Skip to main content
Ukosefu wa taarifa au uelewa kuhusu ngono na afya ya uzazi umechangia msichna wa miaka 18 kupata mimba isiyo tarajiwa huko Timor Leste

Nusu ya mimba zote duniani hazikutarajiwa: UNFPA

© UNFPA/Ruth Carr
Ukosefu wa taarifa au uelewa kuhusu ngono na afya ya uzazi umechangia msichna wa miaka 18 kupata mimba isiyo tarajiwa huko Timor Leste

Nusu ya mimba zote duniani hazikutarajiwa: UNFPA

Wanawake

Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani mwaka 2022, iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA inasema karibu nusu ya mimba zote, ambazo ni jumla ya milioni 121 kila mwaka duniani kote, hazikutarajiwa. 

Ripoti hiyo kwa jina "Kuona Yasiyoonekana: Kuchukua hatua katika janga lililopuuzwa la mimba zisizotarajiwa," imezinduliwa jijini New York Marekani ambapo imeeleza kwa wanawake na wasichana walioathiriwa na mimba zisizotarajiwa, chaguo hili kubwa zaidi la uzazi maishani la kwamba iwapo wanataka kuwa na ujauzito au la huwa siyo chaguo lao binafsi.

“Ripoti hii ituamshe kutoka usingizini. Idadi kubwa ya mimba zisizotarajiwa inaonesha kushindwa duniani kote kutetea haki za kimsingi za wanawake na wasichana,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dk. Natalia Kanem.

UNFPA imeonya kwamba mgogoro huu wa haki za binadamu una madhara makubwa kwa jamii, wanawake na wasichana na afya ya kimataifa kwakuwa zaidi ya asilimia 60 ya mimba zisizotarajiwa huishia katika utoaji mimba na inakadiriwa asilimia 45 ya mimba zote si salama, na kusababisha asilimia 5 mpaka13 ya vifo vya uzazi, hivyo kuwa na athari kubwa katika uwezo wa dunia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs.

UNFPA inatumia njia mpya na zakibunifu ya kueneza jumbe muhimu za kijamii kwa vijana.
UN India/Zainab Dehgamwala
UNFPA inatumia njia mpya na zakibunifu ya kueneza jumbe muhimu za kijamii kwa vijana.

Ukraine na Afghanistan

Vita nchini Ukraine na machafuko katika maeneo mingine duniani kote inatarajiwa kusababisha ongezeko la mimba zisizotarajiwa, kwani upatikanaji wa huduma ya uzazi wa mpango unatatizika na unyanyasaji wa kingono ukiongezeka.

“Ikiwa ungekuwa na dakika 15 kuondoka nyumbani kwako, ungechukua nini? Je, ungenyakua pasi yako ya kusafiria? Chakula? Je, unakumbuka dawa zako za uzazi wa mpango?" Aliuliza Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dk.Natalia Kanem. 

Dkt. Kanem ameongeza kuwa “Katika siku, wiki na miezi baada ya magafuko kuanza, huduma za afya ya uzazi na ulinzi huokoa maisha, hulinda wanawake na wasichana kutokana na madhara na kuzuia mimba zisizotarajiwa. Huduma hizi ni muhimu kama vile chakula, maji na malazi.”

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNFPA amesema tafiti zingine zinaonesha zaidi ya asilimia 20 ya wanawake na wasichana wakimbizi watakabiliwa na ukatili wa kijinsia. 

Nchini Afghanistan, vita na usumbufu wa mifumo ya afya vinatarajiwa kusababisha wastani wa mimba milioni 4.8 zisizotarajiwa kufikia 2025, ambayo itahatarisha utulivu wa jumla wa nchi, amani na kurejea katika hali yake ya awali.

Licha ya kupata mimba isiyotarajiwa, msichana Tineja nchini Thailand ameazimia kuingia Chuo Kikuu.
© UNFPA/Ruth Carr
Licha ya kupata mimba isiyotarajiwa, msichana Tineja nchini Thailand ameazimia kuingia Chuo Kikuu.

Mambo yaliyoibuliwa kwenye utafiti 

Ukosefu wa usawa wa kijinsia na maendeleo huchangia kwa viwango vya juu wanawake na wasichana kupata mimba zisizotarajiwa Ulimwenguni kote, inakadiriwa wanawake milioni 257 ambao wanataka kuepuka mimba hawatumii njia salama na za kisasa za uzazi wa mpango. 

Katika maeneo ambapo takwimu hazikupatikana, karibu robo ya wanawake wote hawatumii njia salama za uzazi wa mpango. Jingine kubwa lililobainika ni wanawake kutokuwa na uwezo wa kusema hapana kwa ngono.

Klabu ya vijana wakike ikitoa mafunzo ya kipekee chini ya Mpango wa Maendeleo Jumuishi wa UNFPA.
UNFPA India
Klabu ya vijana wakike ikitoa mafunzo ya kipekee chini ya Mpango wa Maendeleo Jumuishi wa UNFPA.

Sababu nyingine nyingi zimebainishwa katika ripoti hiyo, ikiwa ni pamoja na:

  •  Ukosefu wa taarifa za huduma ya afya ya ngono na uzazi 
  •  Njia za uzazi wa mpango ambazo haziendani na miili ya wanawake au hali zao
  •  Mtazamo wa kuhukumu au aibu katika kupata huduma za afya
  • Umaskini na maendeleo ya kiuchumi yaliyokwama 

Nini kifanyike?

Wito umetolewa kwa watoa maamuzi na mifumo ya afya kuweka kipaumbele katika uzuiaji wa mimba zisizotarajiwa kwa kuboresha upatikanaji wa aina mbalimbali za uzazi wa mpango na kupanua kwa kiasi kikubwa huduma bora ya afya ya ngono na taarifa za masuala ya uzazi wa mpango. 

Watunga sera, viongozi wa jamii na watu wote wamehimizwa kuwawezesha wanawake na wasichana kufanya maamuzi kuhusu ngono, uzazi wa mpango na uzazi kwa ujumla, na kuhakikisha wanakuza jamii zinazotambua thamani kamili ya wanawake na wasichana kwakuwa wakifanya hivyo wataweza kuchangia kikamilifu katika jamii, na watakuwa na zana, taarifa na uwezo wa kufanya maamuzi yao wenyewe.

Kiujumla ripoti hii ya UNFPA inaonesha jinsi haki za kimsingi zaidi za wanawake na wasichana zinavyo kosekana wakati hakuna amani na katikati ya vita. 
Unaweza kusoma ripoti hii kamili iliwa katika lugha tano kwa kubofya hapa.