Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shehena ya kwanza ya nafaka yaondoka Ukraine: UN yapongeza

Meli ya M/V Razoni inasafiri kutoka bandari ya Odesa kufuatia uidhinishaji wa Kituo cha Uratibu wa Pamoja (JCC), kilichoanzishwa chini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.
OCHA/Saviano Abreu
Meli ya M/V Razoni inasafiri kutoka bandari ya Odesa kufuatia uidhinishaji wa Kituo cha Uratibu wa Pamoja (JCC), kilichoanzishwa chini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.

Shehena ya kwanza ya nafaka yaondoka Ukraine: UN yapongeza

Masuala ya UM

Hatimaye meli ya kwanza yenye shehena ya tani elf 26 za mahindi imeondoka leo katika bandari ya Odesa nchini Ukraine ikielekea Tripoli nchini Lebanon ikiwa ni kuanza utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa tarehe 22 Julai mwaka huu baina ya Urusi na Ukraine chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. 

Akitoa taarifa rasmi ya kuanza safari kwa meli hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewaambia waandishi wa Habari akiwa jijini New York Marekani kuwa meli hiyo “The Merchant Vessel Razoni” imebeba bidhaa mbili muhimu na adimu duniani ambazo ni Mahindi na Amani. 

Gutteres ameeleza kwa mujibu wa mkataba alioushuhudia ukisainiwa nchini Uturuki wiki mbili zilizopita meli hiyo ya kwanza kuondoka Odesa tangu mara ya mwisho February 26 mwaka huu “Itawasili eneo la ukaguzi nchini Uturuki hapo kesho. Na baada ya ukaguzi itaendelea na safari yake hadi Tripoli nchini Lebanon, nchi yenye utegemezi mkubwa wa nafaka kutoka nje ya nchi.”

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema imekuwa safari ndefu ya mapendekezo aliyoyatoa kwa viongozi wa Urusi na Ukraine mwezi April” Kuondoka kwa meli hii ni mwanzo imara wa matokeo ya Mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi” ameeleza pia ni matumaini kwa mamilio ya watu duniani kote wanaotegemea uendeshaji usio na bughudha wa bandari ya Ukraine ili waweze kulisha familia zao.

“Kuondoka kwa leo ni mafanikio makubwa ya pamoja ya yanayotekelezwa na Kituo cha Uratibu kilichoanzishwa wiki iliyopita mjini Istanbul (Uturuki) chini ya ufadhili wa Umoja wa Mataifa, na wawakilishi kutoka Ukraine, Urusi, na Uturuki. Makundi yote yanafanya kazi kwa bidii kufikia hatua hii muhimu, kwa msaada waUmoja wa Mataifa na Uturuki.”

Katibu Mkuu António Guterres akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi na usafirishaji wa kwanza wa nafaka kutoka Ukraine.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu António Guterres akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi na usafirishaji wa kwanza wa nafaka kutoka Ukraine.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema Mpango huo wa Nafaka wa Bahari Nyeusi utaruhusu usambazaji wa kiasi kikubwa nje ya nchi kupitia  bandari tatu za Ukraine ambazo ni Odesa, Chornomorsk na Yuzhny. 

Makubaliano yaliyosainiwa nchini Uturuki pia yalitaka kuwepo na usambazaji wa mbolea kutoka nchini Urusi kwenda soko la kimataifa itasaidia kuleta ahueni na utulivu kwenye soko la chakula na kusaidia kushighulikia tatizo la chakula ulimwenguni.

Guterres amesema “Kuhakikisha kuna nafaka, mbolea na bidhaa nyingine za chakula katika bei nzuri inayoridhisha kwa nchi zinazoendelea ni jambo la lazima na la kibinadamu. Watu walio katika njaa wanahitaji hii mikataba ifanye kazi ili waweze kuishi. Nchi zilizo katika hatihati ya kufilisika zinahitaji mikataba hii kufanya kazi ili waweze kuweka uchumi wao hai.” 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametangaza shirika la Umoja wa Matafa la Mpango wa chakula duniani WFP katika kuonesha mshikamano wa kibinadamu limepanga kununua tangu 30,000 za awali za ngano kutoka Ukraine  kwenye meli iliyokodishwa na Umoja wa Mataifa. 

Umoja wa Mataifa umeeleza kufanya kazi kila siku ili kuleta nafuu kwa watu wa Ukraine, na kwa wale wote wanaoteseka na madhara ya migogoro duniani kote. “Vita hivi lazima viishe, na amani lazima ianzishwe, kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.” Ameeleza wakati akihitimisha hotuba yake Katibu Mkuu Guterres