Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiswahili ni lugha ya uhuru, amani, umoja na Maendeleo: Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia kwa njia ya video washiriki wa maadhimisho ya kwanza ya siku ya Kiswahili Duniani kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani.
UN Video
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia kwa njia ya video washiriki wa maadhimisho ya kwanza ya siku ya Kiswahili Duniani kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani.

Kiswahili ni lugha ya uhuru, amani, umoja na Maendeleo: Rais Samia

Masuala ya UM

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameupongeza ubalozi wa kudumu wa Tanzania nchini Marekani na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kwa kaundaa maadhimisho makubwa ya kwanza ya Siku ya Kimataifa ya Kiswahili duniani na kusema kuwa wameitendea haki lugha hiyo amabayo ni alama ya uhuru, amani na Umoja.

Akiwahutumia wahudhuriaji wa maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani Samia amesema “Mmefanya kazi kubwa na nzuri ya kukipa nguvu Kiswahili, asanteni sana”

Lugha ya Uhuru

Akifafanua kwanini ameiita lugha ya Kiswahili kuwa ni ya Uhuru, Rais Samia amesema “Msishangae kwanini nimeihusisha siku hii na uhuru Amani na Umoja, nimefanya hivyo kwasababu Kiswahili kilitumika kama lugha ya ukombozi has akusini mwa Afrika na hivyo ilichangia sana kuleta uhuru na umoja.”

Pia ameeleza namna lugha hiyo ilivyotumika kujenga umoja wa kitaifa na mshikamano na kutatua migogoro katika ukanda wa Afrika mashariki, kati na kusini. 

Akizungumzia Kiswahili na Malengo ya Maendeleo endelevu ya umoja wa Mataifa SDGs Rais huyo wa Tanzania amesema lugha hii ni nyenzo muhimu kwenye utekelezaji wa malengo hayo ya SDGs ifikapo mwaka 2030 na agenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063. 

“Jamhuri ya muungano wa Tanzania iliunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa lenye namba A/76/L57 la mwezi Mei mwaka 2022 kuhusu lugha nyingi yani Multilingualism ambalo lilisisitiza  umuhimu wa Umoja wa Mataifa kuzipa kipaumbele lugha ambazo sio rasmi katika Umoja huo kama vile Kiswahili hii ni kwa kuhakikisha lugha kama vile Kiswahili inawafikia watu wengi zaidi duniani.” Ameeza Rais Samia. 

UN News/Anold Kayanda
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ahutubia maadhimisho ya kwanza ya Kiswahili Duniani.

 Amesema maadhimisho hayo yataendelea kuadhimishwa kila mwaka kama ishara ya kutambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano ya Kimataifa inayokuza ushirikiano wenye mchango katika nyanja mbalimbali za amani, umoja na maendeleo ya mwanadamu.

Amewasihi watanzania kuitumia lugha na siku hii kutangaza utamaduni wao.

Ukuaji kwa kasi 

Lugha ya Kiswahili ni moja la lugha zinazokuwa kwa kasi duniani, ni moja la lugha 10 zinazo zungumzwa zaidi duniani na watu wasiopungua milioni 200 na inafundishwa katika vyuo vikuu vikubwa vingi duniani. 

Lugha hii pia inatumika katika vituo vya redio televisheni na vituo mbalimbali vya kutangazia duniani. Mfano wa vyombo hivyo ni pamoja na Redio ya Kimataifa ya China CRI m na Japan NHK. 

Kiswahili ni lugha ya kwanza la Afrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa kupitia UNESCO ambao ndio waliotenga tarehe 07 mwezi Julai kuwa siku ya kuadhimishwa Kimataifa. 

Aidha Kiswahili ndio lugha ya kwanza ya Afrika kutumika katika shughuli rasmi za Umoja wa Afrika AU, Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika SADC, na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.