Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 25 ya ICPD wakati wa kumpa mwanamke chaguo:UN

Mtoa huduma azungumza kuhusu afya ya uzazi na wanaume na wanawake.
Diana Nambatya/Photoshare
Mtoa huduma azungumza kuhusu afya ya uzazi na wanaume na wanawake.

Miaka 25 ya ICPD wakati wa kumpa mwanamke chaguo:UN

Wanawake

Leo ni siku ya idadi ya watu duniani na mwaka huu Umoja wa Mataifa unajikita na miaka 25 baada ya mkutano wa kihistoria wa kimataifa kuhusu idadi ya watu na maendeleo uliofanyika mjini Cairo Misri mwaka 1994 (ICPD) ambapo serikali 179 ziliafikiana kwamba afya ya uzazi ni msingi kwa maendeleo endelevu.

Katika ujumbe wake wa siku hii mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA Dkt. Natalia Kanem amesema baada ya miaka 25 “Tukitaka kuboresha Maisha ya wanawake, na matarajio ya mafanikio ya nchi zao basi umewadia wakati wa kupanua wigo wa chaguo la uzazi wa mpango kwa kundi hilo. Mwanamke ana haki ya kufanya maamuzi kuhusu endapo, lini na kwa muda gani apate ujauzito na haki hiyo ilithibitishwa mwaka 1994. Ni Maisha yake, chaguo lake na mustakabali wetu”.

Dkt. Kanem ameongeza kuwa mjini Cairo viongozi wa dunia waliutafakari mustakabali ambao kila ujauzito unapangwa kwa sababu kila mwanamke na kila msichana atakuwa na mamlaka kuhusu mwili wake na kuweza kuchagua endapo ni lini na ni nani atakayezaa naye watoto.

Pia mkutano huo ulifikiria ulimwengu ambao hakuna mwanamke ambaye atakufa wakati akijifungua bila kujali mahali aliko au hali yake ya kijamii na kiuchumi anapaswa kuwa na fursa ya huduma bora za afya ya uzazi.

Kwa mujibu wa Bi. Kanem mkutano wa ICPD ulifikiria wakati ambao kila mtu ataishi kwa usalama, uhuru dhidi ya ukatili, kuheshimiwa na utu na dunia ambayo hakuna msichana anayeshinikizwa kuolewa au kuketetwa.

Visu vya mangariba sasa vitasalia butu kwa kuwa watoto wa kike, wanawake na jamii zimefunguka macho juu ya madhara ya ukeketeaji au FGM.
UNICEF/Holt
Visu vya mangariba sasa vitasalia butu kwa kuwa watoto wa kike, wanawake na jamii zimefunguka macho juu ya madhara ya ukeketeaji au FGM.

Hatua zilizopigwa tangu 1994

Tangu mwaka 1994 taarifa hiyo ya mkuu wa UNFPA inasema serikali, wanaharakati, mashirika ya asasi za kiraia na taasisi kama UNFPA zimekuwa mstari wa mbele kupigania program ya hatua na kuahidi kukomesha vikwazo ambavyo vimekuwepo baina ya wanawake na wasicha na afya zao, haki zao na uwezo wao wa kupanga mustakbali wao.

Hata hivyo amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika miaka 25 iliyopita “bado tuna safari ndefu ya kutimiza ahadi ya Cairo. Wanawake na wasichana wengi wanaendelea kuachwa nyuma na wengi bado hawawezi kufurahia haki zao.”

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15, akiwa na binti yake ambaye alijifungua baada ya kunajisiwa na wapiganaji wa Boko Haram waliomteka na kumtia ujauzito
UNICEF/UN0118457/
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15, akiwa na binti yake ambaye alijifungua baada ya kunajisiwa na wapiganaji wa Boko Haram waliomteka na kumtia ujauzito

Zaidi ya wanawake na wasichana milioni 200 wanataka kuchelewa au kuzuia kupata ujauzito lakini hawana njia yoyote ya kufanya hivyo, na UNFPA inasema wale wamasikini zaidi, jamii ya watu wa asili, wanawake wa vijijini, jamii zilizotengwa na wale wanaoishi na ulemavu ndio wanakabiliwa na pengo kubwa katika huduma.

Hivyo amesema “Ni wakati wa kuchukua hatua kuhakikisha kwamba kila mwanamke na msichana anaweza kufurahia haki zake. Kwa kuwepo na wigo mpana wa chaguo ya njia za uzazi wa mpango wanaweza kushamiri kama wadau sawa katika maendeleo endelevu.Gharama ya kutochukua hatua ni kubwa mno, ni kwamba wanawake na wasichana zaidi watakufa, mimba zaidi zisizotarajiwa, utoaji mimba usio salama utaongezeka, wasichana wengi wataacha shule kwa sababu ya ujauzito na uwezo wa watu binafsi na jamii utadidimia. Hakuna muda wa kupoteza mustakabali wetu unategemea hilo”

Baada ya kuolewa akiwa na umri wa miaka 14, mumewe alimtelekeza baada ya yeye kushika ujauzito.
© UNICEF/Noorani
Baada ya kuolewa akiwa na umri wa miaka 14, mumewe alimtelekeza baada ya yeye kushika ujauzito.

Juhudi zinazofanyika

Dkt. Kanem amesema UNFPA inashirikiana kwa karibu na serikali na wadau wengine kuhakikisha kunakuwa na dunia iliyofikiriwa miaka 25 iliyopita na kwa kuhakikisha mambo matatu muhimu yanatimizwa ifikapo 2030 kutimiza mahitaji yote ya uzazi wa mpango, kuhakikisha hakuna vifo vinavyozuilika vya kina mama wakati wa kujifungua na kutokomeza kabisa ukatili wa kijinsia na mila potofu kama ndoa za utotoni na ukeketaji au FGM na takwimu sahihi ndizo zitakazosaidia kutimiza hilo kwa kupeka msaada kunakohitajika.

Ameongeza kuwa katika mkutano utakaoitishwa na Denmark, Kenya na UNFPA mwezi Novemba mwaka huu jumuiya ya kimataifa itakuwa na fursa ya kutimiza ahadi ilizoziweka Cairo na kubadili dunia kwa kuhakikisha haki hizo si ndoto tena kwa wanawake na wasichana.

“Katika siku hii ya idadi ya watu duniani natoa wito kwetu sote, serikali, asasi za kiraia, jamii na watu kutoka kila sekta na aina ya maisha kuwa na msimamo na ujasiri wa kufanya lililo haki kwa wanawake na wasichana kote duniani ili kukamilisha kazi iliyoanza Cairo ya kuhakikisha haki ya chaguo la afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana inatimizwa. Wanawake na wasichan hawawezi kusubiri. Nchi na jamii haziwezi kusubiri, wakati wa kuchukua hatua kutimiza ahadi tulizoziweka na kuhakikisha afya ya uzazi wa mpango ni sasa.”