Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvamizi wa vituo vya UN DRC; Walinda amani 3 wauawa

Magari haya ya kivita ya kubeba askari wa Tanzania huko DR Congo.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Magari haya ya kivita ya kubeba askari wa Tanzania huko DR Congo.

Uvamizi wa vituo vya UN DRC; Walinda amani 3 wauawa

Amani na Usalama

Huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mlinda amani askari wa kulinda amani na polisi  wawili wa Umoja wa Mataifa wameuawa baada ya waandamanaji kuvamia kituo cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MONUSCO huko Butembo na kupora silaha za polisi wa kitaifa na kuanza mashambulizi.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa Habari jijini New York, Marekani hii leo kwamba polisi mwingine amejeruhiwa.

“Tunaongeza sauti yetu kwa Kaimu Mkuu wa MONUSCO, Khassim Diagne, tunalaani mauaji ya wenzetu na tunatuma salamu za rambirambi kwa familia na wafanyakazi wenzao,” amesema Bwana Haq.

Bwana Diagne katika taarifa yake ya awali ameelezea ghasia dhidi ya Umoja wa Mataifa kuwa ni jambo lisilokubalika kabisa na halina maana kwa kuzingatia mantiki ya uwepo wa chombo hicho nchini humo kushirikiana na mamlaka kulinda raia na kukabili vikundi vilivyojihami sambamba na kujengea uwezo taasisi za seriklai na na huduma.

Ametoa wito kwa mamlaka za DRC, mashirika ya kiraia, vikundi vya kjami kukataa ghasia.

Vurugu na mikanganyiko haileti amani ya kudumu

“Si katika vurugu na mkanganyiko kutaweza kupatikana maendeleo ya amani na utulivu,” amesema Bwana Diagne.

Takribani matukio manne yamelenga makazi ya wafanyakazi wa MONUSCO na wafanyakazi wengine tayari wamehamishiwa maeneo mengine.

Mapema leo kundi la watu lilijaribu uingia katika ofisi za shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo ya duniani, UNDP kwenye mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma lakini kundi hilo lilizuiwa na walinzi.

Hapo jana Umoja wa Mataifa uliripoti matukio ya mamia ya washambuliaji kuvamia vituo ya Umoja wa Mataifa mjini Goma na maeneo mengine ya jimbo la Kivu Kaskazini wakichochewa na kauli na vitisho kutoka kwa watu binafsi na makundi dhidi ya Umoja wa Mataifa.

Kikosi cha kujibu mashambulizi kiko makini

Tayari Umoja wa Mataifa unaimarisha usalama na kikosi cha kujibu mashambulizi kiko katika hadhari ya juu na kimeshauriwa kujizuia kwa kiasi kikubwa kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi tu ili kusambaratisha waandamanaji na pale inapobidi kufyatua risasi pindi mfanyakazi au mali ya Umoja wa Mataifa itakaposhambuliwa.

Kwa sasa usaidizi wa lindo la maeneo ya Umoja wa Mataifa unafanyika kwa ushirikiano na jeshi la serikali ya DRC, FARDC.