Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita Ukraine yasababisha uhaba wa Oksijeni itumikayo kutibu wagonjwa - WHO

Bibi akmhudumia mjukuu wake kwenye hospitali ya watoto mjini Kyiv nchini Ukraine
© UNICEF/Oleksander Ratushniak
Bibi akmhudumia mjukuu wake kwenye hospitali ya watoto mjini Kyiv nchini Ukraine

Vita Ukraine yasababisha uhaba wa Oksijeni itumikayo kutibu wagonjwa - WHO

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo tena limekutana kujadili vitisho vya amani na usalama duniani ikijikita zaidi katika uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ambapo Mkuu wa Idara ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo amesema dalili nzuri zilizoonekana wiki hii kufuatia mazungumzo kati ya wawakilishi wa mataifa hayo mawili bado hazijazaa matunda yoyote.
 

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini New York, Marekani, Bi. DiCarlo amesema pamoja na kuunga mkono mazungumzo hayo bado “dalili hizo chanya hazijweza kufanikisha kumalizwa kwa chuki, jambo ambalo linasubiriwa kwa hamu.

“Hali kwenye mji wa bandari wa Mariupol ndio inatia wasiwasi zaidi. Wakazi wengi wa eneo hilo hawajaweza kuondoka wanakabiliwa na uhaba wa chakula, maji, umeme na huduma za matibabu,” amesema Bi. DiCarlo.

Maiti wamesambazaa mitaani Mariupol

Cha kusikitisha zaidi amesema maiti wamesambaa kwenye mitaa, na shambulio la jana linaripotiwa kufanyika kwenye ukumbi wa filamu mjini humo unaotumika kama eneo la kujificha kwa raia, linaongeza idadi ya maeneo ya kiraia yaliyoshambuliwa.

Amesema kipaumbele cha Umoja wa Mataifa sasa na wadau wake ni kufikia watu walionasa kwenye mashambulizi yanayoendelea ikiwemo Mashariki mwa Ukraine.
Hata hivyo amepongeza nchi jirani ambazo zinaendelea kufungua mipaka na kupatia hifadhi wakimbizi kutoka Ukraine.

Wanawake kutoka Ukraine wakitembea mbele ya mahema yaliyosimikwa huko Medyka nchini Poland kusaidia wakimbizi.
© Daniele Aguzzoli
Wanawake kutoka Ukraine wakitembea mbele ya mahema yaliyosimikwa huko Medyka nchini Poland kusaidia wakimbizi.

Poland yapitisha kanuni mpya za uhamiaji

Akizungumzia suala la kupokea wakimbizi, Mwakilishi wa kudumu wa Poland kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Krzysztof Szczerski, amesema tayari serikali ya nchi yake imechukua hatua za dharura kwa kupitisha kanuni mpya za uhamiaji kwa raia wa Ukraine wanaokimbia mapigano nchini mwao.

“Sheria mpya imeanza Jumatatu, na inaruhusu raia wa Ukraine kuishi Poland ili waweze kufanya kazi na pia inawapatia haki ya huduma ya afya, elimu na malazi,” amesema Balozi Szczerski.

Halikadhalika inapatia msaada wa fedha kwa raia wa Poland ambao wanakaribisha wakimbizi kwenye nyumba zao huku serikali ikitenga fungu la shule kwa ajili ya wanafunzi wa Ukraine.
Ameeleza kuwa Poland itaendelea kusaidia raia wa Ukraine wanaokimbia machungu ya vita yaliyosababishwa na Urusi.

Uhaba wa Oksijeni wakabili Ukraine

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akihutubia kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi baada ya kueleza madhara ya vita hivyo ikiwemo kupungua kwa Oksijeni ya maji inayohitajika hivi sasa kwa ajili ya wagonjwa ikiwemo wake wale wa COVID-19, alikuwa na maombi makuu matatu.

Mosi, Baraza la Usalama lifanye kazi ili mapigano yasitishwe na suluhu ya kisiasa ipatikane; Pili, wahisani wasaidie kuchangia mahitaji ya kibinadamu nchini Ukraine na nchi Jirani zinazopokea wakimbizi na tatu, pamoja na kwamba hivi sasa suala la Ukraine ndio linapatiwa msisitizo, “nasihi sote tusisahau majanga mengine yanayoendelea ambako watu wanakumbwa na machungu; Afghanistan, Ethiopia, Yemen na Syria.”

Wajumbe wa Baraza pia walipata taarifa kutoka kwa Kamishna Msaidizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR . Raouf Mazou ambaye naye pia alihutubia kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi.

Bwana Mazou amesema ili UNHCR iweze kufanya kwa ufanisi kazi yake ya kusambaza misaada ya kuokoa maisha nchini Ukraine, imelazimika kurekebisha utekelezaji wa operesheni zake kwa kuhamishia ofisi na mabohari yake kuelekea maeneo ya kati na magharibi mwa  Ukraine.

“Sisi na wadau wetu tumeweza tumeweza kusambaza misaada na vifaa muhimu kwa wakimbizi wa  ndani na raia walioathiriwa na vita, ikiwemo vifaa kama vile mahema,” ametanabaisha Bwana Mazou.