuhusu mustakhbali wao kupitia Facebook wakati UNFPA ilipotembelea eneo lao. Na njia hii inasaidia kufanikisha SDGs. ( Maktaba)
UNFPA/Roar Bakke (maktaba)
Wasichana na wavulana kutoka kituo cha vijana mjini Nairobi, Kenya wakielezea fikra kuhusu mustakhbali wao kupitia Facebook wakati UNFPA ilipotembelea eneo lao. Na njia hii inasaidia kufanikisha SDGs. ( Maktaba)

UNFPA yatangaza washindi 10 wa miradi ya kuwawezesha wanawake na wasichana

Wanawake

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, leo limetaja washindi 10 wa pamoja wa shindano la miradi bunifu inayoweza kuleta mabadiliko chanya na kuwezesha wanawake na wasichana duniani. 

Taarifa ya washindi hao imechapishwa kwenye wavuti wa UNFPA ambayo imefafanua kuwa washindi hao wamepatikana baada ya mchujo wa washiriki 300 kutoka nchi 61 waliotuma maombi na kisha kuchujwa mpaka kupatikana 20 na leo wamepatikana 10 ambao walikuwa wanaendesha miradi midogo midogo lakini sasa kwa Ushindi huo wataweza kupanua miradi yao kwakuwa kila mmoja atapokea kitita cha dola 60,000 kwa ajili ya uwekezaji. 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt.Natalia Kanem amesema kufikiri kwa ubunifu na ufumbuzi wa kibunifu ni muhimu ili kuharakisha maendeleo kwa wanawake na wasichana duniani kote.

“UNFPA inafuraha kusaidia kundi hilo la wajasiriamali wenye nguvu na mawazo ya kubadili mchezo . Tunashukuru kwa ufadhili wa fedha kutoka Serikali za Luxembourg, Finland, na Denmark, sasa miradi ya kubadilisha maisha kama hii inawezekana.” Amesema Dkt Kanem.

Washindi 10

Kati ya washindi hao 10  waliotangazwa wanne wanatoka Afrika katika nchi za Uganda, Rwanda, Cameroon na Nigeria. Nchi nyingine sita ni Costa Rica, Mongolia, Armenia, Colombia, Bangladesh na Uturuki. 

Kutoka Uganda, Global Pre-Eclampsia Initiative  wamebuni kifaa kinachobeba mjamzito na kumwezesha kufuatilia shinikizo la damu ambalo ni changamoto kubwa kwa kundi hilo, Hillspring Diagnostics, Nigeria wamebuni mbinu ya kubaini mapema ujauzito uliotunga kwenye mirija ya uzazi, Urukundo Initiative, Rwanda: wamebuni mchezo wa ubao unaoelimisha kuhusu haki za uzazi na kutoka Cameroon wamebuni mfumo wa kuwaunganisha manusura na walio hatarini kukumbwa na ukatili wa kijinsia. 

Miradi hii yote ipo chini ya ufadhili wa mfuko wa kuharakisha usawa wa UNFPA na unatekelezwa na kwa ushirikiano na Shirika la Haki Miliki Duniani WIPO, Muungano wa Muungano wa kimataifa wa mawasiliano ITU na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC), 

Kusoma kwa undani kuhusu miradi iliyoshinda kutoka kila nchi bofya hapa

Kujua zaidi kuhusu mashindano haya yaliyotoa washindi bofya hapa