Nelson Mandela alikuwa mponyaji wa jamii:Guterres
Nelson Mandela alikuwa mponyaji wa jamii:Guterres
Wakati dunia hii leo ikiadhimisha siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kiongozi huyo wa zamani wa Afrika Kusini ameonyesha kila mtu kila mahali anao uwezo na wajibu wa kujenga maisha bora ya baadae ya wote.
Nelson Mandela kwa jina jingine Madiba, Rais wa kwanza Mweusi wa Afrika Kusini aliyeshika madaraka mwaka 1994 kuongoza taifa hilo baada ya kukaa miaka 27 gerezani, lakini alivyotoka hakuweka kisasi kwa wale waliomsweka ndani sababu ya harakati zake za kugombania uhuru wa taifa hilo.
Uongozi na falsafa zake zimevutia dunia mpaka Umoja wa Mataifa kutenga siku ya leo Julai 18 maalum kama siku ya Nelson Mandela na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii kwa njia ya amemsifu Mandela kuwa ni mtu bora wa wakati wote, kiongozi aliyekuwa na ujasiri pasi na kifani ambaye alikuwa na mafanikio makubwa, mwenye utulivu na ubinadamu wa kina.
“Nelson Mandela alikuwa mponyaji wa jamii na mshauri kwa vizazi na vizazi. Anabaki kuwa dira ya maadili na kumbukumbu kwetu sote.”
Katibu Mkuu Guterres amesema wakati huu dunia ikiwa imegubikwa na changamoto lukuki kuanzia kwenye vita, masuala ya haki za binadamu, majanga ya dunia, mabadiliko ya tabianchi, umasikini, na ubaguzi, njia bora ya kutatua changamoto hizi pamoja na mambo mengine, ni kukumbatia urithi ulioachwa na Madiba ambao ni kupaza sauti dhidi ya chuki na kutetea haki za binadamu.
“Kwa kukumbatia ubinadamu wetu wa kawaida ambao ni utajiri wa utofauti wetu, usawa kwa heshima, umoja katika mshikamano. Na kwa pamoja kuifanya dunia yetu kuwa ya haki zaidi, yenye huruma, yenye mafanikio, na endelevu kwa wote.”