Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN WOMEN kushirikiana na FIFA katika Kombe la Dunia la wanawake

Kathely Rosa, mwenye umri wa miaka 19 (kati awkiwa na mpira) akiwa na wahitimu wengine wa "One Win Leads to another", programu wa michezo nchini Brazil.
UN Women/Camille Miranda
Kathely Rosa, mwenye umri wa miaka 19 (kati awkiwa na mpira) akiwa na wahitimu wengine wa "One Win Leads to another", programu wa michezo nchini Brazil.

UN WOMEN kushirikiana na FIFA katika Kombe la Dunia la wanawake

Wanawake

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN WOMEN linashirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA katika mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA la wanawake yanayoanza tarehe 20 Julai mpaka 20 Agosti 2023 huko nchini Australia na New Zealand ambayo yanatarajiwa kutazamwa na zaidi ya watu bilioni mbili duniani kote, ikiwa ni hadhira kubwa zaidi katika historia ya mchezo mmoja wa wanawake. 

Taarifa iliyotolewa leo na UN Women kutoka New York nchini Marekani imesema malengo ya ushirikiano huo ni kusherehekea ujuzi na mafanikio ya timu na wachezaji, kuendeleza usawa wa kijinsia katika soka, na kuzuia unyanyasaji na ubaguzi ndani na nje ya uwanja.

Lisa Zimuuche, mchezaji kijana wa kulipwa mweneye uraia wa Algeria na Ufaransa. Katika Jukwaa la Vijana, alielezea umuhimu wa wanawake katika michezo
ONU Info/Florence Westergard
Lisa Zimuuche, mchezaji kijana wa kulipwa mweneye uraia wa Algeria na Ufaransa. Katika Jukwaa la Vijana, alielezea umuhimu wa wanawake katika michezo

Chini ya mwavuli huo wa ushirikiano mashirika hayo yanatoa wito wa masuala mawili makuu. 

Mosi, “Kuunga Mkono Usawa wa Kijinsia” – Lengo ni kutambua usawa wa kijinsia kama haki ya msingi ya binadamu na muhimu kwa ulimwengu wa amani na endelevu. 

Pili “Kuungana kwa ajili ya Kukomesha Ukatili dhidi ya Wanawake”- Lengo ni kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana kama ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani kote.

“Wanawake wanaoshindana katika Kombe hili la Dunia ni mifano ya kuigwa kwa kila msichana kwenye sayari hii”, amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women Sima Bahous.

Ameongeza kuwa mashindano hayo ni ukumbusho kwamba kuna wanawake na wasichana wengi sana ambao wametengwa na ulimwengu wa michezo, na kwamba hata kwa wale wanaoshiriki mara nyingi hukumbana na ubaguzi na, hata katika baadhi ya matukio, unyanyasaji. 

“Kombe la Dunia la Wanawake linatuonesha ni kwa kiasi gani si wao tu bali dunia nzima inakosa wakati tunaposhindwa kumudu kutoa fursa sawa kwa wanawake na wasichana fursa sawa kama zitolewavyo kwa wanaume na wavulana.” Amesema Mkuu huyo wa UN WOMEN.

Melodie Donchet (Ufaransa), bingwa mara nne wa kombe la dunia la mpira wa miguu akifanya maonyesho ya ujuzi wake. (Maktaba)
UNESCO/Christelle ALIX
Melodie Donchet (Ufaransa), bingwa mara nne wa kombe la dunia la mpira wa miguu akifanya maonyesho ya ujuzi wake. (Maktaba)

Maeneo watakayo shirikiana

Ushirikiano huo wa UN WOMEN na FIFA utahusisha kampeni ya kimataifa ya ‘Soka Inaunganisha Dunia’, unaolenga kuonesha dhamira na nia ya dhati ya kushughulikia hilo kwa manufaa ya kila mtu.

Miito miwili ya kuchukua hatua kuhusu usawa wa kijinsia itakuwa ikipigiwa chepuo kupitia kwa manahodha wa kila timu kupitia kitambaa cha unahodha wa timu.

Maeneo ya matangazo katika mbao za pembeni ndani ya uwanja yatawekwa matangazo hayo, kutakuwa na bendera kubwa zitakazooneshwa uwanjani, runinga kubwa viwanjani, na kupitia mitandao ya kijamii. 

"Unganeni kwa Usawa wa Jinsia" utakuwa ujumbe utakaoangaziwa siku 3 (30 Julai - 3 Agosti 2023) na "Unganeni Kukomesha Unyanyasaji dhidi ya Wanawake" utakuwa ujumbe ulioteuliwa wakati wa Nusu Fainali (16 Agosti 2023).

Mashirika mengine matano ya Umoja wa Mataifa yamejiunga na kampeni hiyo ya “Mpira unaunganisha dunia” kwa lugha ya kiingereza "Football Unites the World" ikiwa ni pamoja na lile la Elimu Sayansi na Utamaduni - UNESCO, la masuala ya wakimbizi UNHCR, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, Mpango wa Chakula Duniani- WFP, na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO.