Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde ongezeni fedha tunusuru wakimbizi Burkina Faso- UNHCR

Mamia ya raia wa Burkina Faso wanaokimbia mashamnbulizi wilaya ya Seytenga nchini Burkina faso wamesaka hifadhi Niger
© CIAUD/Abdoulaye Seydou Amadou
Mamia ya raia wa Burkina Faso wanaokimbia mashamnbulizi wilaya ya Seytenga nchini Burkina faso wamesaka hifadhi Niger

Chonde chonde ongezeni fedha tunusuru wakimbizi Burkina Faso- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR lina hofu kubwa juu ya ongezeko la mashambulizi na ghasia vinavyofanywa na makundi yalioyjihami dhidi ya raia nchini Burkina Faso.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, Matthew Saltmarch amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa mashambulizi hayo  yamelazimu maelfu ya raia kukimbia makazi yao na hivyo kuweka shinikizo kwa mahitaji ya kibinadamu kwa kuwa ukosefu wa usalama unazidi kukumba ukanda wa Kati wa Sahel.

“Tangu tarehe 12  mwezi huu wa Juni, takribani raia 16,000 wa Burkina Faso wengi wao wakiwa wanawake na watoto wamewasili Dori, eneo la kaskazini-,mashariki mwa taifa hilo wakikimbia shambulizi liliofanywa eneo la Seytenga, mji ulioko kilometa 15 kutoka mpaka na Niger,” amesema Bwana Saltmarch.

Raia wengine wengi zaidi wanatarajiwa kuwasili siku zijazo, wakati huu ambapo yaripotiwa watu 360 wamevuka mpaka na kuingia eneo la mkoa wa Tillabéri nchini Niger na hivyo kuongeza idadi zaidi kwa raia wengine 15,500 wa Burkina Faso ambao tayari waliingia eneo hilo wakikimbia mashambulizi.

“Mamlaka za mji wa Tera mkoani humo pamoja na wenyeji wamekaribisha na kuwahifadhi wakimbizi licha ya kwamba familia zenyewe za wenyeji hazina uwezo wa kutosha,” amesema afisa huyo wa UNHCR.

Janga la ukimbizi wa ndani Burkina Faso linakua kwa kasi

UNHCR inasema janga la ukimbizi wa ndani Burkina Faso ni moja ya majanga yanayokua kwa kasi kubwa duniani ambapo hadi mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu kulikuweko na wakimbizi wa ndani milioni 1.9.

Shambulio la hivi karibuni zaidi lilikuwa usiku wa tarehe 11 mwezi Juni huko Seytenga ambako  takribani watu 79 waliuawa na watu wenye silaha, tukio ambalo linaripotiwa kuwa baya zaidi la mauaji ya watu wengi kwa wakati mmoja tangu tukio la Solhan mwezi Juni mwaka 2021 ambapo watu 130 waliuawa.

Wengi walishuhudia waume au baba zao wakiuawa

Wakimbizi waliowasili Dori wanasema watu wenye silaha walipita nyumba kwa nyumba kusaka na kuua watu wazima wanaume ikimaanisha kwamba, “wengi walishuhudia waume au baba zao wakiuawa. Takribani theluthi mbili za waliokimbia Seytenga wana umri wa chini ya miaka 18.

UNHCR inashirikiana na serikali kusaidia wakimbizi wa ndani Burkina Faso na wale waliokimbilia Niger lakini, “licha ya ongezeko la mahitaji, bajeti ya UNHCR yad ola milioni 109.9 kwa mwaka 2022 kusaidia operesheni hizo imefadhiliwa kwa asilimia 20 tu. Tunatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuonesha mshikamano na watu wa Burkina Faso ikiwemo kuchangia operesheni za kibinadamu za kuokoa maisha.”