Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yakaribisha azimio la kupunguza kwa nusu vifo na majeruhi wa ajali barabarani ifikapo 2030

Mwanamke akivuka barabara kwa haraka
PAHO
Mwanamke akivuka barabara kwa haraka

WHO yakaribisha azimio la kupunguza kwa nusu vifo na majeruhi wa ajali barabarani ifikapo 2030

Masuala ya UM

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO limekaribisha tamko la kisiasa au azimio litakalopitishwa na nchi wanachama wakati wa mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu usalama barabarani duniani.  

Azimio hilo linajitolea kupunguza vifo na majeruhi wa ajali za barabarani kwa asilimia 50% ifikapo 2030, ambayo kwa mujibu wa WHO ni hatua muhimu kwa usalama barabarani na uhamaji endelevu.

Mkutano huo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unafanyika kuanzia leo tarehe 30 Juni hadi tarehe 1 Julai 2022 chini ya kaulimbiu "Kuufikia mwaka 2030 kwa ajili ya usalama barabarani: kupata muongo wa utekelezaji na utimizajii". 

Akizungumzia umuhimu wa kudumisha usalama barabarani mkurugenszi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema  "Usalama barabarani unaathiri kila mtu. Kila siku tunatoka majumbani mwetu kupitia barabara zinazotupeleka kwenye kazi zetu, shuleni na kukidhi mahitaji yetu muhimu ya kila siku. Hata hivyo mifumo yetu ya usafiri inasalia kuwa hatari sana. Hakuna kifo kinachopaswa kukubalika kwenye barabara zetu. Mustakabali wa usafiri unapaswa kukuza afya na ustawi, kulinda mazingira na kufaidisha wote,”  

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa suala la usalama barabarani "Iitahitaji uongozi wa mabadiliko kutoka ngazi za juu za serikali kuweza kuchukua hatua kwa Azimio la kisiasa ili kuftimiza malengo haya."  

Magari yaliyobeba abiria kupita kiasi, usafiri wa bodaboda maarufu kama 'mshikaki' kama ilivyo pichani ni chanzo cha ajali nyingi.
Benki ya Dunia/Stephan Gladieu
Magari yaliyobeba abiria kupita kiasi, usafiri wa bodaboda maarufu kama 'mshikaki' kama ilivyo pichani ni chanzo cha ajali nyingi.

Mamilioni wanakufa kwa ajali kila mwaka 

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa duniani kote ajali za barabarani zinakatili Maisha ya watu takriban amilioni ya milioni 1.3 kila mwaka ambao ni sawa na zaidi ya watu wawili kila dakika huku wengine milioni 50 wakijeruhiwa. 

Pia takwimu zimeongeza kuwa zaidi ya asilimia 90% ya vifo hivyo au vifo 9 kati ya 10 vinatokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati. 

Na wengine wanaokufa au kifo 1 kati ya vifo 4 vya ajali hizo za barabarani vinawahusu watembea kwa miguu au waendesha baiskeli. 

Azimio la Baraza Kuu 

Mkutano huu wa Baraza Kuu kuhus usalama barabarani unatokana na makubaliano ya nchi wanachama kupitia azimio nambari 75/308 na miongoni mwa wazungumzaji katika mkutano huo ni Rais wa Baraza Kuu Abdulla Shahid, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu usalama barabarani Jean Todt.