Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saa chache baada ya makubaliano, makombora yatua mji wa bandari wa Odesa, Ukraine- Guterres alaani

Mwanamke akipita kando mwa magunia ya mchanga yenye lengo la kuimarisha ulinzi kwenye mji wa Odesa nchini Ukraine
© UNICEF/Siegfried Modola
Mwanamke akipita kando mwa magunia ya mchanga yenye lengo la kuimarisha ulinzi kwenye mji wa Odesa nchini Ukraine

Saa chache baada ya makubaliano, makombora yatua mji wa bandari wa Odesa, Ukraine- Guterres alaani

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali ripoti za mashambulizi ya  hii leo ya makombora dhidi ya mjiwa bandari wa Odesa nchini Ukraine.

Hayo yamo kwenye taarifa iliyotololewa leo na Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq  jijini New York, Marekani.

Shambulizi hilo limetokea chini ya saa 24 tangu Urusi na Ukraine zitie saini makubaliano ya kuruhusu kuanza kusafirishwa nje ya nchi kwa nafaka na vyakula kutoka Ukraine kupitia bandari Nyeusi.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa makombora mawili yalipiga mji wa Odesa nyakati za alfajiri ya Jumamosi licha ya Urusi kupitia makubaliano ya jana kukubali kuwa haitolenga bandari wakati shehena za nafaka zikiwa kwenye  maandalizi ya kusafirishwa.

Taarifa imemnukuu Katibu Mkuu akisema ,”jana pande zote zilieleza bayana mbele ya dunia nzima kuhakikisha usafirishaji salama wa nafaka na bidhaa nyingine kwenda soko la dunia.”

Guterres amesema bidhaa hizi zinahitajika mno ili kukabili janga la chakula duniani na kupunguza machungu ya mamilioni ya watu duniani kote wanaohaha kupata chakula.

“Suala la Urusi, Ukraine na Uturuki kutekeleza kwa ukamilifu makubaliano ya jana ni muhimu,” amesema Katibu Mkuu.