Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jina la ndui ya nyani au Monkeypox linabadilishwa kuepusha unyanyapaa- WHO

Virusi vya ndui ya nyani vinaweza kusambazwa kupitia malengelenge
© Harun Tulunay
Virusi vya ndui ya nyani vinaweza kusambazwa kupitia malengelenge

Jina la ndui ya nyani au Monkeypox linabadilishwa kuepusha unyanyapaa- WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, liko kwenye mchakato wa kubadilisha jina la ugonjwa wa ndui ya nyani au Monkeypox.

Msemaji wa WHO huko Geneva, Uswiwi, Fadéla Chaib, amethibitisha hayo alipoulizwa swali na waandishi wa habari jumanne ya Agosti 17, 2022 kuhusu mchakato huo. 
Bi. Chaib amesema ni wajibu wa WHO na mfumo wake wa kubainisha magonjwa kufanya hivyo, “hivyo katika kupatia majina magonjwa, WHO inafanya mashauriano ya wazi kupata jina jipya la ndui ya nyani.”

Amesema mtu yeyote wa kawaida, taasisi za elimu, mashirika ya kiraia anakabirishwa kupendekeza jina jipya, kuna jukwaa kwenye wavuti wa WHO ambako watu wanaweza kupendekeza majina.

Bi. Chaib amesema ni vema sana kupata jina jipya la ugonjwa wa ndui ya nyani kwa kuwa ni njia bora kutokosea kabila, ukanda, nchi au mnyama na kadhalika. Kwa hiyo WHO ina hofu kubwa juu ya hili hivyo tunatafuta jina lisilonyanyapaa.”

Kwa nini kubadili ndui ya nyani na si magonjwa mengine?

Amefafanua kuwa hadi sasa hakuna muda kamili wa kupata jina hilo na kwamba iwapo jina jipya likipatikana umma utajulishwa.

Alipoulizwa ni kwa nini jina la ndui ya nyani linaonekana kuwa linanyanyapaa na hivyo libadilishwe, Bi. Chaib amesema kwa miaka kadhaa imekuwa ni utamaduni wa WHO kuhakikisha majina ya magonjwa hayaleti unyanyapaa kwa ukanda, nchi au kabila au mnyama na kwamba kwa sasa wanamulika ndui ya nyani.

Ndui ya nyani iko tangu mwaka 1958

Ugonjwa wa ndui ya nyani uligundulika kwa mara ya kwanza mwaka 1958 na umekuwa umejikita Zaidi katika nchi za Afrika hadi mlipuko wa mwaka huu wa ndui ya nyani ambapo wagonjwa wameripotiwa nchi za Ulaya.

Tarehe 23 mwezi uliopita wa Julai, WHO ilitangaza kuwa ndui ya nyani ni dharura ya afya duniani na tishio la afya ya umma.

Kwa mujibu wa WHO, ndui ya nyani iliwekwa kwenye kundi la magonjwa ya kitropiki yanayopuuzwa, NTDs.

Bofya hapa kuwasilisha pendekezo la jina badala ya ndui ya nyani.