Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimaye meli yenye shehena ya ngano yaondoka Ukraine kuelekea Pembe ya Afrika

Mwelekeo wa shehena za vyakula kutoka Ukraine.
UN News
Mwelekeo wa shehena za vyakula kutoka Ukraine.

Hatimaye meli yenye shehena ya ngano yaondoka Ukraine kuelekea Pembe ya Afrika

Msaada wa Kibinadamu

Meli ya kwanza ya Ukraine yenye na unga wa ngano wa Ukraine utakaosambazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP kwenye operesheni zake za kibinadamu imeondoka bandari ya Yuzhny nchini Ukraine hii leo,  hatua ambayo imetajwa kuwa ya muhimu zaidi na inayohitajika ya kuondoa nafaka kwenye taifa hilo lenye mzozo kuelekea nchi zinazokumbwa na janga la uhaba wa chakula duniani. 

WFP ikipakia shehena ya ngano kwenye meli
© WFP/Anastasiia Honcharuk
WFP ikipakia shehena ya ngano kwenye meli

 

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo kwenye miji ya Yuzhny Ukraine na Roma Italia inasema meli hiyo imebeba tani elfu 23 za ngano na zinapelekwa Pembe ya Afrika ambako ukame umesababisha mamilioni ya familia kutokuwa na uhakika wa chakula.

WFP inasema eneo hilo ni ambalo kukaribia kukoma kupatikana kwa ngano na chakula kutoka Ukraine, kwenye soko la dunia kumesababisha maisha kuwa maguu kwa familia ambazo tayari zilikuwa zinakabiliwa na njaa.

Mkurugenzi Mkuu wa WFP David Beasley akizungumzia hatua ya kuondoka kwa meli hiyo amesema “kitendo cha bandari katika Bahari Nyeusi kuanza kufanya kazi ni moja ya jambo sahihi zaidi kufanyika wakati huu ili kusaidia wale walio na njaa zaidi ulimwenguni hivi sasa. Itahitajika meli nyingi zaidi kutoka Ukraine ili kukomesha njaa, lakini kitendo cha nafaka za Ukraine kurejea kwenye soko la dunia tuna fursa ya kukomesha janga la chakula duniani ili lisiendelee kusambaa.”

Hali ya uhaba wa chakula duniani

Kwa sasa watu milioni 345 katika nchi 82 duniani wana uhaba mkubwa wa chakula ilhali watu milioni 50 katika nchi 45 wako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa iwapo hawatapatiwa msaada wa kibinadamu.
Kurejea kwa safari za meli za kibiashara na kibinadamu kutoka Ukraine kupitia Bahari Nyeusi kunaweza kuleta ahueni kwenye mnyororo wa safari za meli zinazobeba shehena za vyakula na nafaka kwenye ukanda huo kuelekea maeneo mengine duniani. Halikadhalika kutasaidia kuondoa shehena za nafaka kwenye bohari za Ukraine wakati huu ambapo mavuno ya msimu wa kiangazi yanakabiria.

Meli ya kwanza ya kibiashara  M/V Fulmar S, ikiwa inaelekea Ukraine kutoka Uturuki kupitia mpango wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi.
UNOCHA/Levent Kulu
Meli ya kwanza ya kibiashara M/V Fulmar S, ikiwa inaelekea Ukraine kutoka Uturuki kupitia mpango wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi.

Idadi ya Meli na Shehena kupitia Bahari Nyeusi

Safari za meli za shehena za nafaka kutoka Ukraine zinaratibiwa na Kituo cha Pamoja cha Uratibu, JCC kilichozinduliwa huko Istanbul, Uturuki tarehe 27 mwezi uliopita wa Julai baada ya uzinduzi wa Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi baina ya Urusi, Uturuki, Ukraine na Umoja wa Mataifa.

Tangu tarehe 1 hadi 15 mwezi huu wa Agosti, JCC imeidhinisha safari za meli 36, 21 zikitoka Ukraine zikiwa na shehena na 15 zikielekea Ukraine kuchukua shehena wakati huu ambapo bado uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unaendelea.

Meli hizo kupitia njia iliyoruhusiwa ya kupitisha kwa usalama misaada ya kiutu kwenye bahari Nyeusi zinabeba kutoka bandari za Ukraine shehena za nafaka, vyakula na mbolea.

Bandari hizo za Ukraine na idadi ya meli ambazo zimeshaondoka na shehena ni Odesa (11) , Chornomorsk (6)  na  Yuzhny (4)  ijulikanayo pia kama Pivdennyi.

Meli hizo zilichukua tani 563,317 za nafaka na vyakula vinginevyo - JCC

Taarifa kutoka JCC imesema maeneo ya awali ambako vyakula hivyo kutoka Ukraine kwa ajili ya mauzo ni pamoja na Uturuki, Iran, Korea Kusini, China, Ireland, Italia, Djibouti, Romania. 
Meli inayoelekea Djibouti ina chakula kilichonunuliwa na WFP kusaidia wanaokumbwa na njaa nchini Ethiopia.

JCC inakagua meli zinazoingia na kutoka Ukraine na tangu tarehe 1 hadi 15 mwezi huu imekagua meli 27 na zote zimeidhinishwa kupita.