Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumuenzi Madiba kwa kuzidisha mshikamano: Guterres

Siku ya Kimataifa ya  Nelson Mandela inatambua alivyopigania demokrasia na utamaduni wa amani kwa ulimwengu wote
Unsplash/John-Paul Henry
Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela inatambua alivyopigania demokrasia na utamaduni wa amani kwa ulimwengu wote

Tumuenzi Madiba kwa kuzidisha mshikamano: Guterres

Masuala ya UM

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya Nelson Mandela, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amewasihi watu wote ulimwenguni kumkumbuka na kumuenzi Mandela kwa kutafakari juu ya utu, usawa, haki, na haki za binadamu. 

Katika ujumbe wake wa siku hii kupitia vyombo vya habari akiwa New York, Marekani Guterres amesema, Nelson Mandela au kwajina lingine Madiba ambaye alikuwa rais wa Afrika Kusini alipenda na kuhimiza mshikamo na kukomesha ubaguzi wa rangi, jambo ambalo sasa lipo hatarini kwani mshikamo wa kijamii ulimwenguni kote unatishiwa na mgawanyiko.

“Kila mwaka, katika siku hii, siku ya kuzaliwa ya Nelson Mandela, tunamshukuru mtu huyu wa ajabu ambaye alijumuisha matakwa ya juu zaidi ya Umoja wa Mataifa na ulimwengu. Tumeshuhudia sasa jamii zikizidi kuparaganyika, lugha za matusi na uongo zimeongezeka, habari zinazofifisha ukweli, kuhoji sayansi na kudhoofisha taasisi za kidemokrasia.”

Amesema janga linaloendelea la COVID-19 limechangia kurudisha nyumba maendeleo na vita dhidi ya umasikini lakini pia katika kipindi cha matatizo ni wale ambao wapo kwenye makundi yenye kuhitaji msaada ndio wanaoteseka zaidi, na mara nyingi ndio hulaumiwa ilihali hawana hatia kwa yaliyotokea. 

“ Janga hilo la Corona limeonesha  umuhimu wa mshikamano na umoja, maadili yaliyopigiwa chepuo na Nelson Mandela katika kipindi chake chote cha uhai akipigania haki.”

“Hakuna aliye salama mpaka wote tuwe salama. Na kila mmoja wetu ana jukumu la kufanya.” Ameongeza Guterres katika ujumbe wake huo. 
Amehitimisha kwa kusema watu wote wanatakiwa kuhamasika na ujumbe wa Madiba kwamba kila mtu anaweza kuleta madiliko katika kutangaza amani, haki za binadamu, maelewano na utu kwa watu wote.

“katika kuenzi maisha ya Madiba , tuheshimu wito wake na kuchukua hatua na kutiwanguvu na urithi aliotuachia.”