Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nini kifanyike kupunguza pengo la uwakilishi wa wanawake katika nafasi za umma na siasa?

Leonida Zurita, aliteuliwa kuwa Rais wa Chama cha Wawakilishi wa Idara za Wanawake wa Jimbo la Plurinational la Bolivia (AMADBOL), ambacho kiliundwa kwa usaidizi wa kiteknolojia na kifedha kutoka kwa UN Women.
© UN Women/David Villegas Zambrana
Leonida Zurita, aliteuliwa kuwa Rais wa Chama cha Wawakilishi wa Idara za Wanawake wa Jimbo la Plurinational la Bolivia (AMADBOL), ambacho kiliundwa kwa usaidizi wa kiteknolojia na kifedha kutoka kwa UN Women.

Nini kifanyike kupunguza pengo la uwakilishi wa wanawake katika nafasi za umma na siasa?

Wanawake

Itachukua miaka 155 kwa wanawake kufanikiwa kuondoa pengo la kushiriki kikamilifu katika masuala ya  umma na kisiasa. 

Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk katika taarifa yake aliyoitoa hii leo jijini Geneva Uswisi akitoa wito wa ushiriki sawa na wenye maana wa wanawake katika maisha ya umma na kisiasa. 

“Mfumo dume lazima iwe ni jambo la kizamani. Mustakabali wetu unategemea wanawake na wasichana kuwa mezani kila mahali maamuzi yanapofanywa,” alisema Kamishna Türk.

Kamishna Mkuu huyu wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia mwaka jana ndio wabunge waliwakilishwa katika kila bunge linalofanya kazi duniani. 

Hata hivyo mpaka sasa takwimu zinaonesha bado, mbunge mmoja tu kati ya wanne ni mwanawake. Hii ikimaanisha iwapo mambo hayatabadilika, itachukua miaka 155 kwa wanawake kuziba pengo la kijinsia. Na hali ni mbaya zaidi kwa wanawake wa jamaii za asili ambao uwakilishi wao ni mdogo zaidi.  

Kamishna Turk amesema takwimu hii iwe kama simu iliyopigwa kuamsha jamii “Usawa hauwezi kusubiri. Ushiriki sawa na wa maana wa wanawake katika utendaji si tu kuhusu haki za wanawake kusikilizwa, ni kuhusu uwezo wa jamii zetu kukabiliana na matatizo makubwa zaidi yanayoikabili dunia yetu leo.” 

Ameeleza ni muhimu kwa jamii zote ulimwenguni kutumia uwezo kamili na mchango wa pamoja wa wananchi wote katika kuchukua hatua madhubuti kulinda sayari dunia, kupata amani ya kudumu, na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs.

Je hatua gani zichukuliwe kumaliza pengo hili?

Kamishna Mkuu Volker Türk amezitaka nchi, wabunge, vyombo vya habari, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na kila mmoja wetu kuchukua hatua zifuatazo ili kuweza kufikia usawa na ushiriki kikamilifu na wenye maana wa wanawake katika masuala ya umma na kisiasa:

  1. Kukabiliana na mizizi ya ubaguzi wa kijinsia, hii ikijumuisha kanuni za kijamii, ambazo zinapunguza ushiriki wa wanawake na wasichana katika maisha ya umma na ya kisiasa. Mbinu zakutumia ni pamoja na kutoa elimu na kampeni za kukuza ufahamu.
  2. Kuwathamini, kuwatambua na uwepo wa mgawanyo mpya wa kazi za matunzo hususan ya familia ambazo hazina malipo na mara nyingi zinaonekana kuwahusu zaidi wanawake.
  3. Kuzingatia viwango, kutenga viti maalum na fursa za mafunzo ili kuongeza uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya kutunga sheria, na taasisi nyingine muhimu za maisha ya kisiasa na ya umma, na pia katika sekta ya kibinafsi.
  4. Kufanya kazi ili kufikia usawa wa kijinsia katika mashirika ya Umoja wa Mataifa ya mkataba wa haki za binadamu.
  5. Kuanzishwe kanuni za maadili na taratibu za kuripoti kwa lengo la kutovumilia ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake katika siasa, ikiwa ni pamoja na mtandaoni.
  6. Kuwatangaza wanawake wanaoweza kuwa mifano ya kuigwa kwa jamii na kuhakikisha wanapewa fursa ya kuonekana zaidi kutokana na michango yao wanayotoa.