Pasaka ya waothodoksi Ukraine na Urusi ikikaribia, sitisheni mapigano kwa siku 4: Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa siku nne za sitisho la mashambulizi nchini Ukraine kuanzia Alhamisi ya wikii hii wakati huu ambapo wiki takatifu ya kuelekea sikukuu ya PAsaka kwa waumini wa madhehebu ya kikristo ya kiothodoksi nchini Ukraine ikianza keshokutwa Alhamisi. Ametaka sitisho hilo liendelee hadi Jumapili tarehe 24 mwezi huu kilele cha Pasaka ya kiothodoksi.
Guterres ametoa wito huo leo alipozungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mbele ya sanamu ya Bastola iliyokunjwa, yenye ujumbe wa kuachana na silaha na kusaka amani.
Amesema hali hiyo inaweza kufungua fursa ya mazungumzo na amani ili kusongesha imani na maana ya ujumbe wa Pasaka.
“Siku tano zijazo, raia wa Ukraine na Urusi wataadhimisha pasaka. Sikukuu hii inaunganisha waumini wa madhehebu ya kikristo wa kiothodoksi walioko Urusi na Ukraine, pamoja na wale wa kikatoliki. Pasaka ni msimu wa kujipanga upya, ufufuo na matumaini,” amesema Guterres.
Katibu Mkuu amesema ni wakati wa kutathmini juu ya maana ya machungu, kujitoa sadaka, kifo na kuzaliwa upya akisema huu ni wakati wa Umoja.
Guterres amesema mwaka huu, wiki takatifu inaadhimishwa chini ya wingu zito la vita linalowakilisha ukinzani kabisa na ujumbe wa Pasaka.
“Badala ya kusherehekea maisha mapya, Pasaka hii inakutana na mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine. Huu uwepo wa majeshi mengi unafanya vita hii kuwa ya kali, haribifu na inayosababisha vifo,” amesema Katibu Mkuu.
Ameongeza kuwa mashambulizi na idadi kubwa ya raia waliokufa hadi sasa kunaleta taswira ya janga lililo siku za usoni.
Katibu Mkuu amesema hawawezi kuruhusu hali hiyo itokee siku za usoni. Mamia ya maelfu ya maisha ya watu yako mashakani. “Juhudi nyingi za pande nyingi zilizofanyika kuleta sitisho la mapigano Ukraine zimegonga mwamba.”
Ni kwa mantiki hiyo amesema sitisho la mapigano kwa siku nne kutawezesha raia wanaotaka kukimbilia maeneo salama kufanya hivyo kwa uratibu wa Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, ICRC.
Pili, itatoa fursa kwa operesheni za kibinadamu za kusambaza misaada kuendelea kufanyika kwa usalama hasa kwenye maeneo yaliyo hatarini zaidi ya Mariupol, Kherson, Donetsk na Luhansk.
Amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kupeleka misafara yenye misaada ya kibinadamu wakati wa kipindi hicho kwenye maeneo hayo, akisema “tunapelekea wadau wetu mipango mahsusi.”
Zaidi ya watu milioni 12 wanahitaji misaada ya kibinadamu nchini Ukraine. Miongoni mwao, theluthi moja wako Mariupol, Kherson, Donetsk na Luhansk.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa idadi hiyo itafikia milioni 15.7 sawa na asilimia 40 ya raia wa Ukraine waliokimbia nchi yao.
Hadi sasa, kwa mujibu wa Guterres, watu wapatao milioni 2.5 wamepata misaada ya kibinadamu katika wiki chache zilizopita, wengi wao wakiwa mashariki mwa Ukraine.
“Kwa wengi wao sasa hali waliyo nayo ni kifo au uhai. Natoa wito kwa warusi na waukraine waweke silaha chini na kusongesha mazingira ya amani kwa ajili ya wengi walio hatarini.
Guterres amesema kipindi cha siku 4 cha Pasaka kinapaswa kuwa fursa ya kuungana na kuokoa maisha na kusongesha mazungumzo ya kumaliza machungu nchini Ukraine.