Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaripoti kuibuka kwa ugonjwa wa Monkeypox katika nchi 8 barani Ulaya

Virusi vya Monkeypox vinakaribia vile vya surua.
© CDC/Cynthia S. Goldsmith
Virusi vya Monkeypox vinakaribia vile vya surua.

WHO yaripoti kuibuka kwa ugonjwa wa Monkeypox katika nchi 8 barani Ulaya

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni kanda ya Ulaya imeripoti kuibuka kwa ugonjwa wa Monkeypox katika nchi nane barani humo.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Dkt. Hans Henri P. Kluge imetaja nchi hizo kuwa ni Ujerumani, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Italia, Ureno, Uhispania na Uingereza. 

Ugonjwa huo ambao unasababisha na virusi kutoka kwa Wanyama kwenda kwa binadamu kwa nadra hutokea katika jamii zilizopo karibu na misitu huko Afrika ya kati na Magharibi ambapo kuna hifadhi za Wanyama hata hivyo dalili za wagonjwa waliogundulika barani ulaya zina fanana na vile vilizoripotiwa siku za karibuni katika nchi za Australia, Canada na Marekani.

Akitaja sababu za kuwepo kwa ugonjwa huo Dkt.Kluge ameeleza ingawa idadi ya kesi za wagonjwa barani ulaya bado ni ndogo na ingawa na hakuna uhusiano wa watu kusafiri kutoka kwenye maeneo yanayojulikana kuwepo kwa ugonjwa huo lakini idadi inaweza kuongezeka kwakuwa matukio mengi ya wagonjwa wa Monkeypox yamegunduliwa katika kliniki maalumu za magonjwa ya zinaa.

“Kesi hizi za hivi karibuni zinatokana na sababu kadhaa. Kwanza, visa vyote vya watu wenye ugonjwa huu kasoro mtu mmoja pekee havina historia ya kusafiri kwenda maeneo ambayo ni kawaida kuwepo kwa ugonjwa huo ambapo ni Afrika Magharibi au Afrika ya Kati. Pili, kwa sababu visa vingi vya awali vimegunduliwa kupitia huduma za afya ya ngono na ni miongoni mwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume. Na tatu, kwa sababu ya hali ya kutawanywa kijiografia ya kesi kote barani ulaya na kwingineko, hii inaonesha uambukizaji unaweza kuwa unasambaa na unaendelea kwa muda.” Amefafanua mkuu huyo wa WHO Barani Ulaya.

WHO imeeleza inaendelea kufanya kazi na nchi ambazo ugonjwa huo umeibuka ili kuweza kupata taarifa zaidi na kusaidia katika ugunduzi wa kesi na matukio mengine ingawa mpaka sasa haijulikani wazi kuna kiwango gani cha maambukizi katika jamii lakini kuna uwezekano kwamba kesi zaidi zitatambuliwa katika siku zijazo.

Fahamu hukusu Ugonjwa wa Monkeypox

Ugonjwa wa Monkeypox huambukizwa kutokana na virusi na unaambukizwa wakati wa kugusana baina ya watu, (mgusano huo hutokea iwapo mtu mmoja atakuwa na vidonda kwenye ngozi, kuvuta hewa yenye matone ya mtu aliyena ugonjwa huo au maji maji ya mwilini) pia ugonjwa huo unaambukizwa kupitia kujamiiana, au kwa kugusana na nyenzo zilizoambukizwa.

“Acha nisisitize kwamba kesi nyingi zinazochunguzwa kwa sasa dalili ni ndogo na wengi wa walio ambukizwa watapona ndani ya wiki chache bila matibabu. Hata hivyo, ugonjwa unaweza kuwa mkali zaidi, hasa kwa watoto wadogo, wanawake wajawazito, na watu  ambao hawana kinga mwilini.” Amesema DKt. Kluge

Ingawa dalili za ugonjwa huo zinaweza kuwa ndogo lakini vipele vinavyotokea kwenye ngozi huwasha na kuleta maumivu.

WHO imetoa wito kwa mtu yeyote ambaye ana wasiwasi kuhusu kuwa na vipele visivyo vya kawaida kwenda hospitali kupata ushauria wa daktari au mtoa huduma wa afya.

Watu wanaohisiwa kuwa na Monkeypox wanapaswa kuchunguzwa na kutengwa na dalili za kwanza.

Nchi nyingi za ulaya zikiwa zinaingia katika msimu wa kiangazi mikusanyiko ya watu wengi, sherehe zinakuwa nyingi na hivyo “nina wasiwasi kwamba maambukizi yanaweza kuongezeka kwa haraka kwani kesi zinazogunduliwa kwa sasa ni kati ya wale wanaojihusisha na ngono, na dalili hazijulikani kwa wengi.” Amesema mkuu huyo wa WHO wakati aki hitimisha taarifa yake.