Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vurugu dhidi ya ofisi za UN DRC: Serikali kuwasaka na kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa

Naibu Mwakilisih wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC Kassim Diagne akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari 26 Julai 2022, mkutano  ulihudhuriwa pia na Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Waziri wa Habari Patrick Muyaya.
UN/Boybe Malenga
Naibu Mwakilisih wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC Kassim Diagne akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari 26 Julai 2022, mkutano ulihudhuriwa pia na Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Waziri wa Habari Patrick Muyaya.

Vurugu dhidi ya ofisi za UN DRC: Serikali kuwasaka na kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa

Amani na Usalama

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imesihi utulivu miongoni mwa wananchi baada ya maandamano na uvamizi dhidi ya vituo vya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani MONUSCO kwenye miji ya Goma na Butembo jimboni Kivu Kaskazini, tukio ambalo hata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka mamlaka zichunguze na sheria ichukue mkondo wake. Mwandishi wetu wa DRC Byobe Malenga ana taarifa zaidi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri wa habari wa DRC Patrick Muyaya katika mkutano na na waandishi wa habari uliofanyika kwenye mji mkuu Kinshasa na kuhudhuriwa na Kaimu Mkuu wa MONUSCO Kassim Diagne.

Duru mbalimbali zinadai kuwa waasi wa Maimai walikuwa miongoni mwa waandamanaji waliosababisha vifo vya walinda amani watatu wa umoja wa Mataifa katika maeneo ya Butembo jimboni Kivu Kaskazini.

Waziri Muyaya ambaye pia ni msemaji wa serikali amesema watawasaka na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria huku akisihi raia kusitisha mara moja maandamano.

Bwana Muyaya amesema ,“kulingana na hali ilivyokuwa Goma na Butembo, hadi sasa kuna idadi ya vifo 15 kukiwa wanajeshi 3 wa umoja wamataifa waliofariki Butembo na pia kuna majeruhi ya wati 61 ambao wako katika hospitali za  kivu kaskazini. Ikiwa ushirikiano wetu na Monusco itavunjika inapaswa kumaliza katika hali ya kistaarabu na serikali yetu iko katika mchakato huo. Kufanya vitendo vya uhalifu avikubaliki na tunafanya liwezekanalo kubaini wapi kulitokea hayo”

Kumekuwa na shutuma kuwa vikosi vya MONUSCO vimehusika na mauaji ya raia katika maandamano hayo lakini Kassim Diagne, Kaimu Mkuu wa MONUSCO hapa nchini amesema kuwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa sio wahusika na kwamba jukumu lao ni kulinda Amani.

Amehoji Bwana Diagne, "nani aliwapiga risasi waandamanaji hawa? Sio sisi ... "Kama tungefyatua risasi kwenye umati wawaandamanaji, tusingeweza kuwa na maiti kumi pekee, tungekuwa na mamia ya watu ambao wangekuwa maiti mida hii. kwa hiyo risasi zilizo uwa watu sijui zimetoka wapi, sisi ni Umoja wa Mataifa, hatuwezi kuwafyatulia raia risasi. Wanajeshi wetu walikuwa chini ya shinikizo kubwa, watu waliwasukuma kupita kiasi ili kufika kwenye ofisi nahata maghala yetu, n ahata waka rudi nyuma.silaha na risasi zetu zinajulikana”

Licha ya wito kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa sitisho la maandamano na mamlaka zichunguze tukio hilo, hii leo tena kumeripotiwa ya kwamba vijana wamevamia ofisi za Umoja wa Mataifa katika mji wa Uvira.

Gavana wa kijeshi wa jimbo la Kivu KaskaziniCostant Ndima amekataza maandamano yeyote dhidi ya Umoja wa Mataifa na kutaka amaji irejee.

Kwa zaidi ya miaka 20 sasa, vVikosi vya walinda amani kutoka nchi mbalimbali chini ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, vimekuwa vikiwajibika kwa kiasi kikubwa kwa lengo sio tu la kulinda na kuleta amani kwa kupigana na makundi ya waasi lakini pia kwa kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu, uchumi na kadhalika katika nchi hii ya ukanda wa Maziwa Makuu inayokumbwa na vita kwa miongo kadhaa sasa.