Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi tatu zaidi Afrika zagundua kuwa na wagonjwa wa Monkeypox

Picha iliyokuzwa sana inaonesha chembe ya virusi aina ya mulberry kirusi cha Monkeypox ambayo ilipatikana kwenye umajimaji wa malengelenge ya binadamu.
© CDC
Picha iliyokuzwa sana inaonesha chembe ya virusi aina ya mulberry kirusi cha Monkeypox ambayo ilipatikana kwenye umajimaji wa malengelenge ya binadamu.

Nchi tatu zaidi Afrika zagundua kuwa na wagonjwa wa Monkeypox

Afya

Wakati nchi tatu ambazo awali hazikuwa na historia ya kuwa na ugonjwa wa ndui ya nyani au Monkeypox zikiripoti kuwa na wagonjwa katika mataifa yao, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO kanda ya Afrika imetangaza kuanza kufanya kazi na mataifa ya Afrika katika kuimarisha uwezo wa nchi kufanya uchunguzi wa kimaabara ili kubaini wagonjwa hao kwa haraka na kuzuia kuenea kimya kimya kwa ugonjwa huo.

Taarifa kutoka mjini Brazaville, nchini Congo iliyotolewa na Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Motshidiso Moeti imesema mpaka sasa shirika hilo linafanya kazi n anchi za Afrika ili kuhakikisha wanapata vipimo 60,000, na kati ya hivyo wanatarajia vitendanishi 2000 kuvielekeza kwenda nchi zilizo hatarini zaidi na 1000 katika nchi zenye hatari ndogo.

“Takwimu za mpaka tarehe 28 Juni 2022 zinaonesha jumla ya nchi 13 barani Afrika zimeripoti kuwa na wagonjwa 1821 kutoka maabara 109 ndani ya nchi 9.” Amesema Dkt Moeti na kuzitaja nchi 3 zilizoripoti kuwa na wagonjwa wa Monkeypox kuwa ni Afrika Kusini, Ghana na Morocco ambazo wagonjwa hawana historia ya kusafiri nje ya nchi hali inayo onesha kuna kusambaa kwa ugonjwa huo ndani ya nchi kimya kimya.

Idadi ya wagonjwa Barani Afrika ni asilimia 2 ya wagonjwa zaidi ya 4500 waliogundulika duniani kute. 
Nchi ya Jamhuri ya Kidemorasi Congo DRC ikiongoza kuwa na takriban asilimia 81 ya wagonjwa wote waliogundulika barani Afrika na hii ikiamsha hari ya uhitaji wa kuongeza nguvu kwenye maabara kwa haraka ili kuweza kugundua wagonjwa wapya kwa haraka. 

Mkurugenzi wa shirika la afya duniani, WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moet.
UN News/ Video Capture
Mkurugenzi wa shirika la afya duniani, WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moet.

Akizungumzia sababu za kutaka kuimarisha maabara za Afrika, Dkt Moeti amesema “Kuenea kijiografia kwa wagonjwa wa Monkeypox katika nchi za Afrika ambazo awali hazikuwahi kuwa na wagonjwa hao kunatia shaka. Ni muhimu tuunge mkono juhudi za kitaifa za kuongeza uchunguzi wa kimaabara ambao ndio msingi wa udhibiti wa magonjwa.”

WHO Afrika imesema suala la kuongeza nguvu kwa haraka kwenye maabara ili kugundua kwa haraka wagonjwa ni muhimu kwasasa wakitolea mfano janga la COVID-19 kuwa nchi za Afrika zilichelewa kuimarisha uchunguzi kwa haraka na hivyo ugonjwa kusambaa kwa kasi jambo ambalo hawataki litokee tena sasa hivi kwenye ugonjwa wa Monkeypox. 

Kuhusu chanjo ya ugonjwa huo WHO inashauri kutumika kwa chanjo ya ndui lakini kutosambazwa kwa jamii kwa ujumla na badala yake wazingatie maeneo yanayo onesha uhitaji zaidi kwasasa. 
“kilichotokea nyakati za mwanzo za utoaji wa chanjo ya COVID-19 wakati Afrika ikiangali kwa mbali nchi nyingine zikiwa zinajiandaa kwa kuchukua chanjo na vifaa vichache vilivyokuwepo ili kupambana na ugonjwa huo hakitakiwi kutokea tena.” Amesema Dkt Moeti na kuongeza kuwa “tumeanza kuona dalili za haya tayari yakifanyika mtazamo wa sasa wa Monkeypox unapaswa kuwa kichocheo cha kushinda ugonjwa huo mara moja na kwa wote katika Afrika, kwa hili tunajua chanjo ni muhimu.”


Nchi za Afrika zilizoripoti wagonjwa wa Monkeypox ni Benin, Cameroon, Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nigeria, Ghana, Afrika Kusini, Morocco, Sierra Leone, Ethiopia, Msumbiji na Sudan.