Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maisha ya Nelson Mandela yanatufundisha kuchagua utu – Rais wa Baraza Kuu la UN 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela, 2022. Kutoka kushoto kwenda kulia: Meghan na Prince Harry, Duchess na Duke wa Sussex; Mondli Gungubele, Waziri katika Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini; Maria Theofili, Mwakili
Picha ya UN/Mark Garten
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela, 2022. Kutoka kushoto kwenda kulia: Meghan na Prince Harry, Duchess na Duke wa Sussex; Mondli Gungubele, Waziri katika Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini; Maria Theofili, Mwakili

Maisha ya Nelson Mandela yanatufundisha kuchagua utu – Rais wa Baraza Kuu la UN 

Masuala ya UM

Ili kuadhimisha siku ya kimataifa ya Nelson Mandela, Umoja wa Mataifa umefaya tukio maalum katika ukumbi wa Baraza Kuu, katika makao makuu ya umoja huo jijini New York Marekani ambapo Rais wa Baraza wa sasa, Abdulla Shahid, ameangazia maisha ya Mandela kama utafutaji usio na kuchoka wa "usawa na uhuru kwa wote". 

Bwana Shahid ametumia maneno ya Hayati Madiba na kusisitiza kuwa, "hakuna mtu anayezaliwa akimchukia mtu mwingine kwa sababu ya rangi ya ngozi yake, asili yake au dini yake" na akasisitiza zaidi kuwa vita yake ilikuwa ni kwa ajili ya utu wa watu wote. 

"Wakati wa mtikisiko, maisha ya Madiba yanatufundisha kuchagua utu badala ya kudhalilisha, kupaza sauti wakati wa dhuluma, na kusamehe badala ya chuki." Amesema rais huyo wa Baraza Kuu.  

Suluhu ya matatizo inategemea haki 

Kwa Bwana Shahid, maisha ya Mandela ni ushuhuda kwamba utatuzi endelevu wa migogoro unahitaji zaidi ya kukomesha ghasia; inategemea haki na huruma, kama ilivyowekwa wazi na Tume ya Ukweli na Upatanisho ambayo iliundwa nchini Afrika Kusini ili kukuza upatanisho na msamaha kati ya wahalifu na waathiriwa wa ubaguzi wa rangi. 

“Tume ilifanya kazi kwa msingi kwamba katika makabiliano haya ya binadamu kati ya wema na uovu, ubaya wa mhalifu utafichuliwa kwa jamii na utu wa muathiriwa utakuwepo.” Ameendelea kuweka wazi Bwana Shahid. 

Usawa wa kijinsia 

Aidha, Shahid ameangazia kazi ya Mandela katika kuunga mkono usawa wa kijinsia alipotambua alipokuwa rais kwamba hakuna mafanikio yanayowezekana bila usawa kwa wanawake. 

"Madiba alikuwa na maoni kwamba mradi wanawake wamefungamana na umaskini na mradi tu wanadharauliwa, haki za binadamu zitakosa umuhimu." alisisitiza. 

Vilevile tabia ya Mandela ya uanamazingira pia imejitokeza katika hafla hii ya kumkubuka,  huku Rais wa Baraza Kuu , Bwana Shahid akidokeza maono yake kwamba dunia inapaswa kuwa mahali ambapo watu wote wanaweza kuishi maisha "katika hadhi kamili, yenye hewa safi ya kupumua na maji safi." safi kunywa”. 

Mjukuu wa Malkia  

Prince Harry, Mjukuu wa Malkia Elizabeth wa Uingerza, alikuwepo kwenye hafla ya Baraza Kuu hii leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku ya kimataifa ya Nelson Mandela, na akatumia sehemu ya hotuba yake akilaani kwamba "tunashuhudia shambulio la kimataifa dhidi ya demokrasia na uhuru, jambo ambalo Mandela alijitolea maisha yake.”  

Prince Harry ambaye ameambatana na mkewe, Meghan amehakikisha kwamba tunaishi katika "wakati muhimu" ambapo majanga mengi yanayobadilika, kama vile Covid-19, mabadiliko ya tabianchi na habari potofu, yamesababisha "msururu usio na mwisho wa dhuluma", na ambayo watu wa kawaida wanapata maumivu ya ajabu. 

Janga hili, amesema Prince Harry, litazidi kuwa baya zaidi "isipokuwa viongozi wetu waongoze" na nchi zinazowakilishwa katika Umoja wa Mataifa "zifanye maamuzi ya ujasiri na ya kuleta mabadiliko ambayo ulimwengu wetu unahitaji kuokoa ubinadamu." 

“Maamuzi haya yanaweza yasiendane na ajenda za vyama vyote vya siasa. Wanaweza kuamsha upinzani kutokana na masilahi yenye nguvu. Lakini nini cha kufanya haina mjadala. Na wala sio sayansi. Swali pekee ni iwapo tutakuwa wajasiri wa kutosha na wenye hekima ya kutosha kufanya kile kinachohitajika.” Amesisitiza Prince Harry akiongeza kuomba kufuata ushauri ambao Mandela aliwahi kumpa mwanawe wa kiume: “Usikate tamaa ya kupigana, hata katika saa ya giza zaidi.” 

Naibu Katibu Mkuu UN

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, akihutubia hafla ya ametoa wito kwa kila mtu kuheshimu urithi wa Nelson Mandela kwa kuchukua hatua. 

Akisoma ujumbe wa Katibu Mkuu, Bi. Mohammed amesema, "leo na kila siku, tuheshimu urithi wa Nelson Mandela kwa kuchukua hatua. Kwa kupaza sauti dhidi ya chuki na kutetea haki za binadamu. Kwa kukumbatia ubinadamu wetu wa kawaida, matajiri katika utofauti, sawa kwa heshima, umoja katika mshikamano. Na kwa pamoja kuifanya dunia yetu kuwa ya haki zaidi, yenye huruma, yenye mafanikio, na endelevu kwa wote.” 

Meya wa New York

Kwa upande wake, Meya wa Jiji la New York Eric Adams amesema, "majanga yanayoendelea ya COVID, vita, na uhalifu vimetufunga katika magereza yetu ya Kisiwa cha Robben. Lakini haya ni masharti ya muda. Sio kifungo cha maisha. Hadithi yangu ya kibinafsi ni taswira ya hilo. Nilikuwa na Dyslexia (matatizo ambayo yanahusisha ugumu wa kujifunza kusoma au kufasiri maneno, herufi na alama nyingine, lakini ambayo haiathiri akili ya jumla) na nilinyimwa huduma za usaidizi nikiwa mtoto. Nilikamatwa nikiwa kijana na nilihisi nimekataliwa kuwa mtu, lakini nilijua haukuwa mwisho, wala si kizuizi. Na leo nasimama mbele yenu nikiwa na nguvu kwa ajili ya yote ambayo nimevumilia katika safari yangu pia.”